Makala

Ruto: Kalonzo alinikataa nikamwendea Raila

Na PIUS MAUNDU May 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto amefichua kuwa alijaribu kushirikiana na Kalonzo Musyoka baada ya uchaguzi wa 2022 kabla ya kumgeukia kiongozi wa ODM Raila Odinga, lakini Bw Kalonzo alikataa.

Katika mkutano wa faragha na viongozi wa Ukambani uliofanyika Ikulu siku ya Jumatano, Rais Ruto alimshambulia kisiasa aliyekuwa Naibu Rais wake Rigathi Gachagua, pamoja na Bw Musyoka, huku akijitetea kwa kushirikiana  na Bw Odinga.

“Nilimtafuta Kalonzo kwanza” Rais Ruto alisema

“Baada ya uchaguzi wa 2022, nilimwendea Bw Musyoka kabla ya Bw Odinga. Lakini alinijibu kwa kusema ‘vomwe vetwe’ (silegezi kamba kamwe) – usemi wa ukakamavu wa kisiasa ambao Bw Kalonzo amekuwa akitumia mara kwa mara.”

Hii ni mara ya pili kwa Rais Ruto kufichua jaribio lake la kushirikiana na Bw Kalonzo, akisema bado yuko tayari kushirikiana na viongozi wa ngazi za mashinani kutoka Ukambani hata kama Kalonzo hataungana naye.

Rais Ruto pia alimkejeli vikali Bw Gachagua, aliyefutwa kazi kupitia mchakato wa bunge mwaka jana.

“Mtu ambaye alishindwa hata kuwapata maseneta 14 wa kumuokoa dhidi ya kufutwa kazi hawezi kusema anaweza kuwaongoza mamilioni ya Wakenya. Alipoteza nafasi kubwa niliyompa. Amejaa chuki na kisasi.”

Kwa kauli hizo, Rais alionyesha kujitenga kabisa na Gachagua, ambaye sasa anaonekana kuungana na Kalonzo katika upinzani.

Ruto alitaja wapinzani wake kama watu wa kauli tupu wasio na ajenda ya maendeleo:

“Ajenda yao ni ‘Ruto Must Go’, ‘One Term’ na ‘Kasongo’ – maneno tu bila mpango wowote wa kilimo, afya, au makazi ya bei nafuu.”

Mkutano huo wa Ikulu uliwaleta pamoja viongozi wa ngazi za chini na wataalamu kutoka Ukambani, wakati ambao Rais anajipanga kuvamia ngome ya kisiasa ya Kalonzo Musyoka iliyo na zaidi ya kura milioni mbili kutoka Machakos, Kitui na Makueni.

Mkutano huo uliandaliwa siku moja baada ya Bw Musyoka kujitangaza kuwa mgombea wa urais wa upinzani mwaka 2027 na kumshutumu vikali Rais Ruto kwa kile alichokiita utawala mbaya.

“Ukombozi wa nchi hii utatoka mashariki,” Bw Musyoka alisema akimaanisha ngome yake ya Ukambani wakati wa mazishi ya mjomba wake David Mburu Mairu katika kijiji cha Kathungu Kaunti ya Kitui.

“Sasa si siri tena kuwa William Ruto atamenyana na Kalonzo Musyoka kwenye uchaguzi na ataenda nyumbani,” aliongeza siku hiyo hiyo alipojiunga na Seneta wa Kitui Kiio Wambua na Spika wa Bunge la Kaunti ya Makueni Douglas Mbilu kuwashauri wafuasi wake kutohudhuria mkutano wa Ikulu uliopangwa.

Maspika wa mabunge ya Kitui na Machakos, Kinengo Katisya na Anne Kiusya, waliwaongoza baadhi ya washirika wa Bw Musyoka kumkaidi.

Naibu Gavana wa Machakos Francis Mwangangi alipuuza mkutano wa Ikulu akisema ni kupoteza muda.

Aliwataja washirika wa Rais Ruto Ukambani kama mabroka wa kisiasa huku akishangaa kwa nini serikali haijatekeleza ahadi zake kwa eneo hilo.

“Kabla ya uchaguzi wa 2022, Kenya Kwanza walizunguka nchi nzima wakikusanya maoni kuhusu maendeleo ya kila eneo. Ni nini kinawazuia kutekeleza miradi hiyo sasa ambapo wako mamlakani? Hauhitaji watu kwenda kupiga magoti ili eneo lao lipate maendeleo wanayostahili kutoka kwa serikali ya kitaifa,” alisema jana.

Miongoni mwa mikakati ya Rais Ruto ya kujihakikishia sehemu ya kura takribani 2 milioni kutoka Ukambani ni ziara ya kukutana na wananchi pamoja na kutumia watu wenye ushawishi wakiwemo viongozi wa kidini.

“Mara tu baada ya kusherehekea Madaraka katika Kaunti ya Homabay, kituo kinachofuata ni Ukambani,” alisema katika mkutano na viongozi wa Ukambani uliowaleta pamoja takriban wajumbe 1,500.

Kiongozi wa Taifa anatarajiwa kuzindua miradi ya miundombinu ya thamani ya mabilioni ya pesa katika ziara yake ya kwanza ya maendeleo Ukambani.

Alitumia mkutano wa Ikulu kueleza mafanikio ya serikali ya Kenya Kwanza.

Alisema kuwa ameimarisha uchumi wa nchi kupitia maamuzi magumu kama kuondoa ruzuku kwenye bidhaa za msingi kama unga wa mahindi na mafuta, pamoja na kuongeza ushuru huku akitabiri mustakabali mzuri wa taifa.

“Hatuwezi kuiacha jamii ya Wakamba nyuma wakati tunapobadilisha nchi hii. Hakuna fahari kuwa katika upinzani,” Rais Ruto alisema katika hafla hiyo ambayo wito kwa jamii ya Wakamba kujiondoa upinzani ilitawala.

Waziri wa Kazi na Ulinzi wa Jamii Alfred Mutua, Mbunge wa Kangundo Fabian Kyule, Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, Mbunge wa Kitui Kusini Rachael Kaki, Mbunge wa Machakos mjini Caleb Mule na Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka pamoja na maseneta walioteuliwa Beth Syengo (ODM) na Tabitha Mutinda (UDA) walimshutumu Bw Musyoka kwa kuipotosha jamii ya Wakamba.

Kiongozi wa Kanisa la African Brotherhood Askofu Mkuu Timothy Ndambuki, mwenyekiti wa baraza la makanisa tawi la Ukambani Leonard Kasyoka na kiongozi wa Kanisa Katoliki Kaunti ya Machakos Askofu Norman King’oo waliwaongoza viongozi wa kidini kuonyesha uaminifu wao kwa Rais Ruto.