• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
RIZIKI: Kutoka vibarua vya ujenzi na udobi hadi kumiliki biashara

RIZIKI: Kutoka vibarua vya ujenzi na udobi hadi kumiliki biashara

Na SAMMY WAWERU

BAADA ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE mwaka 2012 Milcah Muthoni hakuweza kujiendeleza kimasomo.

Alizoa alama C + na anasema alitamani kusomea uuguzi lakini kwa sababu ya ukosefu wa karo hilo halikuwezekana.

Kozi mbadala ilikuwa masuala ya biashara.

“Wazazi wangu hawakujiweza kifedha hivyo basi sikuweza kujiendeleza kielimu,” aeleza.

Muthoni anasema alitafuta njia mbadala kusukuma gurudumu la maisha.

Anasimulia kwamba miaka miwili baadaye, alikutana na mwanamume ambaye aliishia kuwa mchumba wake, na hatimaye wakawa mume na mke.

Katika ndoa hakuna kinachoridhisha wanandoa kama kujaaliwa mtoto au watoto, na Muthoni anadokeza kwamba walijaaliwa mtoto wa kiume.

Mwanadada huyo anasema miaka ya kwanza uhusiano wao ulikuwa mithili ya chanda na pete.

Hata hivyo, ndoa yao ilianza kuingia doa kupitia mashemeji wake.

Lililoanza kama mzaha lilitunga usaha, ambapo mashemeji zake walishinikiza mumewe kutafuta mke mwingine.

“Hawakunieleza sababu halisi ya kunichukia. Nilitetea kudumisha ndoa yetu lakini haikuwezekana,” anasema.

Kilele kikawa kupokezwa talaka na kufurushwa katika ndoa yake. Huo ulikuwa mwaka wa 2018.

Kwa uhakika ulikuwa wakati mgumu kwa mama huyo, akisema hakuwa na mbele wala nyuma.

Licha ya jitihada zake, kuhusisha wazazi wake, maji tayari yalikuwa yamemwagika na yasingezoleka.

Aliamua kuondoka, ingawa si kwa hiari yake, Muthoni akisema alikuwa amejitolea kwa hali na mali kuimarisha ndoa yake.

Akishauri kuhusiana na masaibu ya mwanadada huyo, mhubiri Samuel Mwaniki anasema ndoa inapoingiliwa na mtu wa tatu ni muhimu mume au mke kusimama kidete na mchumba wake.

“Ndoa ni ya watu wawili, wengine ni wa kutia chumvi na chuku,” asisitiza.

Hata hivyo, anasema mambo yakizidi unga haja ipo mwathiriwa kuondoka mara moja ili kukwepa dhuluma. Pia anashauri umuhimu wa kuhusisha wazazi, mhubiri au mshauri wa masuala ya ndoa.

Ndoa ya Milcah Muthoni iligonga mwamba na anasema hakuwa na budi ila kuenda zake.

Anasema alikita kambi Nairobi, ambapo alifanya vibarua vya hapa na pale, ikiwamo shughuli za ujenzi na dobi.

Muthoni anaiambia ‘Taifa Leo’ kwamba mwanzoni mwa 2019 alianzisha duka la bidhaa za kula Kasarani, Kaunti ya Nairobi, kwa mtaji wa Sh30, 000, biashara ambayo inaendelea kukua.

“Inaniwezesha kulipa kodi, karo ya mtoto wangu na kujiendeleza kimaisha,” akasema wakati wa mahojiano.

Katika ruwaza yake ya miaka kumi ijayo, Muthoni 25, anasema anapania kufungua duka la kijumla. Isitoshe, anasema maazimio yake ni kuona amebuni nafasi tele za ajira kwa vijana.

“Alfajiri na mapema niamkapo, hupiga dua kwa Mwenyezi Mungu anitimizie ndoto hizo,” aeleza.

Pia anasema analenga kujiendeleza kielimu, ambapo anaazimia kusomea masuala ya biashara ili kuimarisha jitahada zake.

  • Tags

You can share this post!

AFYA: Faida za majani ya giligilani/ korianda katika mwili...

Magoha na wenzake waitwa bungeni

adminleo