RIZIKI: Uyatima, hali ngumu ya maisha haikuzima ndoto yake kuwa mwalimu
Na SAMMY WAWERU
KWA kawaida mtoto anapozaliwa hukaribishwa kwa shangwe, vifijo na nderemo na familia yake ambao ni wazazi na wanaohusishwa kwa karibu nao.
Madaktari na wauguzi wakijibidiisha kuhakikisha anazaliwa salama, malaika hulia, huku mama akijawa na tabasamu na furaha kushuhudia baraka.
Ipatayo miaka 32 iliyopita, taswira hiyo ndiyo ilikaribisha Caroline Muthoni alipozaliwa, ingawa hakuna alichofahamu.
Anachokumbuka, ni aliyoelezwa alipofikisha umri wa kufahamu mbivu na mbichi, kwamba alikuwa mtoto mtulivu, mchangamfu na mtiifu.
Unapokutana naye, ana kwa ana, kwa hakika anawiana na hulka hizo. Ni msichana mfupi kwa kimo, mrembo na ambaye rangi yake ya ngozi ni kivutio cha wengi.
Anapozungumza, hakosi kutabasamu huku ucheshi ukimtawala. Hata hivyo, ni hulka zinazoficha mengi, magumu na mazito aliyopitia.
Hata ingawa hakujua kilichoendelea akiwa mchanga, yaani mdogo kiumri, Muthoni anafichua kwamba yeye ni yatima.
Licha ya hali hiyo, ana kila sababu ya kutabasamu na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kujaaliwa ‘mzazi’ aliyemkumbatia.
“Amenilea kama mwanawe, na kuchukua nafasi ya mzazi,” Muthoni anaelezea.
Matamanio yake baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, miaka kadhaa iliyopita yalikuwa ajiunge na taasisi ya elimu ya juu kusoma kozi, kisha kwa neema za Maulana akipata mchumba aanzishe familia.
Kulingana na Muthoni, familia ndiyo ilitangulia kabla ya kusomea taaluma aliyomezea mate.
Hilo lilijiri baada ya kukutana na mwanaume anayesema alionekana kuwa komavu na tayari kuwa kwenye ndoa.
“Niliitikia posa lake, na tukajaaliwa mtoto wa kiume,” anafichua.
Anasimulia kwamba nyakati za kwanza, ndoa yake ilikuwa mteremko na aliifurahia.
“Nililijilipia karo kusomea kozi ya ualimu nikiwa kwenye ndoa,” anadokeza.
Muthoni amesomea masuala ya chekechea ndiyo ECDE, na pia anasema ameweza kujiendeleza na kupata kozi ya madarasa ya juu, hadi darasa la nane (P1).
Ndoa yake iliyodumu kipindi cha muda wa miaka minane mfululizo, anasema ilianza kuingia doa mumewe alipoanza kuasi majukumu yake kama baba na mume.
“Kilichoniuma moyo zaidi ni kulala nje usiku, ishara ya kuenda nje ya ndoa. Ninachothamini zaidi kwenye uhusiano na ndoa ni uaminifu na uvumilivu wa changamoto zinazoweza kutatuliwa,” anaelezea.
Muthoni anasema kwamba matukio hayo yalimkosesha usingizi, na mambo yalipozidi unga hakuwa na buda ila kuipungia kwaheri ndoa yake.
Huku mwanadada huyo akihisi alihitaji muda kutathmini mchumba wake, Askofu Wilson Karanja ambaye ni mshauri wa masuala ya ndoa, anasema kiini cha mahusiano na ndoa nyingi kuvunjika au kusambaratika ni “kukosa kupekua historia na tabia za mwenzako kabla kuoana”.
Kulingana na mtaalamu huyo, kuchumbiana ni jukwaa muhimu kusoma na kujua mwenzako ndani na nje, ili kufanya uamuzi ikiwa utaendelea na uhusiano au la.
“Si rahisi kutambua tabia za mtu kwa siku moja, mbili au tatu; jipe muda, mtangamane mara kwa mara, na mfunguliane nyoyo zenu,” Bw Karanja anahimiza.
Muhimu pia kulingana na Askofu huyo ni kushirikisha Mungu katika kila hatua kwa njia ya maombi.
Caroline Muthoni ambaye kabla ya mkurupuko wa ugonjwa wa Covid-19 nchini, alikuwa mwalimu katika shule moja ya kibinafsi Nairobi, anasema kwa sasa anajishughulisha kulea mvulana wake.
“Kila kitu kina wakati wake. Mtoto wangu ananihitaji, anahitaji riziki, mavazi, na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi, yakiwemo kupata masomo bora, na ndiyo ninajibidiisha kumkithi,” anafafanua.
Sawa na walimu wengine wa shule za kibinafsi, mama huyo pia anasema janga la corona limemuathiri, kufuatia kufungwa shule zote na taasisi za elimu ya juu nchini mnamo Machi 2020.
Wizara ya Elimu hata hivyo imetangaza kwamba shule zote zitafunguliwa tena Januari 2021. Muthoni kwa sasa anafanya vibarua vya hapa na pale, kujiendeleza kimaisha.