Rais Ruto alianguka nao
Mutua atua Mwala
Alfred Mutua
ALIKUWA Waziri wa Utalii katika serikali ya Kenya kwanza kabla shoka kuangushwa Alhamisi. Alihamishiwa wizara hiyo kutoka ile ya Mashauri ya Kigeni ambapo alilaumiwa kwa kauli zilizoathiri sera ya kigeni ya nchi huku akitumia muda mwingi akitalii majiji kote ulimwenguni. Alikuwa amepokonywa baadhi ya majukumu katika wizara hiyo kabla ya kuhamishwa. Mutua alihudumu kwa mihula miwili kama gavana wa Machakos, kabla ya kuteuliwa waziri baada ya chama chake kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.
Aisha Aishia Kilifi
Aisha Jumwa
Mbunge huyo wa zamani wa Malindi aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuongoza Wizara ya Utumishi wa Umma na Jinsia kabla ya kuhamishiwa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi.
Bi Jumwa, mfuasi shupavu wa Rais Ruto katika kampeni, alihudumu kama Kamishna katika Tume ya Huduma za Bunge.
Bi Jumwa aliondolewa mashtaka ya ubadhirifu katika Hazina ya Kitaifa ya Eneo Bunge la Serikali (NGCDF) na madai ya mauaji wakati wa uchaguzi mdogo huko Malindi.
Mbolea yaramba Linturi
Mithika Linturi
Bw Linturi aliwahi kuwa Mbunge wa Igembe Kusini na Seneta wa Kaunti ya Meru. Alifanikiwa kuwania kiti cha ugavana na kuangushwa na Kawira Mwangaza katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Alinusurika kufuatia hoja ya kuondolewa madarakani kuhusiana na ununuzi na usambazaji wa mbolea feki kwa wakulima.
Katika enzi yake kama Mbunge wa Igembe Kusini, Linturi alifadhili hoja ya kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Anne Waiguru. Baadaye, alikosa kujitokeza kuitetea.Wito wa kujiuzulu kwa Bw Linturi umekuwa ukiongezeka hadi Baraza la Mawaziri lilipovunjwa Alhamisi.
Maisha mepesi yakomoa Murkomen
Kipchumba Murkomen
Aliyekuwa Seneta wa Elgeyo Marakwet na Kiongozi wa Wengi katika seneti aliteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi na Barabara baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita.
Bw Murkomen amekuwa akikasirisha umma kwa kuanika utajiri wake huku Wakenya wakimtuhumu kwa kuvalia mavazi ya bei ghali, saa ya karibu milioni, mishipi na viatu.
Mafuta yakausha Kuria
Moses Kuria
Mbunge huyo wa zamani wa Gatundu Kusini alinaswa katika sakata ya mafuta ya kupikia ambayo ilimfanya ahamishwe kutoka Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda hadi Utumishi wa Umma.
Kabla ya kuhamishwa hadi Wizara ya Utumishi wa Umma, Bw Kuria hakuandamana na wajumbe wa ngazi ya juu walioongozwa na Rais Ruto hadi Amerika.
Bw Kuria aliwania ugavana Kiambu na kushindwa na Kimani Wamatangi baada ya kuhudumu katika Bunge la Kitaifa kwa mihula miwili.
Namwamba agonga mwamba
Ababu Namwamba
Mbunge huyo wa zamani wa Budalangi anakumbukwa vyema kwa kukataa kula kiapo chake cha utiifu kwa aliyekuwa Rais, marehemu Mwai Kibaki.
Mshirika wa muda mrefu wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, Bw Namwamba aliteuliwa kuongoza Wizara ya Masuala ya Vijana na Michezo.
Alikuwa waziri msaidizi wa Masuala ya Kigeni katika utawala wa Rais Kenyatta na alikosolewa vikali na Bunge la Kitaifa kuhusu usimamizi wa wizara hiyo.
Chirchir achiriza miale hadi Kericho
Davis Chirchir
Alisimamishwa kazi na aliyekuwa Rais Kenyatta kama Waziri wa Nishati na Petroli kwa madai ya ufisadi. Chirchir alirejea Wizarani baada ya kuteuliwa na Dkt Ruto.
