Makala

ROSE NYABATHE: Mwigizaji aliyepata motisha kwa Mercy Johnson

September 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

NI matumaini ya kila msanii kuona anafanya vizuri kisanaa. Kwa mwigizaji yeyote huwa na maazimio ya kuona talanta yake ikiinuka pia kazi zake zikifanikiwa kuchota wafuasi wengi.

Pia hupenda kuwashirikisha mastaa makubwa ili kujifunza mengi kutokana na ujuzi wao. Rose Nyabathe ni miongoni mwa waigizaji wanaotamba hapa nchini wanaoendelea kujituma mithili ya mchwa kwenye jitihada za kuhakikisha wametimiza malengo yao hasa kutinga upeo wa hadhi ya kimataifa miaka ijayo.

Katika mpango mzima anasema amepania kufuata nyayo za wasanii waliovuma katika tasnia ya filamu duniani kama Genevieve Nnaji mzawa Nigeria. Kando na uigizaji dada huyu ni produsa, mwandishi wa script pia anamiliki televisheni ya mitandaoni inayoitwa MoCha TV.

‘Wasanii wa Kenya tunapaswa kufahamu lazima tuwe wabunifu pia tujitahidi tuwezavyo kwenye juhudi za kuzalisha kazi bora ili kupata mpenyo kama ilivyo kwa filamu za kigeni ambazo zimeibukia kuzima matumaini ya wengi wetu,” anasema na kuongeza kuwa itakuwa vyema kwa wasanii wa hapa nchini wajitume bila kulaza damu pia wafanye utafiti zaidi na kila mmoja kuwa na malengo fulani.

Anadokeza kuwa alipata motisha kushiriki uigizaji baada ya kutazama filamu iitwayo ‘Dumebi’ ya mwigizaji mahiri Mercy Johnson ambaye hushiriki filamu za Kinigeria (Nollywood).

Mwigizaji huyu anajivunia kuwa dada wa kwanza katika eneo la Bobasi Kaunti ya Kisii kujiunga na taaluma hiyo pia kuwa mchekeshaji.

Ingawa tangia akiwa mtoto alidhamiria kuwa mtangazaji kwenye runinga ama wakili maisha yalimgeuka ambapo mwaka 2009 alianza kushiriki masuala ya burudani.

”Siwezi kuweka katika kaburi la sahau kwani nakumbuka vizuri muda huo nilishiriki kipindi cha Churchill Top Comic Talent Search kilichokuwa kikipeperushwa kupitia runinga ya NTV.”

Dada huyu anajivunia kushiriki vipindi kadhaa ikiwamo ‘Hapa kule,’ (KTN), ‘Classmate,’ na ‘Je huu ni ungwana,’ zote (KBC), ‘Mke sumu,’ na ‘Afrika Mobimba’ (Capuchin TV), ‘Heart Strings Kenya’ (Stage Show) bila kusahau ‘Masoja’ (MoCha TV).

Kipusa huyu aliyekuwa akijulikana kama Village Girl kwenye kipindi cha Classmate anasema kuwa pia anataka sana kukuza talanta za waigizaji wanaokuja. Dada huyu anatoa mwito kwa serikali ikome kuzitoza ushuru wa juu kampuni za kigeni zinapohitaji kufanyia kazi ya uigizaji humu nchini.

”Hatua hiyo huchangia wasichana na wavulana wengi yaani waigizaji kukosa ajira pia hufanya kampuni nyingi kupigia chini mipango ya kufanyia kazi zao hapa Kenya,” akasema na kuongeza kwamba pia serikali inastahili kutenga fedha za kuinua tasnia ya maigizo hasa kule mashinani ambako wasanii chipukizi wamefurika kila kona.

Anasema hapa nchini angependa kufanya kazi na Consolata Bahati Kamau maarufu Afande Zena ambaye pia ameshiriki filamu ya Mke Sumu na Vioja Mahakamani.

Kwa waigizaji wa kimataifa anatamani sana kufanya kazi nao Anne Kansiime mzawa wa Uganda na Mercy Johnson wa Nigeria. Anawataka wenzie hapa nchini waache kubaguana mbali waige mtindo wa wenzao katika mataifa yanayofanya vyema kama Nigeria na Afrika Kusini ambapo kila msanii husapoti mwenzie.

Demu huyu anasema kuwa anachukulia uigizaji kama ajira kwa kuzingatia ndiyo taaluma inayomsaidia kujikimu kimaisha kwa kila kitu.