RIZIKI MASHINANI: Fundi stadi mlemavu anayeunda hela kwa ushonaji viatu Kisumu
Na CHARLES ONGADI
KATIKA miaka ya nyuma wengi waliamini kwamba maisha hayawezi kumnyokea mtu pasi elimu ya kutosha ya kumwezesha kuajiriwa katika ofisi kubwa mijini.
Kipindi hicho kwa wachache ambao hawakujaliwa kupata elimu ya msingi wala ya upili walichukuliwa kama waliofeli katika maisha.
Lakini kwa Mzee Angelius Okewe Orowe, 60, licha ya kutopata elimu ya sekondari maisha kwake ni shwari baada ya kujifunza ufundi wa kushona viatu.
Pembezoni mwa barabara kuu ya Nairobi kuelekea Kisumu mjini kuna kituo kidogo cha biashara maarufu kama Nyar Bwana Trading Centre katika kijiji cha K’Ochieng’, Kano kaunti ya Kisumu, hapa ndipo Mzee Orowe husakia mkate wake wa kila siku.
“Mimi sikujaliwa kupata elimu ya sekondari ila nilibahatika kujifunza ufundi wa kushona viatu. Hii ni kazi ambayo ni ngao yangu maishani, ” asema Orowe katika mahojiano na AkiliMali hivi majuzi.
Kwa kipindi cha miaka 34, Mzee Orowe amehudumu kama fundi wa kushona viatu, kazi anayoifanya kwa uadilifu mkubwa.
Aidha, kwa mujibu wa mzee Orowe, kabla ya kuamua kujitosa mzimamzima katika kazi hii ya ufundi, aliwahi kuajiriwa katika kampuni ya majani chai mjini Kericho kama mchuma chai .
Lakini baada ya kupigwa kalamu, Mzee Orowe hakukata tamaa maishani bali aliamua kujitosa katika sekta ya ujenzi kama mwashi.
Ulipotimu mwaka wa 1985, mambo yalimwendea tenge alipopata ajali mbaya ya barabarani ambayo nusura imtoe uhai.
Miguu yake miwili ilivunjika na hivyo kumlazimu kutembea kwa mikongojo hali iliyobadilisha maisha yake kabisa.
“ Sikukata tamaa wala kutaka kuonewa huruma na kujigeuza ombaomba barabarani kama baadhi ya walemavu wafanyavyo bali niliamua kutumia ujuzi nilioupata nikiwa mdogo kulea familia yangu,” afichua Orowe.
Mara baada ya kupata nafuu, mzee Orowe aliamua kutumia kiasi kidogo cha hela alizokuwa nazo kuwa mtaji wa kuanzisha biashara yake mjini Eldoret mwaka wa 1985.
Alianza kwa kununua sindano ya kushona, gundi, rangi tofauti za viatu, brashi na uzi. Baada ya kipindi kifupi wateja walianza kumkubali kutokana na ustadi wake wa kushona na kung’arisha viatu.
Lakini mambo yalimwendea mrama mwaka wa 2000 wakati uongozi wa mji wa Eldoret uliamua kuwaondoa wafanyabiashara wote wanaohudumu kando kando ya barabara za mji huo.
Ni hapo ndipo mzee Orowe aliamua kufungasha virago vyake na kutua katika soko dogo la Nyar Bwana Trading Centre kuendeleza biashara yake ya ufundi.
Ijapo alikumbana na changamoto nyingi, usanifu wake kazini ulimwezesha kujipatia wateja wengi hasa walimu wanaofunza katika shule ya karibu ya msingi na upili ya Otieno Oyoo, maafisa wa polisi wanaohudumu katika kituo cha polisi cha Rabuor, wakazi wanaoishi eneo hilo miongoni mwa wateja wengine wengi wanaomfikia kila uchao.
Mzee Orowe anasema hela alizozipata zilimwezesha kujijengea himaya nzuri ya kibiashara jambo ambalo limwezesha kujirundikia hela si haba ambazo nazo zimemwezesha kuwapa wanawe elimu bora.
“Nakumbuka mwaka wa 2015 wanangu watatu walikuwa katika shule ya upili na nilimudu kuwalipia karo kupitia kwa kazi hii yangu ya ufundi,” “ aeleza mzee Orowe.
Ijapo Mzee Orowe alidinda kufichua kiasi cha hela anazopata kwa siku, anakiri kwamba ni kazi iliyo na tija licha ya baadhi ya vijana wa kileo kuibeza.
Hata hivyo, fundi huyu anayejivunia ujuzi wa miaka mingi anasema kwamba siri yake ya pekee ambayo imemwezesha kudumu kwa kipindi kirefu katika kazi hii ni kujituma, uvumilivu na muhimu zaidi uaminifu kwa wateja wake.
Kati ya changamoto anazozipitia ni hali yake ya ulemavu ambayo aghalabu huwa ni vigumu kwake kusafiri kwa urahisi hadi mjini Kisumu kununua vifaa vya kazi.
Pia kuna kipindi ambacho biashara huwa chini hasa msimu wa kiangazi ambapo humlazimu kutumia akiba aliyoweka kusukuma gurudumu la maisha.
Kutokana na kuzidi kuongezeka kwa wateja wake, Mzee Orowe anapania kutanua zaidi biashara yake pindi atakapopata hela za kutosha kufanya hivyo.
Anawaasa vijana wanaochipuka kuzingatia kazi za ufundi badala ya kuwazia tu kuajiriwa.
Mzee Orowe ni mwalimu wa wengi. Amewafunza vijana wengi kazi hii na kwa sasa wanavuna matunda mazuri ya maarifa yake.