Makala

ROBERT MUGABE: 1924 hadi 2019

September 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA Waziri Mkuu wa kwanza na hatimaye Rais wa taifa huru la Zimbabwe, Robert Mugabe aliaga dunia Alhamisi akiwa na umri wa miaka 95 na kuacha nyuma hisia za umaarufu mseto kimaoni ulimwenguni.

Kwa wengine, bila kuzingatia hisia za ubaguzi wa rangi, mwendazake atabakia katika kumbukumbu za mashujaa wa kutetea haki za ngozi nyeusi, lakini kwa wengine akibakia kuwa nembo ya utawala wa kiimla katika taifa lake.

Ni kwa msingi huo ambapo Uingereza ambayo ni mtawala wa zamani wa Zimbabwe, imesema inaomboleza wale wanaotuma salamu za pole baada ya kutokea kifo cha kiongozi huyo, ikimtaja kuwa mtu dhalimu na dikteta.

Aliongoza baina ya 1980 hadi 2017 alipotimuliwa na jeshi la taifa hilo na Emmerson “Mamba” Mnangagwa akachukua hatamu za urais.

Rais wa kwanza mweusi Zimbabwe alikuwa ni Canaan Sodindo Banana ambaye alikuwa mwanasiasa na Msomi wa Maswala ya Dini na ambaye pamoja na Mugabe na Mnangagwa walipigania uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa serikali ya Mkoloni.

Ripoti zilizotiwa rasmi na familia na serikali Zimbabwe zimesema kuwa Mugabe aliaga dunia Alhamisi akipokezwa matibabu katika taifa la Singapore.

Mwaka wa 2017 aking’atuliwa mamlakani kupitia shinikizo za ajiuzulu alipewa chaguo la kuhamishwa hadi nje ya nchi na akwepe kushtakiwa kwa madai ya udhalimu wa kiutawala lakini akajibu: “Mimi mzalendo kamili kwa Taifa langu naomba nikubaliwe niishi papa hapa Zimbabwe na ikiwa nitaaga dunia, iwe ni katika udongo ulio katika mipaka ya taifa hili langu.”

Mugabe alizaliwa Februari 21, 1924, akiwa mtoto wa baba wa kusaka riziki katika taaluma ya useremala na akasomea katika shule za ufadhili wa Kanisa Katoliki na ambapo taaluma yake ya kwanza ilikuwa ualimu.

Alipata ufadhili wa kielimu katika chuo cha Fort Hare nchini Afrika Kusini na akajipa moja ya kati ya digrii saba alizokuwa nazo hadi akiaga dunia.

Alisomesha katika taifa la Ghana na ambapo alishawishika sana na mitazamo ya Rais wa kwanza wa taifa hilo, Kwame Nkrumah kiasi kwamba, kupalilia mapenzi yake na maono ya Nkrumah, alijipa mke wake wa kwanza kutoka taifa hilo akifahamika kama Sally Mugabe.

Mwaka wa 1960 alirejea Zimbabwe wakati huo taifa hilo likijulikana kama Southern Rhodesia na akaunda vuguvugu la Zimbabwe African National Union (Zanu).

Mwaka wa 1964 alianza ubabe wake wa kisiasa ambapo katika hotuba ya hadhara alimtaja Waziri Mkuu wa kikoloni Ian Smith kama “kiongozi wa serikali ya watundu wa ujana kiwango cha “cowboys”.

Alikamatwa na akatupwa ndani bila kufanyiwa kesi kwa miaka 10 na hata mauti ya mtoto wake wa kwanza hayakushinikiza Wakoloni kumpa hata ruhusa ya kumzika, nje umaarufu wake ukaenea na mwaka wa 1973 akachaguliwa kuwa Rais wa Zanu akiwa korokoroni bado na alipoachiliwa mwaka wa 1974, alihamia katika taifa jirani la Msumbiji na akawa kiongozi wa waasi.

“Afueni yetu ya ukombozi wa taifa letu itatokana tu na utumizi wa bunduki na risasi,” akasema akiwa Mjini London mwaka wa 1976. Umilisi wake wa lugha, ufasaha na ubongo uliokuwa na ujasiri na busara, uliwafanya wanahabari enzi hizo wamtambue kama “muasi wa kipekee ambaye hufikiria”: kwa Kiingereza ikiwa ni “the only thinking man’s guerrilla”.

