Ruth Chepengetich apigwa mafuruku kukimbia kwa kutumia dawa za kusisimua misuli
MWANARIADHA wa mbio za kilomita 42 ya wanawake, Ruth Chepng’etich, amepigwa marufuku miaka mitatu na Kitengo cha Maadili cha Shirkisho la Riadha Duniani (AIU) mnamo Alhamisi, Oktoba 23, 2025.
Hiyo ni baada ya kukubali makosa ya kukiuka Sheria za Kukabiliana na Matumizi ya Pufya (ADRVs) kufuatia kupatikana na kutumia dawa iliyopigwa marufuku aina ya Hydrochlorothiazide (HCTZ).
Chepngetich, 31, ambaye ni bingwa wa dunia wa marathon mwaka 2019 na mshindi mara tatu wa Chicago Marathon, alikubali mashtaka na adhabu hiyo baada ya sampuli yake ya mkojo iliyochukuliwa Machi 14 mwaka huu kuonyesha matumizi ya dawa hiyo iliyopigwa marufuku, na kufuatiwa na uchunguzi wa AIU kuhusu tukio hilo.
Ingawa dawa zinazochochea utolewaji wa mkojo (diuretics) zinajulikana kutumiwa vibaya na wanariadha ili kuficha uwepo wa dawa nyingine za kusisimua misuli katika mkojo, HCTZ pia imewahi kugunduliwa kama kichafuzi kinachoweza kuwepo katika baadhi ya dawa halali.
Shirika la Dunia la Kupambana na Matumizi ya Pufya (WADA) limeweka kiwango cha chini cha kuripoti cha 20ng/ml, ambapo matokeo chini ya kiwango hicho hayapaswi kuripotiwa kama kosa. Hata hivyo, sampuli ya Chepng’etich ilionyesha kiwango cha takriban 3,800ng/mL cha HCTZ.
Alipofanyiwa mahojiano ya awali na AIU hapo Aprili 16, 2025, Chepng’etich hakuweza kutoa maelezo ya kueleweka kuhusu matokeo yake. Ili kuondoa uwezekano wa kuchafuliwa kwa bahati mbaya, AIU ilikusanya ushahidi, ikiwemo orodha ya kina ya virutubisho na dawa zote alizotumia kabla ya kupimwa, na pia ilikusanya dawa na virutubisho vyote vilivyokuwa kwake kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Simu yake pia ilinakiliwa kwa ajili ya uchunguzi.
Katika mahojiano ya pili mnamo Julai 11, 2025, Chepng’etich alielezwa kuwa kulikuwa na ushahidi kutoka kwenye simu yake uliotoa mashaka ya msingi kwamba matumizi ya HCTZ huenda yalikuwa ya makusudi.
Isitoshe, Chepngetich alijulishwa kuwa dawa na virutubisho vyote alivyokabidhi kwa uchunguzi viliripotiwa na maabara ya WADA kuwa havikuwa na HCTZ. Chepng’etich aliendelea kushikilia msimamo wake kwamba hakuweza kueleza matokeo hayo na kwamba hajawahi kutumia dawa za kusisimua misuli.
Hata hivyo, Julai 31, 2025, alibadilisha kauli yake. Aliandika kwa AIU akisema amekumbuka kuwa alipata maradhi siku mbili kabla ya kupimwa, na akatumia dawa ya yaya wake bila kuthibitisha kama ilikuwa na dawa iliyopigwa marufuku. Alisema alisahau kutaja jambo hilo wakati wa uchunguzi wa awali. Aliwasilisha pia picha ya pakiti ya dawa ambayo ilionyesha wazi kuwa ni Hydrochlorothiazide.
Ingawa AIU iliona maelezo hayo mapya hayakuwa ya kuaminika, kwa mujibu wa sheria za kupambana na pufya, hayakusaidia kupunguza adhabu ya kawaida ya miaka miwili kwa matumizi ya dawa maalum kama HCTZ.
Kinyume chake, sheria zinasema kitendo cha uzembe kama alichokieleza, kutumia dawa bila uhakiki, kinaangukia katika “nia isiyo ya moja kwa moja”, ambayo inastahili adhabu ya miaka minne. Hivyo, Agosti 22, 2025, AIU ilimuarifu kuhusu mashtaka, ikipendekeza adhabu ya miaka minne.
Chepng’etich alikiri makosa hayo, na kwa kuwa alikubali adhabu ndani ya siku 20, Septemba 10, 2025, alipunguziwa mwaka mmoja chini ya kifungu cha ADR 10.8.1 kinachohusu kukubali mapema.
“Kesi kuhusu matokeo chanya ya HCTZ imehitimishwa, lakini AIU itaendelea kuchunguza taarifa za kutia shaka zilizopatikana kwenye simu ya Chepng’etich ili kubaini kama kulikuwa na makosa mengine. Kwa sasa, rekodi na mafanikio yake yote yaliyopatikana kabla ya Machi 14, 2025 yanasalia kuwa halali,” akasema Mkuu wa AIU, Brett Clothier.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa AIU, David Howman, alisema kesi hiyo inaonyesha kuwa “hakuna aliye juu ya sheria” na akasifu juhudi za kudumisha uadilifu kwenye michezo.
“Ingawa ni jambo la kusikitisha kwa wale waliomwamini mwanariadha huyu, mfumo umefanya kazi kama inavyotakiwa. Tasnia ya mbio za barabarani inastahili pongezi kwa kufadhili juhudi za kupambana na pufya ambazo zimewezesha kufichua makosa haya. Kiwango cha uchunguzi katika kesi hii kiliwezekana kutokana na ufadhili kutoka mradi wa Shirikisho la Riadha Duniani wa mbio za barabarani, marathon kama Chicago, mawakala, wanariadha na wadhamini wanne wa viatu – adidas, ASICS, On na Nike.”