Raila aunga mkono mfumo wa ‘mtu mmoja, shilingi moja’
NA MWANGI MUIRURI
KIONGOZI wa Azimio La Umoja-One Kenya Bw Raila Odinga sasa anaunga mojawapo la maazimio ya Kongamano la Limuru III ambapo baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya walisema wanataka mfumo wa ugavi wa rasilimali kwa kigezo cha idadi ya watu almaarufu ‘mtu mmoja, kura moja, shilingi moja’.
Bw Odinga ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) anatoka eneo la Nyanza.
Alisema kila eneo lina haki ya kupata mgao wake wa kutosha kutoka kwa serikali.
“Ninaunga mkono ugavi wa rasilimali kwa msingi wa mtu mmoja-kura moja-shilingi moja. Ninajua baadhi ya watu hawafurahishwi na hili ila ninachoweza kusema ni kwamba huu ni mjadala muhimu tunaopaswa kushiriki kikamilifu,” akasema Bw Odinga mnamo Alhamisi.
Mjadala wa ugavi wa rasilimali kwa kuzingatia idadi ya watu umekuwa ukiendelea, ukitishia kupasua ukanda wa Mlima Kenya huku kukizuka mirengo ya wanaounga mkono wakiongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagau, na pia wanaopinga wakiongozwa na mshauri mkuu wa kiuchumi wa Rais William Ruto, Dkt David Ndii.
Kwa shabaha ya kisiasa, wadau mbalimbali wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Bw Jeremiah Kioni wanasema kwamba “ukimwona Dkt Ndii anapinga na mkubwa wake ni Rais Ruto, ujue kwamba hiyo ni ikulu yenyewe inakataa tupate haki yetu ya ugavi wa rasilimali”.
“Tukikosa hiyo haki yetu tubakie watumwa wa wengine,” akalia Bw Kioni.
Katika kuunga mkono, Bw Gachagua anasisitiza kwamba “sisi ndio walipa ushuru na ndio wengi na yeyote wa kutoka Mlima Kenya ambaye atadinda kuunga mkono mfumo huo anafaa aorodheshwe kama msaliti”.
Akiongea katika hafla ya utamaduni wa muziki wikendi iliyopita katika Kaunti ya Laikipia, Bw Gachagua alisema kwamba wapigakura wote wa kutoka Mlima Kenya wanafaa wapige msasa wanasiasa wao wote.
“Yeyote atakayepinga mfumo huo, ahesabiwe miongoni mwa wasaliti,” akasema Bw Gachagua.
Hata hivyo, Dkt Ndii anashikilia kwamba mfumo huo hauwezi ukafanya kazi katika taifa linalolenga kujiangazia kama la usawa wa kila mwananchi kwa kuwa huwa unalenga kudumisha ukiritimba wa ugavi ambapo idadi ya watu hutumika kuendeleza ukandamizaji kwa walio wachache huku wale waliobahatika kuvuna manufaa ya uchumi wa kitaifa wakitumia bahati yao kuwanyanyasa wengine.
Dkt Ndii aliambia Taifa Leo kwamba hakuna vile eneo la Mlima Kenya linaweza likadai kwamba halivuni manufaa ya taifa hata kuliko wengine.
“Barabara nyingi zimejengwa katika eneo la Mlima Kenya, kuna stima, mabwawa ya maji, hospitali nzuri, shule pamoja na taasisi nzuri. Mazuri hayo yote yako katika eneo la Mlima Kenya na hufadhiliwa kwa kutumia pesa za umma,” akasema Dkt Ndii.
Wa kuunga mkono ni Mbunge wa Embakasi Kaskazini Bw James Gakuya anayeteta kwamba Rais Ruto anacheza siasa na suala hilo kwa kuwa anaogopa kupoteza kura za jamii zilizo na idadi ndogo ya watu.
Licha ya kutoa ahadi hiyo kwa wenyeji wa Mlima Kenya alipokuwa akipiga kampeni zake za kuchaguliwa urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, kwa sasa amekuwa kimya huku jamii zile ndogo nchini zikiungana kuupinga kwa dhati.
Bw Gakuya alisema kwamba ni wakati wa Mlima Kenya kuamka na kudai mfumo huo uanze kutumika upesi iwezekanavyo.
“La sivyo, tuanze kuwazia mengine nje ya ndoa yetu na walio mamlakani nchini,” akasema Bw Gakuya anayemenyana na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kuwa mwenyekiti wa Nairobi wa chama cha Dkt Ruto cha United Democratic Alliance (UDA).
Mbunge wa Laikipia Mashariki Bw Mwangi Kiunjuri kwa upande wake anaunga mkono kiasi kwamba hata ameandaa mswada katika bunge la kitaifa akitaka mfumo huo uwe sheria.
Akiunga, kinara wa Narc Kenya Bi Martha Karua anasema kwamba “Bw Gachagua analialia leo kuhusu mfumo huo na wakati ulwekwa katika mpango maalum wa BBI ndio uwekwe ndani ya katiba, alipinga akiandamana na Dkt Ruto ambaye wakati huo ndiye alikuwa Naibu wa Rais”.
Bi Karua anasema kwamba mfumo huo unafaa kuanza kutekelezwa pasipo kuchelewa tena na wote ambao wanapinga ni wale ambao hawana nia njema na taifa la usawa.
Mbunge wa Kangema Bw Peter Kihungi anasema kwamba “huo ni mpamgo ambao hauwezi ukatekelezwa na kuna haja ya Wakenya waambiane ukweli”.
Alisema kwamba mfumo huo hata mahakama imeshindwa kuupa mashiko “kwa kuwa tulianza harakati hizo za kudai utumike nchini miaka ya tisini (1990s) na hatujawahi kufanikiwa kwa kuwa ukadiriaji wa kina wa takwimu na mazingira halisi unaonyesha kwamba hiyo ni ndoto”.
Seneta wa Nyandarua Bw John Methu alisema kwamba mfumo huo ni bora lakini unafaa kuambatana na utathmini wa masuala mengine pana ya kiuchumi ili “kutupatia hali ya umoja ndani ya usawa”.
Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria, ambaye amekuwa akiunga huku akipinga ametoa kauli yake ya hivi karibuni akikataa kuunga mfumo huo.
“Hata sijui ni nini sisi watu wa Mlima Kenya tunapenda kulialia hivyo. Tayari tuko na nyadhifa za juu serikalini… tuko na mamlaka ambayo ni ya kiwango cha asilimia 47. Kile tunachohitaji ni kuamua kwamba tutasaidia maeneo yetu kuvuna manufaa ambayo wanalilia pasipo kuingia kwa majukwaa kulialia kama walio nje ya serikali,” akasema Bw Kuria.
Cha kuzua cheche za kisiasa ni kwamba, aliye mwenyekiti wa kamati kuhusu bajeti na utekelezaji Bw Ndindi Nyoro ni mwenyeji wa Mlima Kenya na amekuwa kimya katika mjadala huo wote.
Kaunti za Mlima Kenya ambazo ziko na idadi kubwa ya watu ni Kiambu, Nakuru, Murang’a na Meru. Pia Nairobi inahesabika kwa kundi hili, ingawa hujitenga kama kaunti ya jiji kuu. Kaunti hizo ndizo ziko na zaidi ya watu 1 milioni kwa kila mojawapo.