Makala

Ripoti yafichua uchumi wajikokota licha ya serikali kujipiga kifua

Na BENSON MATHEKA January 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UCHUMI wa Kenya ulikua kwa asilimia nne katika kipindi cha miezi mitatu hadi Septemba mwaka jana, ikiwa ni kasi ya chini zaidi katika kipindi cha miaka minne huku kulemaa kwa sekta kuu za ujenzi na madini kukiathiri ustawi.

Ukuaji wa jumla wa ndani au jumla ya pato la nchi, uliongezeka kwa kasi ndogo ikilinganishwa na asilimia sita katika robo ya tatu ya 2023, kulingana na takwimu za Shirika ya Kitaifa ya Takwimu Kenya (KNIBS) zilizotolewa Jumanne.

Ulikuwa ukuaji wa chini zaidi tangu 2020 wakati serikali iliweka hatua za kuzuia kusambaa kwa Covid-19, ambayo ilitatiza shughuli za kiuchumi na kusababisha idadi kubwa ya Wakenya kukosa kazi.

Huu ni mwendelezo wa mwelekeo katika robo mbili za kwanza ambapo ukuaji wa Pato la Taifa ulipungua ikilinganishwa na vipindi sawia mwaka wa 2023, na unaonyesha ukuaji wa polepole wa mwaka mzima kama inavyotarajiwa na wataalamu wengi wa kiuchumi.

“Ukuaji uliodorora ulichangiwa pakubwa na kushuka kwa jumla kwa ukuaji katika sekta nyingi za uchumi,” ilisema KNBS katika ripoti yake ya Pato la Ndani ya lila robo mwaka.

“Ukuaji ulichangiwa na kupungua kwa shughuli za ujenzi na uchimbaji madini na uchimbaji mawe. Shughuli za ujenzi zilipungua kwa asilimia 2.0 wakati uchimbaji madini na uchimbaji mawe ulipungua kwa asilimia 11.1 katika robo ya tatu ya mwaka huo,” KNIBS iliongeza.

Utumiaji wa saruji ulipungua kwa asilimia 10 hadi tani 2.2 milioni katika kipindi cha ukaguzi, na hivyo kuchangia utendaji duni wa sekta hiyo huku serikali ya Rais Ruto ikiendelea na hatua zake za kubana matumizi ambazo zimeifanya kupunguza miradi mikubwa ya miundombinu.

Kwa kuwa barabara chache zinajengwa, lami kidogo iliagizwa kutoka nje.

Utengenezaji wa mabati ulishuka huku mikopo iliyokuwa ikitolewa kwa makampuni katika sekta hiyo pia ikishuka katika kipindi cha utafiti wa KNIBS.

Kilimo, ambacho kinachangia zaidi ya theluthi moja ya pato la kitaifa, kilisajili ukuaji wa polepole wa asilimia 4.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.1 mnamo 2023.

“Ukuaji huu (katika kilimo) ulitokana kwa kiasi kikubwa na hali nzuri ya hali ya hewa ambayo ilikuwepo katika robo tatu ya kwanza ya 2024, ingawa ilikuwa chini ikilinganishwa na 2023,” shirika lilisema Jumanne.

Ukuaji wa kilimo ulidorora na kushuka kwa asilimia 12.2 kwa uzalishaji wa chai kutoka tani 138,771.6 mwaka 2023 hadi tani 121,868.3 katika robo sawa mwaka jana, ingawa uzalishaji wa miwa na maziwa uliimarika.

Sekta nyingine zilizosajili ukuaji wa polepole ni pamoja na viwanda, huduma za malazi, usambazaji wa umeme na maji, ICT, huduma za kifedha na bima, na mali isiyohamishika.

Hata hivyo, biashara ya jumla, elimu na usafiri ilikua kwa kasi zaidi katika kipindi cha utafiti kuliko katika kipindi sawia mwaka 2023.

Licha ya kuboreshwa kwa viashirio vya uchumi mkuu, kama vile kiwango thabiti cha ubadilishaji fedha na bei ya chini ya baadhi ya bidhaa, wataalam wengi walitarajia uchumi kukua kwa kasi ndogo mwaka wa 2024 kuliko mwaka wa 2023.