• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 5:55 AM
RIZIKI: Ndoto zake za biashara ‘hazikufa’ licha ya kukosa fursa kujiendeleza zaidi kimasomo

RIZIKI: Ndoto zake za biashara ‘hazikufa’ licha ya kukosa fursa kujiendeleza zaidi kimasomo

Na SAMMY WAWERU

BAADA ya kufanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE 2002) Bi Alice Wanjiku alikuwa na matumaini makuu kufua dafu ajiunge na shule ya upili, kisha asomee kozi ya uhasibu aliyoitamani tangu utotoni.

Alizoa alama 370 kwa jumla ya 500 zinazowezekana, na akapata mwaliko wa kujiunga na mojawapo ya shule bora za wasichana nchini.

Matamanio yake hata hivyo hayakuwezekana kwa kile anataja kama ukosefu wa karo, uliozima ghafla ndoto zake. Wanafunzi walipoanza kujiunga na kidato cha kwanza, wiki ya kwanza iliisha, ya pili ikafuata, ya tatu, mwezi, miezi miwili na hatimaye muhula akiwa na matumaini atapata mfadhili.

“Wazazi wangu walifanya vibarua vya kijungu jiko, vilivyotukimu riziki pekee. Mavazi tuliyanunua kupitia udobi. Hivyo basi kupata karo ingekuwa kibarua kigumu,” anasimulia Wanjiku.

Maazimio yake yalitia nanga licha ya juhudi zake kutafuta mfadhili, bila mafanikio.

Sharti gurudumu la maisha lisukumwe, na Wanjiku anasema hakuwa na budi ila kufanya vibarua vya hapa na pale ili kusaidia wazazi angaa kulea wazawa wake.

Wanjiku ambaye ametoka kaunti ya Murang’a alifanya vibarua tofauti tofauti, kikiwamo cha dobi, kulimia watu mashamba na ujenzi.

“Niling’ang’ana ili wazawa wangu wahitimu darasa la nane na ikiwezekana waingie shule ya upili,” asema.

Mtoto wa kike anapobaleghe huwa na changamoto nyingi zinazomzingira, na kulingana naye miaka minne baadaye alikutana na mwanamume aliyemhadaa na kuahidi kumuoa.

Anakumbuka barabara ilikuwa 2006, alipoitikia posa na bila ati ati, wakawa mume na mke.

Maisha wakati wa kuchumbiana na katika miaka ya kwanza ya ndoa yalikuwa matamu.

Miaka mitatu baadaye, walijaliwa kifungua mimba na ndipo Wanjiku anasema ndoa ilianza kuingia doa.

Anasimulia kwamba mume wake alitekwa nyara na unywaji wa pombe kupindukia, kiasi cha kuasi majukumu yake na hata kuzua vita. Juhudi zake kuhusisha wazazi kumrekebisha, hazikuzaa matunda.

Hata baada ya kujaaliwa mtoto wa pili, Wanjiku anasema tabia zilikuwa zile zile. Anasema hakuwa na budi ila kuondokea madhila ya ndoa. Hatua hiyo ilikuwa mithili ya kutia chumvi kwenye kidonda kinachouguza.

Wanjiru anaiambia safu hii kwamba alihamia jijini kuzimbua riziki, ili aweze kulea familia yake changa. “Sikubagua kazi muradi tu ni halali,” asema. Vibarua vilivyopatikana upesi ni vya ujenzi, na anasema ni katika harakati hizo aliweza kuweka akiba kima cha Sh100, 000, kwa muda wa miaka mitano mfululizo.

Anaeleza kwamba mtaji huo aliwekeza kwenye duka la kuuza mvinyo kijumla. Ni biashara yenye changamoto hasa wakati wa utangulizi, kwa sababu leseni zinazohitajika.

“Licha ya kuhangaika kupata leseni, sikufa moyo. Hatimaye nilifanikiwa, na kazi inaendelea,” asema. Biashara hiyo imenoga kiasi cha kumuwezesha kununua kipande cha ploti Nairobi. Tayari mama huyo ameanza shughuli za ujenzi wa nyumba za kupangisha.

Wakati wa mahojiano, Wanjiku alisema ili kuanzisha biashara ya uuzaji wa mvinyo kijumla inahitaji mwekezaji kujipanga sawasawa. Aidha, alisema leseni ndizo hugharimu kiasi kikubwa cha pesa.

“Kuna leseni ya baraza la kaunti, Bodi ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini (Nacada) na zinginezo kwa mujibu wa sheria zinazodhibiti vileo nchini, na zinahitaji pesa,” akasema.

Wanjiku, 32, ameajiri mfanyakazi mmoja anayemsaidia hasa anaposimamia ujenzi wa ploti yake.

Pia anasema hufanya biashara ya uuzaji wa nguo kupitia mitandao ya kijamii, ambayo humlazimu kusafiri kufikisha bidhaa kwa wateja.

Miaka 18 baada ya ndoto zake kujiendeleza kimasomo kufika kikomo, Wanjiku anasema jitihada zake zimemuwezesha kwa kiasi fulani kuafikia matamanio yake kuwa kwenye sekta ya biashara.

Kwa kuwa sasa ana uwezo kifedha, anashauriwa kujiunga na masomo ya ziada, ngumbaru, katika shule ya upili.

“Kuna taasisi zinazotoa mafunzo ya masomo ya shule za upili, wengi licha ya kuwa kwenye familia na kuzidi umri wanajiendeleza kimasomo na hata kujiunga na vyuo vikuu na anuwai,” ahimiza Boniface Gathogo, mhadhiri wa chuo anuwai.

Kulingana naye, hatua hiyo itamfanikisha kusomea uhasibu ili aweze kuimarisha biashara zake.

  • Tags

You can share this post!

Mgogoro wa kiitifaki wanukia Mombasa mkutano wa uhamisisho...

Sonko akesha akiomba kesi ya kuvamia askari itupwe

adminleo