RIZIKI: Jinsi unavyoweza kujiimarisha kimapato kupitia kilimo cha biringani
Na SAMMY WAWERU
TANGU Kenya ianze kuwa na visa vya Covid-19, sekta mbalimbali zinazochangia ukuaji wa uchumi zimeathirika.
Kuanzia ile ya biashara, utalii, uchukuzi, kilimo, miongoni mwa nyinginezo, zote zinahisi athari na makali ya ugonjwa huu unaosababishwa na virusi vya corona.
Corona, mbali na kuyumbisha uchumi, imesababisha biashara nyingi kufungwa na maelfu ya watu kupoteza nafasi za ajira nchini.
Sekta ya kilimo licha ya kuathirika, ndiyo uti wa mgongo wa taifa hili, ikizingatiwa kuwa ni kapu la lishe. Wengi hasa wenye mashamba wamegeukia kulima, na waliojiajiri katika kilimo kukaza kamba jitihada zao.
Liwe liwalo, watu sharti wale na janga la corona limetia muhuri “wakulima ni kati ya wahudumu muhimu nchini na kimataifa kwa jumla”.
Ili kuangazia uhaba wa chakula, wakulima wanahimizwa kukuza mimea inayochukua muda mfupi kuzalisha mazao.
Mboga na viungo vya mapishi ni kati ya mimea inayochukua muda mfupi kuzalisha, aghalabu mwezi mmoja.
Biringai, ni kiungo cha mapishi na pia mboga. Ken Zachariah ni miongoni mwa wakulima wa biringani nchini, na anasema huchukua kipindi cha mwezi mmoja pekee kuanza kuvunwa, baada ya upanzi.
Isitoshe, kulingana na mkulima huyu, ni zao lisilo na ugumu wowote ule kukuza, na unaloweza kukumbatia kujiendeleza kimaisha hasa wakati huu Covid-19 imesababisha wengi kupoteza kazi.
Ken anakuza biringani na mimea mingine eneo la Magarini, Kaunti ya Kilifi. Ana uzoefu wa miaka miwili katika ukuzaji wa zao hili.
Anasema muhimu katika kufanikisha kilimo cha biringani ni kuwepo na maji ya kutosha.
“Kilimo cha biringani kinafanikishwa ikiwa mkulima ana maji ya kutosha,” asisitiza, akieleza kwamba hutumia maji ya Mto Athi, ulio mita chache kutoka shamba lake.
Aidha, Ken amekumbatia mfumo wa mifereji kunyunyuzia mimea na mashamba maji ambapo ana jenereta nne.
Anakuza biringani katika shamba la ukubwa wa ekari tatu.
“Kila ekari ina jenereta yake,” akasema wakati wa mahojiano.
Mkulima huyo alianza kilimo cha zao hilo kwenye shamba lenye ukubwa wa robo ekari.
Kwa chipukizi, kabla kuingilia kilimo cha biringani, Ken anahimiza haja ya kufanya utafiti wa kina, unaoshirikisha wataalamu na wakulima waliobobea.
“Kando na utafiti, mkulima limbukizi atumie mitandao na pia makala ya kilimo magazetini na vyombo vya habari,” anaeleza, akiongeza kusema: “Hilo litamuwezesha kujua namna ya kukuza, kutambua mbegu bora kupanda na matunzo, soko na pia kujihami na mtaji.”
Ken hukuza mbegu aina ya black beauty, miche ikichukua muda wa siku 30 sawa na mwezi mmoja kwenye kitalu. Ameibuka na mbinu ya kipekee, master pits, katika upanzi. “Ni mfumo wa kuunda shimo kubwa mfano wa ‘besini’, mashimo sita yanaandaliwa ndani yake, kila moja likisitiri mche mmoja,” akaeleza wakati wa mahojiano.
Aidha, kila ‘besini’ ina kipimo cha mita tatu, urefu, na mita mbili, upana. Huandaa mashimo yenye urefu wa sentimita 45, kuenda chini na upana wa kipimo sawa na hicho. Kulingana na Ken, mfumo huo husaidia kudhibiti uvukizi wa maji.
Alisema huchanganya udongo na mbolea ya mifugo, hususan ya kuku kwa kuwa pia ni mfugaji. “Baada ya upanzi, ninatunza biringani kwa maji,” akasema.
Matunzo mengine ni kuzuia kwekwe kwa njia ya palizi. Mazao yanastawishwa kwa fatalaiza ya kisasa, Ken akipendekeza isiyo na kemikali kutumika ili kudumisha rutuba ya udongo. “Ninapopanda kwa mbolea, huwa situmii fatalaiza yoyote ile kunawirisha mazao. Hunyunyizia maji kwa wingi,” anasema.
Wataalamu wanaonya kuwa matumizi ya fatalaiza zenye kemikali hudhoofisha udongo. “Magonjwa mengi yanayohusishwa na udongo yanajiri kwa sababu ya matumizi ya fatalaiza na dawa zenye kemikali. Wakulima wakumbatie mfumo asilia wa mbolea ya mifugo ili kudumisha rutuba udongoni, la sivyo utaendelea kuwa duni,” atahadharisha David Muriuki, mtaalamu na afisa wa kilimo Kirinyaga.
Afisa huyo pia anasisitiza haja ya wakulima kupimiwa udongo wa mashamba yao, ili kujua kiwango cha asidi na alkali, pH, kilichoko na kushauriwa namna ya kuutibu, endapo haja itajiri.
Biringani hukomaa kuanzia siku ya 30 hadi 40 baada ya upanzi. Ken Zachariah anasema huvuna kwa muda wa miezi minne au mitano, mfululizo. Kilo inauzwa kati ya Sh15 – 40.
Kwa kuzingatia taratibu bora kitaalamu, ekari moja ina uwezo kuzalisha kilo 7,000 – 8,000.
“Siri kufanikisha ukuzaji wa biringani ni kuwa na maji ya kutosha. Unapoanza kuvuna, itunze kwa maji ikiwa si msimu wa mvua,” Ken anasema.
Changamoto za biringani ni ugonjwa aina ya blight, wadudu wanaoshuhudiwa wakiwa viwavi.