Makala

RISSEA: Kituo kinachohifadhi utamaduni wa jamii za Pwani

September 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

NA RICHARD MAOSI

RISSEA (Research Institute of Swahili Studies of East Afrika) ni taasisi ambayo ilibuniwa mnamo 1992 ili kuhifadhi tamaduni za Waswahili wanaopatikana katika Pwani ya Kenya na janibu zake.

Mpaka sasa ni kituo cha kipekee nchini kinachotilia maanani umuhimu wa vijana,kupata ujuzi wa kufanya kazi za mikono,ambazo zinatambulika Mashariki ya kati,Uchina na Ujerumani.

Kupitia International Labour Organisation, UNESCO, makavazi ya kitaifa na jamii za uswahilini, washikadau wakuu walishirikiana kuanzisha Utamaduni wa Waswahili.

Walijihusisha na turadhi ambazo zinaweza kusikika na kuonekana, miongoni mwa vijana ikiwa ni pamoja na useremala, uchongaji na ile stadi ya kuunganisha samani za thamani.

ISSEA inapakana na makavazi ya Fort Jesus na Bahari Hindi ambapo hutoa mazingira mazuri kuhusu turadhi za waswahili. Picha/ Richard Maosi

Nao akina dada walifundishwa kushona mavazi ya kitamaduni na yale ya kawaida.

Kulingana na mratibu wa RISSEA Khalid Omar Kitito UNESCO ilisaidia jamii za waswahili kuhifadhi majumba ya kale, na walifanya mradi kwa ushirikiano na EU (European Union) hadi 1995 taasisi ilipofikia kwenye upeo.

“1995 mradi ulipokuwa umepata mashiko wafadhili walijiondoa ndiposa makavazi ya kitaifa yakachukua hatamu za kuendesha operesheni zake japo kwa mwendo wa kobe.,”akasema.

Kuanzia hapo ilibidi wanafunzi walipe ada fulani ya kuwasaidia kununua vifaa vya kiufundi kufanyia taaluma,jambo lililowafanya baadhi yao kukimbia wakaachana na masomo.

Vijana hupewa ujuzi wa kutengeneza samani za bei ghali ambazo huagiziwa hadi mataifa ya nje. Picha/ Richard Maosi

Kitito alifichulia Taifa Leo Dijitali kuwa RISSEA hailengi vijana waliosoma,ila inawapatia uwezo na ujuzi wa kujiajiri ili kukabiliana na janga la mihadarati lililosheheni kwa vijana wengi wa pwani.

Wakati tukizungumza na baadhi ya vijana wanaofanya useremala,walikuwa wakimalizia fanicha zilizokuwa zimeagizwa kwenda Uarabuni, labda kutokana na upekee wa mafundi kuendesha kazi kwa umahiri.

Mbali na kupaka rangi,wana uwezo wa kuweka aina mbalimbali ya mapambo ya kiasilia kwenye samani,jambo linalowafanya wanunuzi wengi kutoka nchi za mbali kuwania bidhaa zao.

Bakari Mwakarimu ni mmoja wao ambaye anajipatia riziki kutokana na kazi za mikono.Anasema kuwa ingawa nafasi za ajira ni finyu siku hizi vijana wanaweza kuvumbua riziki kutokana na kazi kama hizi muradi ni halali.

Mhudumu akionyesha baadhi ya kazi zilizohifadhiwa na waandishi mahiri waliotunga misamiati ya Kiswahili kama vile Profesa Sheikh Nabahany. Picha/ Richard Maosi

“Vijana wanapaswa kujiwekea malengo na kufahamu kuwa maisha ni safari,wala wasikate tamaa kwa kile kidogo wanachokifanya kinaweza kuwafikisha mbali,”Bakari alitueleza.

Madirisha na milango wanayotengeneza ni nafuu na huchukua miundo mbalimbali ambayo huweza kumvutia mnunuzi

Ilipofika 2005 washikadau walipanua wigo na kuanzia hapo, ikawa lengo lake sio tu kazi za mikono bali pia utafiti katika nyanja mbalimbali ikiwemo maswala ya lugha,ukalimani na kujifunza lugha za kigeni.

Kitito alieleza kuwa RISSEA ilikuwa na tawi jingine katika kisiwa cha Lamu, ambapo vijana walipatiwa ujuzi wa kutengeneza majahazi kitengo kinachofifia kwa sababu vijana wengi siku hizi hawajishughulishi na utengenezaji wa vyombo vya majini.