Aliwahi kuwa mkurugenzi wa teknolojia ya habari katika Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi (IIEC). Bw Chirchir alikuwa ajenti mkuu wa Rais Ruto wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.
Bw Chirchir anahusishwa na mpango wa Serikali na Serikali wa kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi na kampuni tatu kuu za mafuta za Ghuba ambazo zilisaidia kupunguza gharama ya mafuta.
Uozo wa afya wasakama Nakhumicha
Susan Nakhumicha
Kipindi cha Bi Nakumicha katika Uongozi wa Wizara ya Afya kimekumbwa na migomo mingi ya wahudumu wa afya.
Nakhumicha alikabiliwa na mgomo wa madaktari uliodumu siku 56 huku maafisa wengine wa kliniki na wahudumu wakigoma wakitaka malipo na mazingira bora ya kufanyia kazi.
Liwe liwalo lakini Owalo naye aenda
Eliud Owalo
Bw Owalo aliwahi kuwa mshauri mkuu wa Bw Odinga alipokuwa Waziri Mkuu. Alichukua wadhifa wa Wizara ya ICT kutoka kwa Joe Mucheru na amefanikisha Miswada kadhaa, wa hivi punde zaidi ukiwa Mswada tata wa ICT uliokuwa umekataliwa na Bw Kenyatta.
Bw Owalo amewasilisha tena Mswada uliowasilishwa kwa mara ya kwanza na Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale mnamo 2016 ambao unahitaji wahudumu wa ICT kusajiliwa na baraza.
Mvurya naye alifurushwa
Salim Mvurya
Alihudumu kwa mihula miwili kama Gavana wa Kaunti ya Kwale. Aliteuliwa kuongoza Wizara ya Madini na Uchumi wa Baharini ambapo alisifiwa kwa kuidhibiti kikamilifu.
Mvurya hivi majuzi alitangaza kugunduliwa kwa hifadhi kubwa ya madini ya Coltan. Madini hayo adimu hutumika kutengeneza betri za magari ya umeme, simu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki.
Bore pia aliporwa kiti chake
Florence Bore
Mwakilishi wa zamani wa wanawake Kericho aliteuliwa kuongoza Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii baada ya kuwania kiti cha ugavana Kericho bila mafanikio.
Bi Bore, ambaye alinaswa na kashfa ya nyumba mtaani Karen ya Mbunge wa Gatanga Edward Muriu, amesifiwa kwa kusaidia kujadili makubaliano ya kazi ughaibuni na hasa nchi za Ghuba.
Malonza alikataliwa, akaponea, akatemwa
Peninah Malonza
Bi Malonza aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Waziri wa Utalii na Wanyamapori kabla ya kuhamishwa hadi Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika mabadiliko madogo.
Naibu gavana huyo wa zamani wa Kitui alikataliwa kwa kauli moja na Kamati ya Uteuzi (COA) iliyokagua ufaafu wake kama waziri.
Miano aling’aa lakini akapigwa teke
Rebecca Miano
Dkt Ruto kwanza alimteua Bi Miano kama waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Miano ambaye awali alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme KenGen baadaye alihamishwa hadi Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda. Ameorodheshwa kama miongoni mwa mawaziri waliofanya vizuri zaidi.
Kindiki alitoa vitisho na majangili wakamdharau
Kithure Kindiki
Prof Kindiki alikuwa Waziri wa Usalama wa Ndani na Uratibu wa Wizara ya Kitaifa ya Serikali
Kabla ya uteuzi wake, Profesa Kindiki alihudumu kwa mihula miwili kama Seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi kuanzia 2013 hadi 2022. Alishindana na Rigathi Gachagua kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto. Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Masuala ya Ndani.
Prof Kindiki, aliyekuwa Kiongozi wa Wengi katika Seneti ameongoza kura zote za maoni ambazo zilimsawiri kama waziri mchapa kazi.
Anasifiwa kwa kurejesha amani katika eneo la North Rift, kuimarisha uwezo wa polisi na kutuma maafisa 1,000 kusaidia kupambana na magenge huko Haiti.
