RIZIKI: Amejiendeleza kielimu kupitia vibarua, sasa ni mtaalamu wa masuala ya dawa
Na SAMMY WAWERU
NI mwendo wa saa kumi na moja na nusu hivi za jioni na tunakutana na mwanadada Florence Njeri kwenye duka moja la kuuza nguo jijini Nairobi, baada kukunja jamvi majukumu yake kazini.
Njeri yuko katika harakati za kununua mavazi. Anachagua sketi-suti ya maruni, na baada ya kubadilisha na kujipima katika eneo la faragha la shughuli hiyo, anaonekana mwingi wa furaha na tabasamu.
“Kuna wakati singemudu kujinunulia mavazi ya hadhi, lakini kwa neema ya Mungu sasa ninajimudu, pamoja na kuwa wa msaada kwa wengine,” adokeza mwanadada huyo.
Baraka na ufanisi huo anasema ni safari iliyochukua muda wa miaka, si mwaka mmoja, miwili au mitatu. Ni safari na masafa yaliyosheheni magumu, japo hakufa moyo.
Ipatayo miaka 18 iliyopita, Njeri alifanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE na akafuzu kwa alama C+.
Alitamani kusomea uuguzi, lakini hilo lisingewezekana kwa anachotaja kama wazazi kutokuwa na uwezo kifedha.
Akiwa kifungua mimba, nduguze pia walikuwa na kiu ya elimu kufikia alipofika, hivyo basi hakuwa na budi ila kuwapa mwanya wasomeshwe na wazazi wake.
Si kisa kimoja au viwili mtoto wa kike anapofanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, akose karo kujiendeleza kielimu hujipata kuoleka. Hata hivyo, kwa Florence Njeri wazo la aina hiyo halikumuingia kwa vyovyote vile.
Akiwa mzaliwa wa Kiambu, anasema aliamua kukita kambi Nairobi ili kutafuta vibarua kukithi mahitaji yake. Mchagua jembe si mkulima, na kulingana na mwanadada huyo, kuanzia vibarua vya dobi, shughuli za ujenzi, uuzaji wa kahawa miongoni mwa vingine, vyote alivifanya.
“Shabaha yangu ilikuwa kuweka akiba ili niweze kujiendeleza kimasomo,” aeleza.
Baada ya kulipa kodi ya nyumba na mahitaji mengine muhimu, mapato yaliyosalia aliyaweka kibindoni.
Miaka mitano baadaye, Njeri anasema alikuwa ameweka akiba iliyomuwezesha kujisajili na kujiunga na chuo kimoja kinachotoa mafunzo ya afya na matibabu jijini Nairobi. Aidha, anasema alisomea na kufuzu kwa Stashahada ya Masuala ya Huduma za Dawa, miaka mitatu baadaye.
“Haikuwa rahisi kwa sababu muda wa ziada na likizo nilikuwa katika harakati za kutafuta karo na mapato ya kukidhi mahitaji binafsi, pamoja na kodi ya nyumba,” anasema.
Isitoshe, alijinyima maisha ya hadhi ya juu ili aweze kuafikia ndoto zake.
Hata ingawa safari ya kutafuta ajira ilikuwa yenye milima na mabonde, Njeri 36, anasema alifanikiwa kupata vibarua kwenye maduka ya kuuza dawa. Kwa mujibu wa simulizi yake, baadhi ya maduka hayo, yangekosa kumlipa mshahara, jambo ambalo nusra limsababishe kujutia kozi aliyosomea.
Ni hali inayoshuhudiwa miongoni mwa waajiri wengi, hasa ikiwa mwajiri na mwajiriwa hawana mkataba wowote wa makubaliano uliotiwa saini. “Ni muhimu mwajiri na mwajiriwa wawe na mkataba unaoeleza uhalisia wa kazi na makubaliano ya kiwango cha mshahara,” anahimiza Duncan Tallam, wakili.
Mtaalamu huyo wa masuala ya sheria hata hivyo anasema serikali inapaswa kubuni sheria zitakazoongoza waajiri, ili kulinda waajiriwa.
Miaka mitatu iliyopita, Florence Njeri anasema alipata nafasi ya kazi katika kampuni moja ya usambazaji dawa jijini Nairobi, na anayosifia mikakati yake ya utendakazi.
Licha ya kuwa anapania kuanzisha familia hivi karibuni baada ya kupata mchumba, anasema katika maazimio ya ruwaza yake ya miaka mitano ijayo, analenga kujiendeleza kielimu ili apate shahada.
Kando na kuwa mtaalamu wa masuala ya dawa, amewekeza katika sekta ya uchukuzi.
Mwanadada huyo anahimiza vijana kuwa wenye maono maishani, muhimu akiwashauri kujipanga kwa mapato wanayokusanya kupitia vibarua.
“Ikiwa umejaaliwa talanta fulani, itumie ipasavyo. Jiepushe na matendo maovu yanayotishia kuzima ndoto zako. Katika kila jambo mhusishe Mwenyezi Mungu,” anashauri.