Raha ya wakazi serikali ya kaunti ikiwajengea vibaraza vya kubembea baharini
WAKAZI wa kisiwa cha Lamu wamefurahishwa na hatua ya serikali ya kaunti ya Lamu ya kuwajengea vibaraza vinavyobembea kimpango ndani ya Bahari Hindi.
Vibaraza hivyo vimejengwa kwa kutundikwa kwenye ngome ya kukinga maji ya Bahari Hindi kufikia makazi ya binadamu na biashara, hasa mbele ya mji wa kale wa Lamu.
Kimtazamo, vibaraza hivyo viko ndani ya Bahari Hindi, japo vinabembea kwa juu, hivyo kuwapa wageni, watalii na wenyeji furaha na utamu wa aina yake wanapobarizi.
Wenyeji, wageni na watalii waliozungumza na Taifa Leo kisiwani Lamu hawakuficha furaha yao kufuatia ujenzi wa vibaraza hivyo.
Bi Halima Omar, mkazi wa mtaa wa Mkomani, anasema kila anapozidiwa na joto nyumbani, yeye huteremka na kujibanza kwenye mojawapo ya vibaraza hivyo ili kupata hewa safi kutoka baharini.
“Tangu vijengwe, hivi vibaraza vimetuwezesha kupata upepo mwanana wa moja kwa moja kutoka baharini. Yaani tunapokaa vibarazani tunajihisi kana kwamba tuko ndani ya mashua au boti katikati ya Bahari Hindi tukipunga hewa. Twashukuru kaunti kuibuka na mpango huu,” akasema Bi Omar.
Bw Jeremiah Oluoch, mtalii wa ndani kwa ndani kutoka Nyanza, anasema tangu alipozuru mji wa kale wa Lamu wiki moja iliyopita amekuwa mpenzi wa kubarizi kwenye vibaraza hivyo.

Anasema punde anapokaa vibarazani yeye huitalii bahari na mji wa kale wa Lamu kiurahisi.
“Kaunti ilifikiria sana kabla ya kuja na mradi kuu wa vibaraza. Kama mgeni wa eneo hili, nimefurahia si haba. Nikikaa kwenye vibaraza hupata fursa nzuri ya kutalii mandhari ya Bahari Hindi na pia mji wenyewe wa kale. Waongeze hivi vibaraza kwani ni vichache mno,” akasema Bw Oluoch.
Baadhi ya wenyeji, watalii na wageni pia wameshuhudiwa wakiweka meza, viti au hata kutandika mikeka kwenye vibaraza hivyo, hasa nyakati za magharibi ilmuradi wajivinjari pale.

Bw Omar Bunu anasema vibaraza hivyo vimekuwa msaada, hasa kwao kama wazee wa Lamu kwani mara nyingi wamekuwa wakikusanyika hapo na kujadiliana masuala muhimu ya kuuendeleza mji wao.
“Utatupata sisi wazee tukipiga gumzo kwenye vibaraza hivyo, si kupitisha muda tu bali kugusia masuala muhimu ya kuuendesha mji wetu wa kale. Vibaraza hivi vimetupa nafasi nzuri ya kupumzika, kukutanika, kutangamana na kutagusana na wengine. Ni fahari yetu,” akasema Bw Bunu.
Mji wa kale wa Lamu ni kivutio kikuu cha watalii wanaozuru kaunti hiyo kila mwaka.
Mnamo 2001, Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) liliuorodhesha mji huo kuwa miongoni mwa maeneo yanayotambuliwa zaidi ulimwenguni kwa kuhifadhi ukale wake, yaani Unesco World Heritage Site.