Makala

RIZIKI: Bidii na stahamala ni nguzo ya mafanikio ya Sophia Wanjiru 

January 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

LICHA ya kwamba Sophia Wanjiru anataja safari yake ya maisha kama iliyojaa milima na mabonde kwa sasa hilo limebaki kuwa historia.

Sophia ni mzaliwa wa pili katika familia ya watoto wanne na akiwa kwa sasa ana umrio wa miaka 34 .

Ingawa masomo ya shule ya upili chini ya mfumo unaoelekea kutiwa nanga wa 8 – 4 – 4 na mahala pake kuchukuliwa na ule wa uamilifu, CBC, yanachukua muda wa miaka minne mfululizo, Sophia alisoma zaidi ya miaka sita.

Mwanadada huyo anayetoka eneo la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu, anasimulia kuwa alipojiunga na kidato cha kwanza, 1997, ilikuwa kwa neema ya Mungu tu kwa kuwa wazazi wake hawakujimudu kifedha.

Sophia anaiambia safu hii kwamba wazazi wake walifanya vibarua vya hapa na pale, ili kukimu mahitaji yake na wazawa wenza.

“Vilikuwa vya kijungu jiko, wakati mwingine tungelala njaa,” aeleza.

Kujiunga na shule ya upili, kulingana naye ilikuwa kuwabebesha mzigo, ambao hata kuuinua na kuuwekelea mgongoni ilikuwa balaa.

Ndoto za Sophia zilikuwa ahitimu masomo ya shule ya upili, ajiunge na chuo kikuu asomee taaluma ya udaktari. Anasema kidato cha kwanza alisaidiwa na baadhi ya wasamaria wema kijijini na kanisani.

“Kidato cha pili mambo yakawa mlima, sikuwa na budi ila kuacha masomo,” afichua.

“Mtoto wa kike ana changamoto chungu nzima hasa akiwa katika umri wa kidato cha pili. Nilipata ujauzito baada ya kuhadaiwa na mwanamume aliyeniahidi makuu,” adokeza, akiongeza kusema kwamba aliishia kuoleka. Kwa mujibu wa simulizi yake, hususan ya matukio yaliyojiri, hatua hiyo ilikuwa sawa na kutia chumvi au pilipili kwenye kidonda kinachouguza.

Sophia anasema aliishia kuwa ‘mke wa nyumba’, asiye na mbele wala nyuma. Miaka miwili baadaye, mambo yalipozidi unga, aliamua liwalo na liwe, hataendelea kupitia madhila ya ndoa. “Nilitafuta vibarua nikaanza maisha upya,” asema.

Wakati wa mahojiano alisema ni kupitia uamuzi huo ambapo aliweza kuendelea na masomo shule ya upili, hadi akafanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE. Kibarua kikawa kuendeleza masomo katika taasisi ya juu ya elimu.

Sophia anasimulia kwamba aliendelea kufanya vibarua, akajisajili kusomea taaluma ya masuala ya upishi na huduma za mikahawa jijini Nairobi. “Halikuwa jambo rahisi ikizingatiwa kuwa nilikuwa na majukumu ya kulea wanangu,” anasema mama huyo wa watoto wanne.

Jitihada zake baada ya kuhitimu kozi, zilimuzesha kupata nafasi ya ajira katika kampuni ya uhasibu ya PricewaterhouseCoopers (PwC) iliyoko Westlands jijini Nairobi, kama mhudumu wa mkahawa.

“PWC ina mkahawa wa kuhudumia wafanyakazi wake,” aeleza.

Mbali na kuwa mwajiriwa, Sophia anasema pia ni mwekezaji katika biashara. Huuza mapazia ya milango na madirisha na mapambo ya maskani.

Kulingana na Dennis Muchiri, mtaalamu wa masuala ya fedha na uchumi, ili kuafikia miradi mbalimbali, unapaswa kuwa na gange ya ziada kupiga jeki mapato.

“Ni muhimu unapofanya kazi uwe na mpangilio, mshahara unapoingia uwe na wazo la uwekezaji,” ashauri Bw Muchiri.

Mdau huyo anataja sekta ya biashara, ujenzi wa nyumba za kupangisha, ununuzi na uuzaji wa mashamba au ploti, miongoni mwa mengine, kama uwekezaji mfanyakazi anapaswa kutathmini.

“Mshahara uwe haba au mkubwa, tafuta njia mbadala kujiimarisha, kazi za kuajiriwa hazitabiriki hususan wakati huu gharama ya uchumi inaendelea kupanda,” afafanua.

Hata hivyo, Bw Muchiri anahimiza haja ya kufanya utafiti wa kina kabla kuingilia uwekezaji wowote ule.

“Kwa mfano, iwapo unafikiria kuingilia shughuli za kilimo, fahamu mazao bora kukuza na soko lake, pamoja na changamoto ibuka. Pia, zingatia maeneo bora ili kustawisha unachokuza. Hilo liende sambamba na uwekezaji wa nyumba za kukodi, uuzaji na ununuzi wa ploti na biashara yoyote ile unayolenga,” asisitiza mtaalamu Muchiri.

Sophia Wanjiru anasema kabla ya kuanza uuzaji wa mapazia na mapambo mengine ya nyumba, alifanya utafiti na kugundua ni biashara isiyo na wawekezaji wengi. Isitoshe, mtandao wa wateja wake umekuwa na imani na bidhaa zake.