• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Rais atumia ‘mkato’ kuwapa wakazi wa Maragua maji

Rais atumia ‘mkato’ kuwapa wakazi wa Maragua maji

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Maragua Mary wa Maua amesema wenyeji na wakazi wa eneobunge lake wana furaha kuu kwa kuwa Rais William Ruto amewasaidia kupata mhudumu wa maji ambaye atawasikiliza.

Yumkini Rais Ruto alijitwika jukumu la Bodi ya Kudhibiti Huduma za Maji nchini (Wasreb) kwa kuchora mipaka ya huduma za maji Murang’a mnamo Februari 15, 2024.

Hatua ya kiongozi wa nchi ilijiri siku chache baada ya Bi Wa Maua kutishia kuongoza waandamanaji kukita kambi katika Ikulu ya Nairobi kulalamikia ukosefu wa maji.

“Sheria ya 2016 ya kudhibiti maji hasa katika kipengee cha 86 huelezea kwamba, Wasreb ndio tu iliyo na uwezo wa kutathimini upya mipaka ya huduma za maji kwa ushirikiano na wenyeji ambao ni lazima wahusishwe,” akasema wakili wa Mahakama Kuu Geoffrey Kahuthu akirejelea ‘mkato’ ambao Rais alitumia.

Bw Kahuthu anasema kwamba kile kiongozi wa nchi angefanya ni kusubiri harakati za Wasreb, ambazo zilikuwa zimeanzishwa, zikamilike na apewe ripoti atangaze mipaka mipya ikiwa ni lazima angefanya hivyo.

“Kama yeyote angeenda mahakamani kusaka utafsiri wa kikatiba, kuna uwezekano mkubwa kwamba amri ya Rais ingebatilishwa. Lakini sasa Wasreb haiwezi ikachora mipaka vinginevyo kwa njia ya kumdunisha Rais,” akasema.

Kuna minong’ono ya kichinichini kwamba amri ya Rais ililenga kuwapa mabwanyenye fulani ambao walikuwa upinzani lakini wakamrejelea, mwanya wa kula vizuri ndani ya sekta za maji, mashamba, na viwanda. Madai yao hata hivyo ni uvumi tu bila ushahidi wowote.

Katika amri ya Rais Ruto, eneobunge la Maragua lote sasa litakuwa likihudumiwa na kampuni ya maji na usafi ya Murang’a (Muwasco) hivyo basi kuing’oa ile ya Murang’a Kusini ikifahamika kama Muswasco.

Rais William Ruto akiwa katika ziara ya kujionea mradi wa bwawa la Maragua mnamo Februari 15, 2024, alikotekeleza mapinduzi ya ‘serikali ya maji’ eneo hilo. PICHA | MWANGI MUIRURI

Kampuni za Muwasco na Muswasco kwa mujibu wa Seneta wa Murang’a Joe Nyutu, zimekuwa zikijaribu kujiweka katika nafasi ya kudhibiti rasilimali za mabwawa ya kima cha Sh57 bilioni yanayonuiwa kujengwa eneo hilo kabla ya mwaka wa 2032.

“Kwa sasa kuna bwawa moja la kima cha Sh1 bilioni ambalo limekamilika na ndilo linalengwa kutumika kusambaza maji katika eneobunge la Maragua na pia sehemu nyingine za eneobunge la Gatanga. Muswasco ndio ilikuwa ikidhibiti mipaka hiyo ya Maragua na kwa sasa Rais ameitimua,” akasema Bw Nyutu.

Bwawa lile la gharama ya juu limekadiriwa kujengwa kwa bajeti ya Sh45 bilioni katika mpaka wa maeneobunge ya Kiharu, Maragua, Kigumo, na Kangema.

Mkurugenzi mkuu wa Wasreb Julius Itunga alisema kwamba “sisi ndio tuko na mamlaka ya kutathmini upya mipaka ya huduma za maji lakini ukiangalia suala hili vinginevyo, Rais ndiye kinara wetu sisi sote”.

