• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
RIZIKI: Kundi la vijana linavyopata fedha kwa kupakia lishe

RIZIKI: Kundi la vijana linavyopata fedha kwa kupakia lishe

Na PETER CHANGTOEK

TAKRIBANI kilomita saba kutoka eneo la Makutano, katika barabara ya Meru-Maua, sauti ya jenereta yahanikiza kijijini, na kuwavutia wapitanjia wenye shauku ya kutaka kujua kinachoendelea.

Mja anapokaribia katika eneo hilo, anapatana na vijana ambao wanashughulika kwa bidii ya mchwa; wengine wakiziweka foda kwa mashine ili kuzisaga, huku wengine wakipakia lishe zilizosagwa kwa mifuko spesheli.

Wao ni wanachama wa kundi linalojulikana kwa jina Spen Kenya, linalotoa huduma zao kwa wakulima wa ng’ombe wa maziwa kwa ada fulani.

Shirika hilo lilianzishwa na wanachama 12, chini ya ufadhili wa shirika lisilokuwa la serikali, maarufu kama SNV.

Shirika lilo hilo la SNV, kwanza lilianza kwa kuwapa mafunzo wanachama hao kuhusu jinsi ya kuboresha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, kupitia kwa lishe bora, utengenezaji wa lishe za silage, kudumisha usafi kwa maziwa na uhifadhi wa foda.

Hata hivyo, kundi hilo liliporomoka, na likasalia na wanachama watano pekee, na likaanza kufanya biashara ya kuwahifadhia wakulima foda kwa Sh1 kwa kilo moja, huku wakiwapa mafunzo vijana wengine katika kaunti tofauti tofauti nchini.

Wanachama wa Spen Kenya wakitumia mashine kusaga na kupakia foda. Picha/ Peter Changtoek

Mwanzoni mwa mwaka huu, wakazitumia Sh1.8 milioni kuinunua mashine kutoka nchini India, ili kurahisisha shughuli yao.

“Katika sekta ya ufugaji, ubora wa foda ni muhimu, ili kuimarisha ushindani,” asema Timothy Mbugua, mwanachama wa kundi hilo.

Mbugua anaongeza kuwa, lishe za foda zilizotengenezwa na kupakiwa, huwapa wakulima wanaowafuga ng’ombe wa maziwa walio na uhaba wa foda, na wenye mashamba madogo suluhu kwa kuwawezesha kuyazalisha maziwa kila wakati kwa mwaka mzima.

Anafichua kwamba kwa miaka kadhaa ambapo wamejifunza, wameng’amua kuwa sekta ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ambayo ni sekta kubwa, imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kuhakikisha kuwapo kwa uzalishaji mwaka mzima mfululizo. Hilo, asema, limekuwa likichangiwa na ukosefu wa foda zilizo bora.

“Kuhitajika kwingi kwa kwa foda zenye ubora, hususan wakati wa ukame, pia kumekuwa kukiwafanya wakulima kuzinunua lishe za kiwango cha chini, ambazo huathiri uzalishaji wao,” asema Peter Kirethi, mwanachama mwingine wa kundi hilo.

Robert Murage, afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo la Spen Kenya, anasema kuwa, shirika hilo lilishurutika kuinunua mashine hiyo, ambayo ina uwezo wa kufanya shughuli za kuzisaga na kuzipakia foda kwa wakati mmoja, ili kuboresha shughuli ya kuzisaga na kuzipakia lishe.

Wanachama wa Spen Kenya wakitumia mashine kusaga na kupakia foda. Picha/ Peter Changtoek

Kwa mujibu wa Murage ni kuwa, lishe za silage zisipotengenezwa vyema, husababisha hasara kwa sababu kiwango cha virutubisho muhimu hupungua, na huathiriwa na kuvu.

Baada ya kusagwa, lishe huhifadhiwa kwa mifuko spesheli zenye uzani wa kilo 50 na 60, kisha kufungwa kwa karatasi ya nailoni.

Vijana hao wanapotafutwa kutoa huduma kwa mkulima, wao hutoza Sh3 kwa kila kilo. Hata hivyo, ni sharti mkulima alipe ada za nguvukazi.

Mashine hiyo ina uwezo wa kuzisaga na kuzipakia lishe tani 10 kwa muda wa saa nane.

Wao huziuza lishe zilizopakiwa kulingana na uzani. Huuza kilo moja kwa Sh13. Kwa mwezi mmoja, wanaweza kupakia tani 200 za lishe.

Kwa mujibu wa Phillip Oketch, mtaalamu wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, katika shirika la SNV, kununua lishe zilizopakiwa kuna manufaa kwa wafugaji, kwa sababu hawatahangaika na kufadhaika wakitafuta mabua ya mahindi, mashine ya kusaga, na watu wa kupakia.

“Pia, wakulima watajua uzani wa lishe na ubora wazo, kwa sababu zina asilimia 100 ya virutubisho,” afichua mtaalamu huyo.

Ili kupunguza gharama, kundi hilo, aghalabu huwahudumia wakulima wenye mashamba kuanzia ekari tatu na kuenda juu.

You can share this post!

Injera tayari kwa raga ya dunia ya IPL World Tens

RIZIKI: Ukuzaji na uuzaji wa miche wafaidi vijana