RIZIKI: Ususi unavyomkimu
Na SAMMY WAWERU
ARAUKAPO asubuhi, ratiba ya Mary Maina huwa yenye shughuli tele kila siku angalau kusukuma gurudumu la maisha.
Mary ambaye ni mzaliwa wa Nyeri, ingawa ni mkazi wa Kinungi, Naivasha, anafanya kazi ya ususi tamba; usukaji nywele kupitia mialiko.
Baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, ipatayo miaka 21 iliyopita, Mary anasema alikuwa na hamu kujiendeleza kimasomo na pindi tu baada ya kuhitimu kozi aliyotamani aanzishe familia.
Hata hivyo, moja lilijiri kabla ya jingine, alioleka kabla kujiunga na taasisi ya elimu ya juu kusomea masuala ya ususi na urembesho (hair dressing and cosmetology).
“Nilipata mume mbele, kabla kujiendeleza kimasomo hivyo basi sikuwa na budi ila kuanzisha familia,” asema, akisisitiza umri haukuwa hoja kwake kuwa mke na pia mama.
Kwa kawaida, matunda ya ndoa ni kujaaliwa mtoto au watoto, na miaka kadha baada ya kuwa mume na mke, vibarafu hao wa moyo walijaaliwa kupata mtoto wa kiume.
Kwa kawaida katika uhusiano, siku, miezi au miaka ya kwanza, wachumba au wanandoa huogelea katika bahari ya raha, kibwagizo kikiwa ‘nipe-haya pokea, nahitaki-nitakuhitimishia…’ na kulingana na Mary miaka ya kwanza katika ndoa yake, mambo yalikuwa matamu na mteremko. Mapenzi yalinoga.
Walipokutana, bwana alikuwa akifanya vibarua vya hapa na pale. “Alipoajiriwa na serikali ya kitaifa, alifunguka macho na kutafuta mke mwingine aliyedai ni wa hadhi yake,” asimulia Mary. Licha ya kuhusisha familia wa pande zote mbili, wa Mary na mume wake, ili kusuluhisha masaibu yalioibuka, mume hakubadilisha mawazo “hakuskia la mwadhini wala la mteka maji msikitini”.
Ndoa iliyodumu karibu miaka kumi, kilele chake kikawa Mary kutalakiwa.
“Sikuwa na jingine ila kuitikia matokeo, nilijifunza uhusiano au ndoa hailazimishwi,” aeleza.
Ni katika mchakato wa kuuguza majeraha ya moyo kutemwa na mume anayedai alimpenda kwa dhati kiasi cha kusaliti matamanio yake kujiendeleza kimasomo, alipokumbuka ana vyeti vya KCSE. Mary 39, alikuwa amezoa alama ya C+ na bila kupoteza wakati alijisajili katika chuo kimoja jijini Nairobi akasomea kozi ya ususi na urembesho.
Anasema, alikuwa akifanya vibarua vya hapa na pale na pia kupigwa jeki na wazazi wake ili kulipa karo.
Mary anaeleza kwamba baada kukamilisha, mambo hayakuwa rahisi kama alivyotarajia kwani ni kazi inayohitaju uvumilivu wa hali ya juu. Katika shughuli za ususi, wanawake huwa makini kwa anayewahudumia, na wengi wana wasusi halisi.
Mwanadada huyo anaiambia ‘Taifa Leo’ kuwa alikabiliwa na kibarua cha kutafuta wateja, jambo analosema si rahisi. “Nilianza kwa wanafamilia na marafiki ambao wamenifaa pakubwa katika kuvutia wateja,” aelezea.
Hata hivyo, Mary anasema kushawishi wateja kupata huduma zake ilimchukua muda. Anaendelea kueleza kwamba anafanya ususi tamba, ambapo hupokea mialiko ya wateja waliko.
Mbali na usongaji wa nywele, Mary anafichua kwamba hutoa huduma za unyooshaji wa viungo vya mwili, maarufu kama ‘massaging’. Gharama ya huduma zake ni kati ya Sh100 – 5, 000 malipo yakitegemea na muundo au staili ya nywele.
Wakati wa mahojiano tulikutana naye kiungani mwa jiji la Nairobi, ambapo alikuwa ametoka kuhudumia mteja eneo la Thika.
“Wakati mwingine gharama ya usafiri huniacha na faida kidogo, kwa kuwa ninapotoza malipo lazima niijumuishe,” akasema, akieleza baadhi ya changamoto anazopitia.
Ili kuweza kuimarisha huduma zake, Mary Maina anashauriwa kufanya matangazo ya kutosha. Kwa kuwa matangazo kupitia vyombo vya habari ni ghali, msusi huyo anahimizwa kutumia mitandao.
“Teknolojia imerahisisha mambo, wafanyabiashara wanatumia mitandao kama vile Facebook, Instagram na WhatsApp kuvumisha huduma na bidhaa zao,” anasema Samuel Karanja, msusi hodari jijini Nairobi na anayetumia mitandao kuvumisha huduma zake kuvutia wateja.
Karanja anasema alianza kama msusi tamba ambapo ana makundi mbalimbali kwenye mitandao, na ambayo huyatumia kupakia picha za huduma za ususi anazotoa.
“Huandamanisha picha na nambari za simu ili wateja waweze kunifikia upesi,” aeleza, akishauri Mary kukumbatia hilo.
Karanja ana maduka kadhaa ya ususi kiungani mwa jiji la Nairobi, maarufu kama saluni. Anasema ni rahisi kuelekeza wateja aliko, bila kusahau kujiondolea gharama ya usafiri.
Kwenye ruwaza yake, anayoipa miaka miwili ijayo kutoka sasa, Mary anaapa atakuwa amefungua duka la shughuli hiyo. Kando na ususi, pia hufanya uuzaji wa nguo.