Akili MaliMakala

Ripoti yafichua uharibifu wa udongo unaweka kilimo katika hatari

Na WANJIA MBUTHIA March 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Kenya inakabiliwa na mzozo mkubwa wa udongo unaohatarisha usalama wa chakula na uendelevu wa kilimo. Hii ni kwa mujibu wa ripoti inayoitwa Soil Atlas iliyotolewa hivi karibuni na wakfu wa Heinrich Boell Foundation.

Utafiti huu umebaini kuwa ni asilimia 20 pekee ya ardhi nchini inayofaa kwa uzalishaji wa chakula, huku Kenya ikipoteza hadi tani 26 za udongo kwa hektari kila mwaka kutokana na mmomonyoko wa udongo.

Kwa sasa, asilimia 40 ya ardhi inayotumika kwa unyunyuzaji nchini Kenya inaathiriwa na ongezeko la chumvi, huku takriban asilimia 85 ya udongo ukiwa na upungufu wa virutubisho.

Uharibifu huu unakadiriwa kupunguza uzalishaji wa kilimo kwa asilimia 30, hali inayofanya nchi kuendelea kutegemea kuagiza chakula kutoka nje.

Hali ni mbaya zaidi katika Afrika Mashariki, ambako zaidi ya asilimia 40 ya udongo umeharibika, hivyo kuhatarisha usalama wa chakula wa eneo hilo.

“Udongo ndio msingi wa maisha, lakini ni rasilimali ambayo haithaminiwi ipasavyo. Afya yake inaathiri chakula tunachokula, maji tunayokunywa, na hewa tunayopumua,’ alisema Joachim Paul, Mkurugenzi wa Heinrich Boell Foundation, wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo.

Mtaalamu akipima udongo kwenye maabara. PICHA|SAMMY WAWERU

Dkt Silke Bollmohr, mhariri mkuu wa ripoti hiyo kuhusu hali ya udongo Kenya, alisisitiza kuwa mjadala kuhusu udongo haupaswi kuishia kwenye rutuba pekee.

“Bioanuwai, mifumo ya ikolojia, na ustahimilivu ni vipengele muhimu vya afya ya udongo,” alieleza.

Aliongeza kuwa udongo uliodhoofika unakabiliwa zaidi na mmomonyoko, ambapo hasara ya uharibifu wa udongo kimataifa ni mabilioni ya pesa kila mwaka, huku Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ikibeba mzigo mkubwa zaidi.

Mgogoro wa hali ya udongo unachangiwa na matumizi kupita kiasi ya mbolea za viwandani, upanzi wa aina moja ya mimea na ukataji miti.

Kwa sasa, asilimia 63 ya ardhi inayofaa kwa kilimo nchini Kenya inaathiriwa na asidi, asilimia 80 inakabiliwa na upungufu wa madini muhimu, na asilimia 75 imepungukiwa na kaboni hai, hali inayosababisha kupungua kwa rutuba ya udongo na kupungua kwa shughuli za vijidudu vya udongo.

Wataalamu wanatahadharisha kuwa kutegemea mbolea za viwandani pekee si suluhisho la changamoto hii.

Licha ya Kenya kutumia wastani wa kilo 57 za mbolea kwa kila hektari, bado huzalisha mazao machache kuliko Uganda, inayotumia kilo mbili pekee kwa hektari.

Trekta ikilima shambani. PICHA|SAMMY WAWERU