RIZIKI: Anajichumia pato kwa kuuza mishumaa yenye manukato
JANGA la corona lilipoikumba Kenya, mambo mengi nchini yalisitishwa kwa muda ikiwemo safari za ndege, wanafunzi kuenda shuleni, baadhi ya biashara, mikutano miongoni mwa mambo mengine.
Tilyan Abdulrehman, 24, anasema janga hilo lilimnyima uhuru wa kutangamana na marafiki, lakini halikumnyima nafasi ya kuwa mvumbuzi.
Juni 2020 Tilyan ambaye alihitimu elimu kwa kutunukwa shahada ya Usimamizi wa Biashara kitengo cha Kusimamia Maswala ya Wafanyakazi katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) alianzisha biashara yake changa kwa jina Scented With Hope ambayo inahusika na kutengeneza mishumaa yenye manukato yanayohanikiza na kunukia.
“Napenda mishumaa pamoja na harufu za kuvutia. Hata hivyo, nilikuwa na ndoto ya kutengeneza vitu ambavyo watu wanaweza kuvitumia kujifurahisha binafsi na visiwe ghali,” akasema Tilyan.
Anaongeza kuwa mishumaa hiyo inaweza kutumika na mtu yeyote wakati anataamuli (meditate), muda wa kusoma, kutulia, katika sherehe mbalimbali na hata kama zawadi.
“Mimi ni mpenzi wa kuandika mashairi na ninapenda kusoma sana. Nikiwasha mshumaa wangu, mazingira yanayojengeka yananisaidia kuwa makini zaidi na pia huwa sijihisi kama niko peke yangu,” akasema Tilyan akimaanisha humuondolea upweke.
Kwa sasa anaendeleza masomo yake kitengo cha Maswala ya Kusimamia Wafanyikazi katika chuo maalum cha kutoa mafunzo haya mjini Mombasa.
Mfanyabiashara huyu anasema malighafi ya mishumaa hununua humu nchini na bidhaa ambazo hazipatikani, huwa anaziagiza kutoka ng’ambo.
Bidhaa muhimu zinazohitajika kutengeneza mishumaa hiyo ni manukato, nta ya mishumaa, tambi, vikombe vya glasi, rangi yenye mafuta, karatasi za kubandika katika mishumaa iliyokamilika kutengenezwa pamoja na vifaa vya kumfungia mteja kifurushi chake baada ya kununua.
Tilyan ndiye hutengeneza mishumaa hiyo nyumbani kwao, na anasema kuwa mara nyingine mama na ndugu zake humsaidia kuitengeneza na hata kuifanyia majaribio.
“Ninamshukuru mamangu kwa kunisaidia kukuza biashara yangu na pia kuwa miongoni mwa watu ambao hufanyia bidhaa zangu majaribio, na kunipa mwongozo kuzihusu. Baadhi ya manukato huwa nayaagiza kutoka Amerika,” akasema.
Kwa sasa, anatengeneza mishumaa yenye manukato ya machungwa, vanila, peremende (peppermint), mrujuani (lavender), waridi na citronella ambayo inatumika kuwafukuza wadudu kama mbu.
“Hivi karibuni nitaongeza manukato ya mdalasini, yasimini, stroberi na mengine ambayo wateja wangu wameagiza. Mimi napenda manukato ya vanilla na yale ya mrujuani,” akasema Tilyan huku akiongeza kuwa mtu kutoka sehemu yoyote nchini anaweza kuagiza mishumaa hiyo na itawasilishwa hadi alipo.
Tilyan anasema kuwa ameuza zaidi ya mishumaa 50 katika msimu huu wa corona, na akaongeza kuwa anatunukwa sifa kutoka kwa wateja wake wakiisifu kazi yake.
“Mishumaa ya gramu 70 huwa ni Sh300 na ile ya gramu 250 ni Sh700. Kuipamba kama vile kuandika jina la mtu binafsi katika mshumaa pamoja na mapambo mengine ya kibinafsi itagharimu Sh100, na ada ya kusafirisha inategemea umbali alipo mteja,” akasema Tilyan.
Mwanabiashara huyo alisema kuwa kuweko kwa rasilimali zinazohitajika huathiri idadi ya mishumaa na aina ya manukato itakayotumika.
Alisema wateja wake ni kila mtu ambaye anapenda mishumaa yenye manukato au watu wanaopenda kutoa zawadi kwa watu wanaowajali sana.
“Siangalii jinsia, manake naamini kuwa hata wanaume wanaweza kujitengea muda kufanya mambo yao binafsi kando na kazi,” akasema.
Kwa sasa, anajipigia debe katika mitandao ya kijamii ya Twitter, Facebook, Instagram na Whatsapp.
“Nimepata wateja wengi kutoka mitandaoni haswa Instagram na pia marafiki zangu wanainua biashara zangu,” akasema Tilyan.
Alisema kuwa huwa anajadiliana na wateja wake ili kujua ni manukato gani wanataka, miundo itakayotengenezwa, maandishi na picha gani zitawekwa katika karatasi zitakazobandikwa kwa mishumaa iliyokamilika kutengenezwa.
Tilyan alisema kuwa anaweza kutengeneza mishumaa ya kusherehekea siku za kuzaliwa, harusi na aina zingine za sherehe, kulingana na vile wateja wake wamependa.
“Ningependa kupanua biashara yangu na pia kuweza kuwa na aina nyingi ya manukato. Pia, ningependa kuuza bidhaa zangu katika nchi za nje,” akasema.
Aliwaomba wanabiashara wenzake wanaoanza biashara zao binafsi wasife moja bali wajikaze hadi kazi hizo ziwe imara na ziweze kuwavunia kipato kikubwa.
“Kwa mtu yeyote anayetaka kuanza biashara, siri ni kuanza. Fedha za kuanza pamoja na rasilimali zingine zinweza kuwa changamoto, lakini ni vizuri kuanza na kile ulichonacho ili biashara ikue polepole,” akasema.