RIZIKI: Mwalimu, mwokaji keki na mtengenezaji wa bidhaa za shanga
Na MARGARET MAINA
MWALIMU wa shule ya upili kwa sasa anaoka keki na kujihusisha na sanaa ya shanga kipindi hiki cha janga la Covid-19 ambapo shule zingali zimefungwa.
Tangu agizo la serikali la kufunga shule, Bi Lucy Macharia wa shule ya sekondari ya Ndururumo iliyoko Nyahururu amekuwa akijishughulisha na mambo tofauti ya kumwezesha kupata hela.
“Ni safari ya kujitambua. Kwa miaka mingi nilipenda kazi ya mikono, ambayo nilijifunza kutoka kwa mama yangu. Nakumbuka mara nyingi nilikuwa nachukua vyombo vyake nikijaribu kufanya kama yeye. Kwa upole alikuwa akinisahihisha na kunitia moyo,” anaambia Taifa Leo.
“Mnamo mwaka wa 2017, nilifanyiwa upasuaji wa goti na nikalazwa kwa miezi mitano. Hapo ndipo nilifikiria kujaribu sanaa ya kutengeneza bidhaa za shanga. Nilianza na mikeka ya mezani,” anasema.
Bi Macharia alianza pia kutengeneza vishikizi vya funguo, vishikizi vya serviettes, mikoba na vikapu.
“Nilianza kupeana kama zawadi na wakati nilipona goti na kuripoti shuleni, nilikuwa nimetengeneza vishikiliaji vya funguo vingi vya shanga ambavyo niliwapa wanafunzi wangu kuwatia hamasa; hasa watahiniwa waliofanya mitihani ya tathmini endelevu kwa kujiandaa kwa ajili ya mitihani yao ya mwisho,” anasema.
Hatua hii iliwafanya wanafunzi kujitahidi ili kupata zawadi wakati wa matokeo kwa kila mtihani waliofanya.
Kazi hizi za mikono zimemfanya mwalimu huyu wa sayansi ashughulike nyumbani anapoendelea kupona kutokana na upasuaji mara tatu mfululizo wa goti tangu 2017.
“Nilitengeneza pia ‘shaggy mats’ kwa kufuata utaratibu kutoka kwa YouTube. Leo ninafanya hivi kupata hela za ziada mbali na kazi yangu ya ualimu. Wateja wangu wengi ni marafiki; hasa kutoka eneo langu na pia marafiki wengine ambao nimekutana nao kwenye mitandao ya kijamii,” anaeleza.
Bi Macharia pia amekuwa akioka keki na mikate. Ni ujuzi ambao alijifunza kutoka kwake mama mzazi.
“Nilifurahiya kupika tangu nikiwa na umri mdogo sana, na hii ilikamilishwa baada ya kuhitimu kozi ya digrii ya Sayansi ya Nyumbani na Teknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Moi Eldoret. Nilianza kuoka keki za siku za kuzaliwa za ndugu zangu na pia sherehe,” anasema.
Mazoea yalijenga ustadi hivyo akaanza kuoka kibiashara.
“Leo, mimi hutengeneza keki kwa hafla zote ikiwa ni pamoja na siku za kuzaliwa, harusi, uchumba, maadhimisho ya miaka, kufuzu kwa wanafunzi vyuoni na sherehe zingine nyingi,” anasema Bi Macharia.
Keki ya kawaida anauza Sh1,000 kwa kilo, wakati keki kama ya harusi itagharimu hela zaidi kutegemea viungo na aina ya mapambo.
Shaggy mats huanzia Sh1800 kwa kila mita mraba. Vishikizi vya serviettes huanzia Sh750 hadi Sh1,000 kulingana na saizi, wakati kikapu cha umbo la kiondo akiza kati ya Sh1,500 hadi Sh2,500.