Picha/Richard Maosi

“Aidha makongamano ya kimataifa kwa walimu wa Kiswahili,waliopata fursa ya kujumuika pamoja ili kubadilishana kimawazo,”alieleza mtaalamu huyu ambaye amewahi kufundisha Kiswahili Marekani..

Ilipotimu 2014 RISSEA ilifanikiwa kuchapisha jarida la kwanza, na imekuwa ikiendelea hivyo ambapo kila baada ya miezi sita wamekuwa wakichapisha majarida ya kitaaluma kufanyia utafiti na kufanikisha masomo..

RISSEA imealea waandishi mahiri kama vile Professa Sheikh Nabahany wanaokumbukwa sana kwa kuchangia hazina ya misamiati ya Kiswahili,kwa mfano neno runinga lenye maana ya televisheni lilitungwa naye.

“Nabahany alikuwa akitumia mifumo ya kibantu ila siku hizi maneno yamekuwa yakibadilikabadilika,kutokana na athari ya sheng miongoni mwa lugha nyinginezo,”akaongezea.

Picha/Richard Maosi

Mchango wao katika matamshi ya Kiswahili wanaziangalia lahaja za Kenya na kuzichunguza kabla ya kuzihifadhi,katika makavazi baada ya kuzifanyia uchunguzi wa kina.

Mnamo 2010 Uhifadhi wa utamaduni katika katiba mpya uliangukia serikali za kaunti, na jambo hili liliwaletea raia huduma karibu na mazingira yao jambo linalofanya iwe rahisi kutangamana na raia moja kwa moja.

Kuanzia hapo RISSEA walianza kushirikiana na matamasha ya kitaifa ambapo mno walijikita katika uhifadhi wa minara ya kitamaduni, na kihistoria kama vile Fort Jesus,Vasco da Gama na Gedi Ruins.

Ilipofika 2015 waliibadilisha jina na kuita National Museum of Kenya Heritage Training Institute ambapo pia wafanyikazi wa kaunti walijifunza kuhifadhi sio utamaduni tu wa Kiswahili bali pia Uswahili.

Picha/Richard Maosi

Kitito anasema pia mbali na RISSEA kuwa makavazi ya kipekee nchini yaliyojizatiti kuwafundisha wageni lugha ya Kiswahili pia wanashiriki kuyafunza mataifa ya Afrika mambo mengi ikiwemo maswala ya uongozi.

“Tumetoa mafunzo mara mbili kwa raia wa tanzania wanaotokea katika kisiwa cha Zanzibar yaani Wazanzibar Stone Town Organisation kuzihifadhi turadhi zao,”alisema..

Hivi sasa RISSEA wamejisajili na TIVET na hii ni taasisi nambari moja inayotoa mafunzo kwa vijana kuhusu kazi za mikono,ambapo vijana wanafundishwa kujiajiri,mara tu baada ya kupokea ujuzi.

Aidha wamekuja na vyeti baada ya kuwatahini wanafunzi wa mataifa ya kigeni wanaofika Kenya kujifundisha lugha ya Kiswahili, ambapo,Kitito anaamini kuwa lugha za kigeni zinafundishwa bora katika taasisi.

Hii ni mijengo inayopatikana ndani ya RISSEA ambapo pia kazi za utunzi wa sanaa na kucheza muziki zimepatiwa kipaumbele. Picha/ Richard Maosi

Kulingana na National Museums of Kenya ni jukumu lao kuhkakikisha kuwa turadhi za kitaifa,historia ,lugha na utamaduni unahifadhiwa ambapo utafiti ni jambo la msingi.

Juni mwaka huu waziri wa michezo Dkt Amina Mohammed anayesimamia wizara ya michezo na turadhi aliweka maagano na balozi wa China Dkt Wu ,namna ya kuboresha vyumba vya kumbukumbu humu nchini.

Maulid Kitito mratibu wa shughuli zote katika makavazi ya RISSEA. Picha/ Richard Maosi

Wu alidokeza kuwa Uchina imekuwa katika mstari wa mbele kupiga jeki utalii humu nchini,kwa kuhudhuria hafla zinazolenga kuchimbua vifusi vya kale na kuvihifadhi.

Stadi ya kupiga picha,ikiwa ni kiungo muhimu kuhakikisha kuwa vyombo vya kale vimeweza kuhifadhiwa na idhibati kutolewa kupitia michoro na picha za aina mbalimbali,zinazoweza kupitiza ujumbe kwa wageni.