• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
RIZIKI: Zuio kuingia na kutoka nje ya Nairobi liliathiri vibaya biashara yake ya madema

RIZIKI: Zuio kuingia na kutoka nje ya Nairobi liliathiri vibaya biashara yake ya madema

Na SAMMY WAWERU

KARAKANA ya Irungu Kimemia imejaa bidhaa anazounda, na zingine hazijakamilika.

Ni mtengenezaji wa madema, makazi tamba ya muda ya vifaranga kuwazuia dhidi ya kushambuliwa na adui kama vile mwewe, panya, na nyoka.

Vifaa hivyo, pia hutumika kusitiri kuku mchana, ili wasivamie mimea au mazao shambani ambapo wanatiliwa chakula na maji wakiwa mumo humo.

Kabla janga la Covid-19 kupenyeza miguu yake humu nchini Machi 2020, Irungu anaiambia Taifa Leo Dijitali kwamba alikuwa amepokea oda chungu nzima za madema.

Wateja wake wakuu wakiwa wafugaji wa kuku na wanaouza bidhaa za kilimo na vyakula vya kuku, mjasirimali huyo anasema alitakiwa kuunda madema yasiyopungua 20.

“Nilikuwa nimeanza kuyatengeneza na yalipaswa kukamilika chini ya mwezi mmoja. Kwa bahati mbaya, kisa cha kwanza cha virusi vya corona kikathibitishwa nchini na baadaye mipaka kuingia na kutoka nje ya Nairobi ikafungwa,” Irungu anaeleza, akisema sheria na mikakati iliyowekwa iliathiri kwa kiasi kikuu utendakazi.

Kisa cha kwanza cha Covid-19, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona, kilithibitishwa mnamo Machi 13, 2020.

Biashara yake ni ya kuunda madema na kuyapeleka sokoni, kwa wateja wanaoagiza, hivyo basi ni kazi inayohusisha uchukuzi na usafiri wa mara kwa mara.

Irungu anadokeza, wengi wa walioagiza vifaa hivyo walikuwa wamelipa amana (malipo ya kwanza kununua bidhaa au kutengenezewa), na Kenya ilipotangaza kuwa mwenyeji wa Covid-19, kazi yake ilishikwa mateka.

Kitendawili kilichokosa mteguzi kikawa: “Njia ya kuwafikia wateja, wengi wakiwa mashambani, ina vikwazo. Kupata kibali cha kusafiri, ni sawa na kutafuta kivuli cha nzi”.

Vikwazo hivyo (japo viliondolewa Julai 6, 2020) viligeuza karakana yake iliyoko eneo la Githurai 44, Kaunti ya Nairobi, kuwa ghala la madema yaliyokamilika, yanayoendelea kuundwa na pia malighafi.

Irungu Kimemia ni mtengenezaji wa madema ya kuku. Covid-19 imelemaza jitihada zake. Picha/ Sammy Waweru

Akitazama vifaa hivyo, Irungu anaona maelfu ya pesa yaliyokwama. Dema moja hununuliwa kati ya Sh1 500 – 4,000, japo anasema kuna mengine ghali zaidi kulingana na maelekezo ya mteja, kwa mujibu wa saizi au ukubwa.

“Nikikokotoa gharama ya kutengeneza kifaa kimoja, ni kati ya Sh900 – 2, 000,” Irungu anadokeza, akikadiria kiwango cha pesa ‘zilizolala’. Wakati wa mahojiano tulimpata akiwa na takriban madema 70, hii ikiwa na maana kuwa amelaza zaidi ya Sh60, 000 ambazo anasema soko likifunguka tabasamu itarejea.

“Haya ni maelfu ya pesa yaliyokwama hapa. Kwa sasa kibarua nilichonacho, ni kufikia wateja wangu turatibu namna kila mmoja atapata oda yake,” akasema, akihofia gharama ya kuwasafirishia madema huenda ikawa ghali.

Ni gange ambayo ameifanya kwa zaidi ya muda wa miaka minane mfululizo, na anafichua kwamba mwaka wa 2018 mbunge mwakilishi wa Kaunti ya Kiambu Gathoni Wamuchomba alimpiga jeki kwa kununua madema yenye thamani ya Sh100, 000, kupitia warsha ya ‘Kuku Forum’.

“Tangu nihudhurie warsha hiyo nimekuwa nikipokea oda chungu nzima, ila mwaka huu, 2020, janga la corona limelemaza utendakazi wangu,” Irungu anasimulia.

Covid-19, ni janga ambalo limeathiri sekta mbalimbali, ikiwemo biashara na kilimo, na kusababisha wengi kupoteza nafasi za ajira.

Irungu hata hivyo anashauriwa kukumbatia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na WhatsApp kutafutia bidhaa zake soko.

“Kuna makundi mengi ya kilimo katika mitandao ya kijamii, hasa Facebook, ambayo wakulima wanahimizwa kujiunga nayo na kuyatumia kutafuta soko la mazao na bidhaa zao,” anashauri Dennis Njenga, mwasisi na mwanzilishi wa e-FARMERS Africa, kampuni inayotoa mashauri ya kilimo kitaalamu mitandaoni na pia kusaidia waklima kupata soko ndani na nje ya nchi.

Kulingana na mdau huyo, mkulima apige picha za mazao yake shambani na pia bidhaa, azipakie katika makundi hayo, zikiandamana na maelezo ya aliko, bei na nambari za simu.

Wenye biashara pia wanahimizwa kukumbatia matumizi ya mitandao kutafutia mazao yao soko.

“Ni muhimu pia mtumizi awe makini, kwa sababu ya matapeli. Biashara iwe, kusambaza bidhaa na kulipwa papo hapo (cash on delivery),” Dennis anasisitiza.

Huku zuio la kuingia na kutoka nje ya Nairobi na viunga vyake likiwa limeondolewa, Irungu Kimemia ana imani soko la bidhaa zake litaanza kuimarika

  • Tags

You can share this post!

Covid-19 yaathiri huduma katika wizara kadhaa

COVID-19: Visa vipya 421 vyafikisha 11,673 idadi jumla

adminleo