RIZIKI: Jinsi unavyoweza kujipa pato kupitia utengenezaji maziwa mtindi
Na SAMMY WAWERU
JANGA la Covid-19 nchini Kenya lilisababisha kazi ya upishi aliyokuwa ameiimarisha kwa muda wa miaka kadhaa kusimama ghafla.
Pauline Kinjah anasema alikuwa amewekeza mamilioni ya pesa katika kazi hiyo, iliyokuwa ikimuingizia maelefu ya fedha kila mwezi kupitia mialiko ya hafla mbalimbali za umma.
“Miezi kadhaa kabla ya Kenya kuthibitisha kuwa mwenyeji wa Covid-19 nilikuwa nimesafiri Uchina kununua vifaa vya mapishi vyenye thamani ya Sh3 milioni,” anadokeza.
Mlipuko wa virusi vya corona uliojiri na sheria na mikakati kusaidia kuzuia msambao zaidi, uliathiri kazi yake kwa kiwango kikubwa na kulingana na Pauline nusra alemewe na msongo wa mazazo ikizingatiwa kuwa ni mke na mama.
Baada ya kutathmini jambo ambalo angefanya kusaidiana na mumewe kukithi familia yake mahitaji muhimu ya kimsingi, Pauline alianza kutoa mafunzo ya mapishi kupitia mitandao ya kijamii.
“Baadaye niliingiwa na wazo la kuuza bidhaa mbichi za kilimo, kwa sababu licha ya mkurupuko wa corona lazima watu wale. Isitoshe, katika kipindi hiki kinachohitajika sana ni chakula,” anaelezea mama huyo.
Anafichua kwamba alianza kuchuuza kwa gari lake, kisha akakodi duka katika mtaa wa Lang’ata, Nairobi, anakoishi. Bidhaa alizouza ni pamoja na mboga, viazi, karoti, matunda, nyanya, vitunguu, kati ya nyinginezo.
Baadaye, alijumuisha nafaka na unga unaotokana na nafaka hizo. Hata hivyo, Pauline anasema changamoto kuu ilikuwa bidhaa mbichi kuoza hasa zilipokosa kuisha.
“Hapo ndipo wazo la kuongeza mazao thamani liliniingia, nikaanza kutengeneza juisi ya matunda tofauti niliyouza na yaliyoathirika kwa kukosa wateja,” anadokeza.
Mbali na juisi, Pauline anasema pia alianza kuunda maziwa ya mtindi, maarufu kama ‘Yoghurt’. Mama huyo anasema maziwa ya mtindi ni kati ya bidhaa rahisi mno kutengeneza na yanayoweza kukuingizia mapato ya ziada.
Anafafanua, unachohitaji ni maziwa freshi, ‘yoghurt culture’ (kiungo cha kuyafanya yawe na uchachu), viungo vya kuyapa rangi tofauti na sukari (kwa hiari). Vifaa, ni kibuyu cha kuyafanya yawe chachu na vya kupakia.
Kulingana na Pauline, inachukua chini ya saa nane pekee kutengeneza maziwa ya mtindi.
“Unayachemsha, subiri yapoe, yaondoe samli kisha uyatie yoghurt culture. Yaweke kwenye kibuyu yachache,” anashauri.
Irene Maina, mpishi, hata hivyo, anasema badala ya kuyachemsha moja kwa moja kwenye sufuria, yatie kwenye sufuria halafu yaweke kwenye maji yanayochemka.
“Muhimu ni yapate joto. Baada ya kuyaweka kwenye kibuyu kilichofungwa yachache, viungo vya rangi tofauti na sukari ndiyo hatua ya mwisho ili yapakiwe,” Irene anaelezea.
Pauline pia anasema badala ya kutumia viungo vya rangi, unaweza kuyaweka sharubati ya matunda (smoothie) kama vile maembe, ndizi, stroberi, bukini…ili yawe ya rangi tofauti.
Kutafuta wateja si hoja, tangulia na majirani na ikiwa utayatengeneza vizuri, yatajivumisha yenyewe na kualika wanunuzi zaidi.