Makala

Ramadhani: Wakristo wafurahia chajio kinachouzwa mitaani kama futari

March 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

VYAKULA vya kipekee vinavyotandazwa na kuuzwa mabarazani, vichochoroni na vishorobani mwa mji wa kale wa Lamu kila jioni inapowadia, hasa tangu Mwezi Mtukufu wa Ramadhni kung’oa nanga, vimewavutia wengi, aghalabu Waislamu na wale wasiokuwa Waislamu.

Vyakula hivyo, ambavyo huuzwa kwa minajili ya futari kwa waumini wa dini ya Kiislamu, sasa vimekuwa kipenzi cha wengi.

Waislamu kwa Wakristo wamekuwa wakifurika kwenye vibaraza, vichochoro na vishoroba vya mji huo wa kihistoria wa Lamu kuvinunua ilmradi wafurahie upekee wa maandalizi au mapishi ya aina yake yanayovifanya kuwa vitamu si haba.

Ikumbukwe kuwa futari ni chakula cha kwanza kinacholiwa magharibi na mtu aliyefunga baada ya kumaliza saumu yake.

Bw Mohamed Swaleh Said, muuzaji maarufu wa futari kisiwani Lamu, anasema kwa wakati huu biashara ya vyakula vya kufungulia saumu imenoga.

Bw Mohamed Swaleh Said (mbele kushoto), muuzaji futari maarufu kisiwani Lamu, akiuzia wateja vyakula. PICHA | KALUME KAZUNGU

Yeye huuza kababu, katilesi, sambusa, kaimati, mkate wa sinia, mkate wa mayai, samosa, mofa, viazi karai, bajia za viazi, bajia za ndegu, chapati, tende na sharubati au juisi ya kila aina ya matunda, ikiwemo ukwaju, maembe, ndizi, pesheni nakadhalika.

Bw Said anasema vyakula hivyo ni vyenye kutia siha kwa mja, hasa yule anayefunga na hata asiyefunga.

“Mimi hujibanza na kutandaza vyakula vyangu hapa kibarazani kila siku punde magharibi inapoingia na nikijua fika kuwa majira ya kufungua saumu kwa ndungu Waislamu yamekaribia. Nafurahia kwamba wateja wangu wanajumuisha Waislamu kwa Wakristo. Wengi hufurika kibarazani kujinunulia mapochopocho haya kufurahia utamu wake,” akasema Bw Said.

Bw Salim Athman, muzaji mwingine maarufu wa vyakula vya futari kisiwani Lamu, anasema yeye huuza bidhaa zake kwa kila bei mteja anataka, hasa kuanzia Sh10 kuendelea.

“Tangu Ramadhani ianze mimi sikai hapa punde nikianika vyakula hivi vya futarti kuuza. Wengi, hasa wale wasiokuwa wa dini ya Kiislamu huja kujinunulia vyakula vyangu. Utapata nikiuza vyakula hivi kwa bei ya kati ya Sh10 na Sh30 kulingana na aina mteja anachagua. Vyakula vyangu ni bei ya kati ya Sh10 na Sh30,” akasema Bw Athman.

Bw Salim Athman (mwenye fulana nyeupe) akiuzia wateja futari kisiwani Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Baadhi ya waliohojiwa kisiwani Lamu walisifu mapishi ya futari inayouzwa mitaani.

Bw Joseph Wafula anasema licha ya kwamba yeye si Mwislamu, amehakikisha hakosi vyakula hivyo vitamu nyumbani kwake kila jioni.

Anasema mara nyingine yeye na mkewe huafikia kununua na kutumia vyakula hivyo nyumbani kama chajio.

Bw Wafula aliweka wazi kuwa mara nyingi msimu wa Ramadhani unapowadia, msongo wa mawazo nyumbani huisha.

“Msongo wa mawazo kuhusiana hasa na vyakula gani vya kupika au kutumia nyumbani huisha. Msimu huu wote wa siku 30 za Ramadhani huwa vyakula vitamu ni vingi mabarazani na vichochoroni. Tunapenda sana hivi vyakula vya futari,” akasema Bw Wafula.

Bi Mary Mwangi, mkazi wa kisiwa cha Lamu, pia alikiri kuwa na  mchuuzi maalumu ambaye hununua vyakula hivyo vya futari kutumia nyumbani kama chajio au vitafunio vya chakula cha asubuhi siku inayofuata.

“Ni vyakula tamu ajabu ambavyo huwezi kuvikwepa. Tunafurahia sote na tunawatakia ndugu zetu Waislamu Ramadhan Kareem,” akasema Bi Mwangi.

Bw Simon Mutua anasema wakati huu wa Ramadhani yeye huvutiwa kupitapita vichochoroni na mitaa ya mji wa kale wa Lamu kufurahia mandhari ya kupendeza yanayopambwa na vyakula vya aina aina mabarazani.

“Wakati huu wa Ramadhani ukarimu umesheheni si haba. Mimi hufurahia nikipita vishorobani na mitaa ya mji wa Lamu na kuwaona Waislamu kwa Wakristo wakijibanza kushiriki futari pamoja. Hiyo inaleta umoja, uwiano na utangamano wa dini na makabila yote hapa kisiwani na Lamu kwa jumla,” akasema Bw Mutua.