• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:01 PM
RIZIKI: Mwalimu aliyejinyima mengi kujiendeleza kielimu sasa anajivunia bidii yake hiyo

RIZIKI: Mwalimu aliyejinyima mengi kujiendeleza kielimu sasa anajivunia bidii yake hiyo

Na SAMMY WAWERU

AKIWA darasani Peninah Ngeteta ambaye ni mwalimu katika shule moja eneo la Thika, ni mwenye furaha ya kipekee.

Chokaa na kitabu mkononi, Peninah amejituma kuondoa uzuzu kwa wanafunzi, watoto ambao ni viongozi wa kesho.

Kila anapotazama ubao, kuandika na kuwaongoza, anatabasamu kwa kuwa ni mojawapo ya gange aliyoitamani tangu akiwa mchanga, yaani mdogo kiumri.

“Nikiwa shuleni, nilitamani sana kuwa muuguzi, la sivyo niwe mwalimu. Hatimaye nilifanikiwa kuwa mwalimu,” anaelezea.

Hivyo basi, anasema ni kazi anayoifanya kwa moyo wake wote.

Hufunza Somo la Hisabati na Sayansi, madarasa ya juu, kuanzia darasa la nne hadi nne, chini ya mfumo mpya wa uamilifu ndio CBC, yanajulikana kama gredi.

Peninah anasema huraukia majukumu asubuhi na mapema.

“Kwa kawaida, majira ya asubuhi walimu huwa na mengi hasa kusahihisha kazi ya ziada, kuandaa mpangilio wa masomo ya siku, hivyo basi huhakikisha nimewahi saa ili nijipange barabara,” afafanua.

Akiwa katika wito huo, Mwalimu Peninah ni mwenye tabasamu chungu nzima.

Ni tabasamu inayoficha mengi, akikumbuka safari ya milima na mabonde aliyopitia kufikia aliko sasa. Baada ya kufanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, KCSE, 2013, Peninah anasema alizoa alama ya C+.

Mwalimu Peninah Ngeteta. Picha/ Sammy Waweru

Hata hivyo, kulikuwa na kizingiti kimoja tu kilichomkodolea macho; ukosefu wa karo kujiendeleza kielimu.

Peninah anasema kufanikiwa kusoma shule ya upili ilikuwa kwa neema ya Mungu, kwa kile anataja kama juhudi za wazazi wake kujikaza kisabuni licha ya kuwa hawakuwa wamejiweza kifedha vile.

“Kwa hakika walijikakamua na kujinyima mengi muradi niweze kusoma. Wamekuwa wa baraka maishani mwangu licha ya hali yao,” aeleza, akifichua kwamba walifanya shughuli za kilimo na ambazo kwa kiasi fulani hazikuwa na mapato ya kuridhisha.

Akiwapongeza, Peninah anasema ni wazazi ambao wanafahamu umuhimu wa elimu, hivyo basi hawakuwa na budi kujinyima.

Baada ya KCSE, anasema hakuwa na lingine ila kuwaruhusu wasomeshe wazawa wenza, ambao pia walikuwa na kiu cha elimu.

Ni katika ziara yake eneo la Thika ambapo Peninah alitangamana na mmiliki mmoja wa duka la bidhaa za kilimo, na anayesema alimpa nafasi ya kazi.

Anasema alitumia fursa hiyo kuweka akiba ambayo ilimwezesha kujiunga na taasisi moja ya mafunzo ya ualimu mjini Thika.

“Hata ingawa maisha hayakuwa rahisi, niliweka kando kiasi fulani cha pesa kupitia mshahara niliolipwa,” asema.

Mwalimu huyo anasema nidhamu katika matumizi ya pesa ndiyo nguzo ya ufanisi katika azimio la kila mmoja, na alikumbatia hilo.

Ni kauli inayopigwa jeki na Michael Muriuki, mtaalamu wa masuala ya fedha, uchumi na biashara.

“Kuna njia nyingi za kuweka akiba, japo la mno ni nidhamu katika matumizi ya pesa ili kupata akiba yenyewe,” Muriuki asisitiza.

Kulingana na Peninah Ngeteta, mwishoni mwa 2015 alikuwa ameweka akiba kitita cha pesa kilichomuwezesha kujiunga na chuo cha ualimu Thika.

“Niliafikiana na mwajiri wangu niwe nikitoka kazi mapema, ili niweze kujiendeleza kimasomo,” asema.

Anaendelea kueleza kwamba safari hiyo haikuwa rahisi kamwe, kwani ni mengi alijinyima ili aweze kuafikia maazimio yake.

“Ratiba yangu ilikuwa kazini asubuhi hadi alasiri, kisha jioni darasani. Kilikuwa kibarua ambacho si rahisi,” aeleza.

Miaka mitatu baadaye, Peninah alifuzu kwa Stashahada ya Mafunzo ya Ualimu.

Anasema alikuwa na bahati kama mtende, kwa kuwa alibahatika kupata nafasi ya kazi katika shule moja ya msingi ya mmiliki binafsi, Thika, ambapo anafunza kufikia sasa.

Wakati wa mahojiano alisema anapania kujiunga na serikali, ambapo kila mwaka nafasi za kazi zinapotangazwa hujaribu bahati yake. Alisema anatazamia kusomea Shahada, mikakati ambayo ameiorodhesha katika ruwaza yake ya miaka saba ijayo.

Aidha, anapenda kusoma magazeti na majarida, akifichua anapenda gazeti laTaifa Leo’.

You can share this post!

Atwoli atoa salamu za pole kwa familia ya Moi, afananisha...

Ajeruhiwa baada ya boti kushika moto baharini

adminleo