RIZIKI: Biashara ya soksi inamsaidia kukidhi mahitaji
Na SAMMY WAWERU
SOKO la Jubilee lililoko eneo la Githurai kiungani mwa jiji la Nairobi ni tajika katika uuzaji wa bidhaa za kula kwa bei nafuu.
Kuanzia nafaka, matunda, mboga, viungo vya mapishi, miongoni mwa mazao mengine ya kilimo, hayakosi katika soko hilo.
Jubilee Market pia ni maarufu katika biashara ya nguo. Kimsingi, eneo hilo la biashara limebuni nafasi chungu nzima za ajira.
Mabasi yanayohudumu kati ya Githurai na jiji la Nairobi, pia yanajumuishwa katika ustawishaji wa eneo hilo. Pembezoni mwa yanakoegeshwa ili kupakia abiria, wachuuzi wamejituma kusukuma gurudumu la maisha.
Katika mazingira yayo hayo, tunakutana na Charles Macharia ambaye amewekeza kwenye biashara ya kipekee, inayohusisha wanaume na wanawake. Bw Macharia, ambaye angali barobaro ni muuzaji wa soksi, na ni gange aliyoizamia zaidi ya miaka mitano iliyopita.
‘Duka’ lake ni kibanda tamba kilichotengenezwa kwa mbao. Kwa kimo, kimeinuliwa takriban mita mbili (eneo la kusitiri bidhaa), juu kimeezekwa kwa karatasi ngumu za plastiki, pia nailoni. Aidha, kina upana wa karibu mita tano.
Isemwavyo, usiangalie wembamba wa reli garimoshi huipitia, kwa kijana huyo anakouzia si hoja.
“Uuzaji wa soksi kwenye kibanda ndio hunikimu pamoja na familia yangu, kuanzia kodi ya nyumba, kuwavisha, lishe na karo ya watoto wangu,” asema Bw Macharia.
Aliingilia biashara hiyo mwanzoni mwa 2014 na alikuwa miongoni mwa waliopata nafasi za kwanza Jubilee Market. Awali, Macharia alikuwa mchuuzi wa peremende na njugu.
Kulingana na maelezo ya mjasirimali huyo, ilimgharimu mtaji wa Sh5, 000, kuanzisha biashara ya uuzaji wa soksi, ikiwamo kujenga kibanda na soksi za kutangulia shughuli hiyo.
Huuza soksi za watoto kwa vijana, kina mama kwa wazee. Bei yake ni nafuu, kati ya Sh30 na Sh100.
“Huzinunua kutoka soko la Gikomba,” afichua mwanabiashara huyo.
Gikomba ni soko maarufu jijini Nairobi, na linalofahamika kwa uuzaji wa mavazi kwa kijumla na bei nafuu. “Ili kupata soksi bora, huraukia sokoni alfajiri na mapema, kabla hazijachaguliwa na wafanyabiashara wenza,” aeleza.
Isitoshe, mchuuzi huyo anasema ameweza kutambua aina ya soksi, kwa msingi wa saizi, muundo, hadhi na rangi, wanazotaka wateja wake.
Kauli yake inapigwa jeki na Samuel Wa Wanjiru, muuzaji wa biashara hiyo, akieleza kinachonogesha biashara ya uuzaji wa soksi ni kujua matamanio ya mteja. “Ukiafikia matakwa ya mteja, hutajutia kuuza mavazi yoyote yale,” asema Bw Samuel.
Kulingana na Bw Macharia, uuzaji wa soksi hushika kasi majira ya asubuhi, ambapo wengi huwa katika harakati za kuelekea kazini. “Wanaume ndio wateja wangu wakuu,” adokeza.
Vilevile Macharia anasema msimu wa wanafunzi kurejea shuleni uuzaji wa soksi huwa umenoga.
Hakuna kazi isiyokosa milima na mabonde, ubomoaji wa vibanda vya soko hilo uliofanyika mwaka uliopita na mwaka huu, ulimtatiza. “Biashara inahitaji utulivu, wateja wakija wanikose, baadhi yao hasa wasio na njia ya kunifikia upesi huenda kwingine – washindani wangu,” Macharia aeleza.
Hata hivyo, ili kujaribu kuwahifadhi na kuwaitia soksi zinapoingia hususan kutoka sokoni, ana kitabu cha kunakili nambari zao za simu, ambapo huwafahamisha.
Kujiri kwa mitandao ya kijamii pia kumechangia kuimarika kwa baadhi ya biashara. Kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaokumbatia matumizi ya Facebook, Whats App na hata Instagram, kufanya mauzo ya bidhaa, na Bw Macharia anahimizwa kuiga nyayo zao.