Duale alifungua milango ya wanajeshi
Aden Duale
Alihudumu kama mbunge kwa mihula minne na Kiongozi wa kwanza wa Wengi katika Bunge la Kitaifa kati ya 2013 na 2020 kabla ya kuteuliwa kusimamia Wizara ya Ulinzi.
Bw Duale alituma Wanajeshi kuunga mkono juhudi za polisi kurejesha amani katika maeneo yenye ujangili katika Bonde la Ufa.
Wakati wa maandamano ya hivi majuzi ya kupinga ushuru na serikali, Bw Duale alikimbilia Bunge la Kitaifa na kupata idhini ya kupeleka jeshi kusaidia kuzima vijana ambao walivamia Bunge siku ambayo Mswada wa Fedha wa 2024 ulipitishwa kwa haraka.
Shilingi ya Kenya iliyeyuka Ndung’u akaidhibiti
Njuguna Ndung’u
Alikuwa Gavana wa nne wa Benki Kuu ya Kenya. Aliteuliwa kuongoza Hazina ya Kitaifa na Wizara ya Mipango ya Kiuchumi wakati nchi ilikuwa inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi iliyochangiwa na na kuongezeka kwa deni.
Prof Njuguna, ambaye ni msomi wa Uchumi, anasifiwa kwa kusaidia nchi kulipa mkopo wa Eurobond wa Sh257bilioni) uliopaswa kulipwa kufikia Juni 24, 2024. Pia anasifiwa kwa kusaidia sarafu ya Kenya shilingi ambayo thamani yake ilikuwa imeshuka hadi Sh162 dhidi ya dola kuwa thabiti.
Kwake Wahome vitisho ndivyo vilikuwa vingi
Alice Wahome
Mbunge huyo wa zamani wa Kandara alichaguliwa kuongoza Wizara ya Maji lakini mgogoro kati yake na Katibu wake Kiprono Ronoh ulimfanya ahamishiwe Wizara ya Ardhi, Ujenzi wa Umma, Nyumba na Maendeleo ya Miji.
Wakili huyo mwenye umri wa miaka 64 anajulikana kwa msimamo mkali wa kisiasa na alimuunga mkono Ruto katika kampeni za 2022.
Machogu alipigwa chenga na masuala ya elimu
Ezekiel Machogu
Bw Machogu, aliyekuwa mbunge wa Nyaribari Chache na mwenyekiti wa kamati ya upishi Bungeni aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu. Afisa wa utawala wa miaka mingi, alipambana na utekelezaji wa Mtaala unaozingatia Umilisi (CBC), udaganyifu wa mitihani na kuchelewa kwa pesa za kufadhili elimu ya bure ya msingi, sekondari, elimu ya juu na chuo kikuu.
Tuya alitulia ndio, lakini miti nayo akaipanda
Sopian Tuya
Bi Tuya ambaye ana Shahada ya Uzamili ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Washington, Amerika alikuwa waziri wa Mazingira,
Kabla ya kuteuliwa waziri, alihudumu kama Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Narok.
Anajulikana sana kwa kuisaidia Kenya kuandaa Kongamano la kwanza la Mabadiliko ya Tabianchi barani Afrika mnamo 2023.
Bi Tuya amekuwa akiongoza mradi wa kupanda miti bilioni 15 katika miaka 15 ijayo.
Chelugui alijikaza kuzipa uhai MSMEs
Simon Chelugui
Bw Chelugui alihudumu kama waziri la Maji na Leba katika kipindi cha miaka kumi ya Rais Uhuru Kenyatta.
Dkt Ruto alimteua Bw Chelugui kuwa waziri wa Vyama vya Ushirika na MSMEs hadi alipofutwa kazi
Kura za maoni zilimsawiri Njeru mlaza damu
Zachary Njeru
Bw Njeru aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuongoza Wizara ya Ardhi kabla ya kuhamishwa hadi Wizara ya Maji. Mzaliwa wa Nakuru, utendakazi wake kama waziri umekuwa ukiorodheshwa kuwa wa chini.