“Kwa sasa hatuna jingine ila tu kusitisha harakati za kutathmini mipaka na badala yake tuweke amri ya rais mbele na tutimize vigezo vinavyohitajika ili ushauri huo wake usimame,” akasema Dkt Itunga.

Aliongeza kwamba hawachukulii amri ya Rais kama mwingilio wa kazi yao kwa kuwa “yeye ndiye ametuteua”.

Sasa mbunge wa Maua aliambia Taifa Leo kwamba “sisi wakazi wa Maragua tuna furaha kuu kwa kuwa Rais ametusaidia kupata mhudumu wa maji ambaye atatusikiliza”.

“Muswasco ilikuwa imelemewa kutupa maji safi na katika Kaunti mzima ya Murang’a iliyo na maeneobunge saba, sisi tu Maragua ndio tuliokuwa na asilimia 20 ya maji huku maeneo mengine yakiwa na zaidi ya asilimia 70,” akadai Bi wa Maua.

Mbunge wa Maragua Mary wa Maua akiwa katika mkutano na Waziri wa Maji Zachary Njeru kupanga jinsi ya kuhalalisha mapinduzi ya Rais kuhusu maji Murang’a mnamo Februari 26, 2024. PICHA | MWANGI MUIRURI

Alisema kwamba Muswasco ilikuwa ikihudumu katika maeneobunge ya Maragua, Kigumo na Kandara na ilikuwa imelemewa na majukumu ya usambazaji maji.

“Mimi mwenyewe ndiye nilimwendea rais na nikamchochea atoe amri hiyo ambayo sasa itaipa Muwasco uwezo hata wa kuchukua usukani miradi ya maji taka ya mji wa Kenol na wa Maragua kwa kima cha Sh3.5 bilioni,” akasema.

Aidha, Kampuni hiyo ya Muwasco sasa itathibiti bajeti ya Sh180 milioni ya usambazaji maji ambayo Muswasco ilikuwa itekeleze.

Bi Maua alisema kwamba “mipaka mipya ya Muwasco sasa itaingia katika eneobunge lote la Maragua na hatimaye ipenye katika maeneo ya Kagundu-ini na Kabati katika eneobunge la Kandara”.

Awali, Muwasco ilikuwa ikihudumia wadi ya Township na Mbiri katika eneobunge la Kiharu.

Bw Nyutu alisema kwamba “kwa sasa tunafaa tukome kujadili suala hilo kwa msingi wa sheria na badala yake tujiulize kama wananchi watapata maji ambayo ndio ya maana zaidi”.

Alisema yeye atasimamia kuhakikisha amri hiyo ya Rais inatekelezwa kwa kuwa usambazaji maji ni jukumu la serikali ya Kaunti “nihakikishe kwamba wananchi wa Maragua wamepata maji kwa asilimia 70 kabla ya 2027”.

Waziri wa Maji katika kaunti ya Murang’a Mary Magochi aliambia Taifa Leo kwamba kulikuwa kumeandaliwa mkutano wa wadau na Wasreb mnamo Januari 30,2024, ili kutafakari suala la mipaka na harakati hizo zilikuwa zikiendelea.

“Tulikuwa katika mkutano huo tukiwa Kaunti, Muwasco na Muswasco. Kile amri ya Rais imefanya ni kuharakisha matakwa ya wengi na kwa sasa serikali ya Kaunti hailalamiki na tuko tayari kutekeleza mwelekeo huo wa Rais,” akasema Bi Magochi.

Mkurugenzi mkuu wa Muswasco Mary Nyaga alisema kwamba wamekubali.

“Kwa sasa hatuna budi ila tu kuhamisha udhibiti wa mipaka mipya kwa Muwasco,” akasema Bi Nyaga.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa Muwasco Daniel Ng’ang’a alisema kwamba wako tayari kuhudumu chini ya majukumu mapya.

“Lakini kwanza tutasaka kulainisha leseni yetu kisheria ili iwiane na mipaka mipya ambayo tumetunukiwa na Rais Ruto,” akasema Bw Ng’ang’a.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Polisi walia kupunjwa fedha zao za sacco

Raila amepenya serikalini?

T L