Makala

Reuben Kigame asuta Rais Ruto, Gachagua akirejelea amri ya korti

June 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA mwaniaji wa urais mwaka wa 2022, Bw Reuben Kigame amewataka Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua wakome kile alichokitaja kama unafiki wa kiutawala wa kuhadaa Wakenya kwamba utawala wao ni wa kuunganisha Wakenya.

Kilio cha Bw Kigame ambaye pia ni mwimbaji wa nyimbo za Injili kimejiri huku baadhi ya viongozi wengine wa makanisa na pia taasisi za haki na uwiano nchini kwa pamoja, wakizua kilio cha haki kuhusu hali ilivyo katika utawala wa Rais Ruto, wakidai kuna ubaguzi mkuu ambao unatishia uwiano wa nchi.

“Huwezi ukawa wa maneno ya usemi ambao asilimia kubwa ni masilahi ya Mlima Kama jinsi anavyofanya Bw Gachagua na, kisha unakuja kwa jukwaa la utaifa kutuambia unaunganisha. Hii serikali ya Kenya Kwanza ikiongozwa na Rais William Ruto imeajiri watu kwa misingi ya kikabila kiasi kwamba mahakama zimetengua baadhi ya kazi,” akasema Bw Kigame.

Bw Kigame alisema kwamba uongozi unafaa kueleweka kwa uwiano wa usemi na matendo, akisema kwamba “kwa sasa yale ambayo hao wawili hutangaza kwa vinywa vyao vinakinzana na uhalisia wa athari za matendo yao”.

Utawala wa Rais Ruto umekuwa ukikemewa kwa kiwango kikuu kutokana na madai ya kutekeleza teuzi za kikabila ambazo huwafaa ‘wanahisa’ wa Mlima Kenya na Rift Valley kwa kiwango kikuu, huku nao mawaziri wakigawa nyadhifa za wakurugenzi wa mawasiliano katika wizara zao kwa kuzingatia misingi ya urafiki na ushirika wa wale walio wao.

Ni hivi majuzi tu ambapo uteuzi wa aliyekuwa mshukiwa wa mauaji Bi Jacque Maribe kama mkurugenzi wa mawasiliano katika Wizara ya Utumishi wa Umma ulizua ghadhabu hata ndani ya serikali yenyewe na kumweka shinikizo Waziri Moses Kuria.

Aidha, kuna kisa kingine ambacho kimekuwa kikichunguzwa cha kitengo cha itifaki katika ikulu kumpa kazi msanii mmoja kazi licha ya kuwa hakumaliza elimu ya Kidato cha Nne.

Bw Kigame alisema kwamba kuunganisha Wakenya hakufai kuwa na unafiki kwa kuwa ni lazima usawa na haki kuwa nguzo muhimu katika kuwafanya Wakenya wote wajihisi taifa ni lao wala sio la wachache.

Uteuzi mwingine ambao ulileta shida ni ule wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ushindani–Competition Authority–ambapo ulimulikwa kwa kashfa ya washirikishi wa mchakato huo kupenyeza majina mengine 33 katika orodha ya mwisho kama njia ya kuwaundia nafasi bila msasa.

Nayo Mahakama Kuu tayari imepiga breki uteuzi wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) kwa msingi kuwa walioishia kupewa kazi hizo walikuwa ni wandani wa mirengo ya kisiasa ndani ya jamii fulani.

Bw Gachagua amekuwa mmoja wa wapigiaji debe wakuu wa mfumo wa kutoa kazi kwa jamii za wale ambao waliunga mkono utawala wa Rais Ruto katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022, akisema kwamba “wale ambao hawakuwekeza imani yao ndani ya Ruto wanafaa tu kulishwa makombo”.

Tayari, kanisa la Anglikana kupitia Askofu Jackson Ole Sapit limeteta kwamba “teuzi ndani ya serikali sio za kuunganisha taifa hili na kuna ule upenyo wa ukabila ambao huwafanya wengine kuangaziwa kama wa jamii za hadhi wengine wakiwa wa kudunishwa”.

Pia, viongozi wa Kanisa Katoliki wakiongozwa na kiongozi wao wa Kaunti ya Nyeri Bw Anthony Muheria wamesena kwamba kunafaa kuwe na uwazi na usawa katika ajira ya serikali ili kulipa taifa ule mshikamano wa kujua kwamba kila aliye na uhitimu hatabaguliwa kwa msingi wa kisiasa na kikabila.