RIZIKI: Anavyojihakikishia kipato kupitia uuzaji wa mavazi ya watoto
Na SAMMY WAWERU
PEMBEZONI mwa Thika Superhighway, katika mtaa wa Githurai kiungani mwa jiji la Nairobi, Bi Purity Wangui ana furaha isiyo na kifani anapohudumia wateja wake.
Ni muuzaji wa nguo za watoto, hasa marinda, suruali ndefu, kofia za kuzuia baridi maarufu kama ‘boshori’, na mashati, miongoni mwa mavazi mengine.
Kipindi hiki ambapo shule zinatarajia kufunguliwa wiki ijayo, muhula wa kwanza, Purity amejibidiisha kuuza soksi za watoto.
“Kibanda changu ni cha mavazi ya watoto pekee. Msimu wa Desemba 2019 nilivuna sawasawa, kwa kuuza nguo mpya. Mwezi huu wa Januari, mauzo yaliyoshika kasi ni ya sweta, sare na soksi za watoto wanaporejea shuleni,” anasema mfanyabiashara huyo ambaye ni mama wa mtoto mmoja.
Kulingana naye, kibanda chake msimu huu anakifungua mwendo wa saa tatu asubuhi ili kuwahi wazazi wanaofika sokoni. Kabla wakati huo, anaraukia soko kununua stoki zaidi.
“Kila siku, ijapokuwa Jumapili pekee, huamkia Gikomba na soko la Kamukunji, jijini Nairobi, ili kukimu mahitaji ya wateja,” anadokeza.
Purity aliingilia biashara ya nguo miaka saba iliyopita.
Anasema hatua hiyo ni baada ya kuchoshwa na kazi ya kuajiriwa aliyofanya eneo la Ruiru.
“Nilikuwa keshia wa mkahawa. Kazi hiyo ilikuwa yenye presha na mikwaruzo ya hapa na pale, ilhali mshahara ulikuwa ule wa kijungu jiko,” anasimulia.
Ni kupitia ukuruba wake na mama mmoja Githurai ambapo Purity alipata motisha kuanza kufanya biashara.
“Alikuwa mwalimu wa shule ya kibinafsi ya msingi na aliacha kazi hiyo baada ya kuonja utamu wa biashara. Aliniambia alikuwa akipokea mshahara kiduchu, ambao baada ya mwezi uliishia kulipa deni. Hadithi yake iliwiana na yangu, alinipa moyo kutafuta njia mbadala kusukuma gurudumu la maisha,” anafafanua.
Kwa mtaji wa Sh60,000 tu aliwekeza kwenye biashara anayofanya sasa na kwa tabasamu anasema hajutii kamwe.
“Kwa sasa ninawafaa pakubwa wafanyabiashara wenzangu kwa sababu biashara imenikubali,” Purity anatueleza.
Hata ingawa utangulizi haukuwa rahisi, mjasirimali huyo anasema alijikaza kisabuni kuipalilia. Biashara ya nguo ni yenye ushindani mkali, na kulingana na Purity alikumbatia matumizi ya mitandao kama vile Facebook na WhatsApp kutafuta wateja, mbali na wapita njia.
Mitandao ya kijamii inasifiwa kuimarisha sekta ya biashara, hususan kwa wanaoitumia ipasavyo.
“Mbali na kufanya matangazo kwenye vyombo vya habari, wafanyabiashara binafsi, kampuni na mashirika yanapakia bidhaa zake kwenye mitandao ili kuvutia wateja,” aeleza Philip Chemweno, mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara.
Mdau huyo ambaye pia ni mhasibu katika benki moja nchini, hata hivyo anaonya wachangiaji kutoangukia kwenye mikono ya matapeli, akieleza kuna wahuni wanaohadaa watu.
“Kuna wanaofungua makundi au kurasa kutapeli. Hivyo basi unapoagiza au kununua bidhaa mitandaoni uwe makini,” Bw Chemweno ashauri, akisisitiza haja ya kulipia bidhaa unapoziona ana kwa ana.
Purity Wangui anakiri mitandao imesheheni matapeli, na kwamba kilichofanikisha kuimarisha biashara yake ni uaminifu. “Wateja wangu huwaelekeza niliko ili kujichagulia wenyewe,” asema.
Bidhaa zake anauza kati ya Sh50 – 1, 000, zile za bei ya juu zikiwa marinda ya wasichana. Mbali na misimu ya mwezi Desemba na Januari, Purity anasema wakati wa baridi sweta na fulana hununuliwa kwa wingi.
Hakuna kazi isiyokosa changamoto, anasema baadhi ya wateja nguo zinazokosa kutoshea watoto wao huzikawisha kabla kurejesha jambo ambalo wakati mwingine hutishia uhusiano wake nao. “Kwa kawaida, mteja akikawia na vazi zaidi ya wiki moja, halipaswi kurudishwa. Linapaswa kurejeshwa chini ya huo muda ili libadilishwe na linalotoshea mtoto wake. Wengine huwavisha watoto, na hata kufua, mavazi hayo ni vigumu kununuliwa na wateja wengine yanaporudishwa,” afafanua.
Wakati wa mahojiani, Purity alisema licha ya changamoto anapania kufungua duka la kijumla Mungu akimjaalia kutimiza ndoto zake.