Nuru gizani

Mwaka wa 1979 kukawa na nuru gizani na uhuru ukapatikana na ambapo uchaguzi uliandaliwa na Mugabe akazoa uungwaji mkono wa kina ingawa kulizuka madai ya wizi wa kura na ulegevu wa kimikakati ya kuweka uwazi katika shughuli hiyo.

Hakuficha uhasimu wake na weupe wa enzi hiyo Zimbabwe kwa kuwa sera zake zilikuwa za kuwafurusha na ndipo kukaanza kuzuka uhasama kati yake na mataifa ya Ulaya.

Alikosana na mshirika wake wa kiutawala Joshua Nkomo, akamfuta kazi na jamii ya Ndebeles ambayo ilionekana kuwa nyuma ya NKkomo ikachinjwa kwa wingi katika eneo la Matabele.

Mugabe alichukua majukumu rasmi ya urais mwaka wa 1987 na akavunja vyama vua upinzani na akaunda chama cha Zanu-PF na mwaka wa 1996 akachaguliwa rais wa awamu ya tatu nakatika afisi kama rais wa kwanza mweusi wa Zimbabwe lakini wa awamu ya tatu, akamuoa Grace Marufu, kufuatia kifo cha yule wa kwanza katika janga la Kansa.

Mwaka wa 1992 ndio Mugabe alizindua sera ya kutwaa mashamba yaliyokuwa mikononi mwa wazungu nay ale yaliyofuata bjora tu yakome kurejelewa kwa kuwa yalikuwa ni uchinjaji wa Wazungu.

Sera hiyo ilikuwa inalenga wazungu 4,500 ambao walikuwa wakimiliki mashamba ya rotuba na hadi mwaka wa 2000, kukiwa kumeunda chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC), kikiongoza na kiongozi wa masuala ya Leba, Morgan Tsvangirai, Mugabe alisema kuwa wazungu hao ndio walikuwa wafuasi wa chama hicho kipya.

Uhasama ukaingia awamu kali kati ya utawala wa Mugabe na jumuia ya Ulaya kiasi kwamba kila aina ya makataa na masharti yaliwekwa dhidi ya utawala wake na uchumi wa Zimbabwe ukaporomoka kana kwamba ulikuwa umevamiwa na matingatinga ya ubomozi.

Katika uchaguzi mkuu wa 2000, chama cha MDC kilijipa 57 kati ya viti 120 vya ubunge lakini uteuzi wa Mugabe wa wengine 20 ukampa uthibiti wa ukiritimba na ukawa ndio mwanza wa utawala wa Mugabe kuingiwa na taharuki ya kung’atuliwa kwa kuwa upinzani uliimarika hadi asilimia 42 katika uchaguzi wa urais wa 2002.

Akisema kuwa ufuasi wa upinzani ulikuwa katika mitaa ya mabanda, Mugabe aliamrisha wachuuzi 30,000 wakamatwe na pia mitaa ya mabanda ibomolewe, hali iliyowaacha watu 700,000 bila makao.

Machi 2008 Mugabe akalipia udhalimu huo kwa kupoteza awamu ya kwanza ya uchaguzi wa urais lakini akatumia kila hila na njama ya kuibuka mshindi katika awamu ya pili ambapo mpinzani wake, Morgan Tsvangirai alisusia. Tsvangirai kwa sasa ni marehemu.

Februari 2009 Mugabe akiwa chini ya shinikizo za utawala uliokuwa umepoteza makali, mashiko na imani akamwapisha Tsvangirai kama waziri wake Mkuu.

Mwaka wa 2013 Mugabe alishinda uchaguzi wa urais kwa asilimia 61 na akawa na mashiko ya kumtema Tsvangirai.

Februari 2016, Mugabe akiwa na umri wa mliaka 94 alitangaza kuwa “nitakuwa Rais wenu hadi Mungu aseme kuja.”

Inaweza kuwa basi ni Mungu aliwatuma wanajeshi wa Zimbabwe National Army ambapo Novemba 15, 2017, alipinduliwa na akashinikizwa kujiuzulu rasmi Novemba 21.

Ni Wazimbabwe ambao wanaweza wakakupa kwa kina uzuri na ubaya wa Mugabe, hukumu ya Mungu ya haki ikiwa nayo ndiyo tegemeo la ufaafu wake kwa utu maishani haya alipokuwa nasi, wote kwa sasa wakiungama kwa kumpungia Mugabe mkono wa buriani kwa kuwa amefariki.