Jamvi La SiasaMakala

Raila aingia na kuwaingiza baridi Mudavadi na Gachagua

Na MOSES NYAMORI August 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

USHIRIKIANO wa Rais William Ruto na Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga umezua wasiwasi na hali ya mshikemshike katika muungano tawala wa Kenya Kwanza huku ‘mayatima’ wa kisiasa wakianza kuhisi baridi.

Ushirikiano huo, ambao Rais Ruto ameuita ‘Serikali Jumuishi’ umeweka hatarini mustakabali wa kisiasa wa baadhi ya viongozi katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Tayari kuna minung’uniko ndani ya Kenya Kwanza kwamba, washirika wake wengine wanaweza kujipata mataani anapojiandaa kutengea wale wa Bw Odinga nyadhifa zaidi serikalini.

Wanachama waanzilishi wa muungano tawala wamekerwa na ripoti kwamba, maafisa zaidi wakuu serikalini watalazimika kutimuliwa kuwapisha washirika wa Bw Odinga.

Taifa Leo imebaini kuna hali ya wasiwasi katika mrengo wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.

Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula – wote kutoka Magharibi mwa Kenya – walitia saini mkataba wa kabla ya uchaguzi ambao ulitenga asilimia 30 ya vyeo serikalini kwa vyama vyao vya Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya.

Lakini baada ya kuingia kwa Bw Odinga na baadaye uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya kwenye Baraza la Mawaziri, huenda makubaliano hayo yakatupiliwa mbali.

Bw Odinga angali anafurahia ufuasi mkubwa katika eneo hilo, hali ambayo inaweza kuvuruga mpangilio uliopo na kuathiri Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula.

Waliokuwa Mawaziri Prof Njuguna Ndung’u (Wizara ya Fedha na Mipango), Ezekiel Machogu (Elimu), Aisha Jumwa (Jinsia), Moses Kuria (Utumishi wa Umma), Zachariah Mwangi Njeru ( Maji) na Mithika Linturi (Kilimo na Maendeleo ya Mifugo) walikuwa wa kwanza kuathiriwa kisiasa Dkt Ruto akijumuisha washirika wa Bw Odinga serikalini kuzima shinikizo za vijana walioandamana wakitaka ajiuzulu.

Baadhi yao ni washirika wa Mudavadi, Gachagua na Wetang’ula.

Wengine walioachishwa kazi ni Ababu Namwamba (Masuala ya Vijana na Michezo), Simon Chelugui (Ushirika na Biashara Ndogo na za Kadri (MSME), Florence Bore ( Leba na Kinga ya Jamii), Eliud Owalo (Habari, Mawasiliano na Uchumi dijitali) , Susan Nakhumicha Wafula (Afya) na Peninah Malonza (Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maeneo Kame).

Rais Ruto alimteua John Mbadi kuongoza Wizara ya Fedha na Mipango ya Kiuchumi, Hassan Joho (Madini na Uchumi wa Majini), Wycliffe Oparanya (Ushirika na MSMEs) na Opiyo Wandayi (Kawi).

Beatrice Asikul, mshirika mwingine wa karibu wa Bw Odinga, pia aliteuliwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maeneo Kame.

Kutimuliwa kwa Bw Owalo, Bw Namwamba na Bi Jumwa kumehusishwa na ushirikiano wa Rais na Bw Odinga ambaye aliteua viongozi kutoka maeneo wanayotoka.

Ushirikiano huo huo pia ni pigo kwa waasi wa kisiasa, hasa kutoka Nyanza ambao walitarajia kuteuliwa kabla ya ukuruba wa Rais na Odinga.

Bw Kuria pia amehusisha kuondolewa kwake serikalini na ushirikiano wa Rais na Bw Odinga na hasa mizozo ya ndani kati ya Bw Gachagua na viongozi wa eneo la Mlima Kenya.

“Watu wa Raila Odinga walijiunga na baraza jipya la mawaziri la Ruto kutokana na hesabu mbovu ya kisiasa na mabishano kati yetu kutoka eneo la Mlima Kenya,” alisema Bw Kuria Jumatano.“Kabla ya Rais William Ruto kufanyia mabadiliko Baraza la Mawaziri, Naibu Rais Gachagua aliwakosoa waziwazi na kuwashambulia mawaziri kutoka eneo la Mlima Kenya na hivyo ndivyo tuliishia kuwa nje ya serikali,”

“Mimi sasa sina kazi. Wakati mabadiliko yalipotokea hivi majuzi, tuliona wengine wakiwaleta Hassan Joho, Wycliffe Oparanya, na John Mbadi. Lakini wale wa eneo letu walibadilishwa na watu ambao sifa zao hazieleweki,” alilalamika.

Wadadisi wa siasa wanasema Serikali Jumuishi inavuruga Bw Gachagua.

“Serikali Jumuishi ndiyo jinamizi baya zaidi kwa Gachagua. Atalazimika kupoteza mengi katika ajenda yake ya kuwa na ushawishi katika sera za serikali kwa sababu hatakuwa wa pekee ambaye Rais atasikiliza,” asema Prof David Monda, Mhadhiri na mchanguzi wa siasa.“Kisiasa, Serikali Jumuishi itatishia muungano wa Kenya Kwanza kwa sababu Ruto na ODM wanaweza kupanga mrengo mbadala wa kisiasa kuelekea 2027 ambao utamweka kando Gachagua.”