Ruto: Mpango wa ‘Bottom Up’ utazaa matunda, ni mimi ninawaambia
RAIS William Ruto ameshikilia kuwa mpango wa serikali kuimarisha uchumi unazaa matunda.
Dkt Ruto amekashifu wanaompinga akidai wana nia ya kuona nchi inarudi nyuma ili wanufaike kisiasa ndiposa hawayaoni matunda hayo.
“Ni lazima tukomeshe roho mbaya katika nchi yetu. Hatuwezi kuruhusu uongo na propaganda kuliharibia taifa jina,” akasema Rais akiwa Kaunti ya Taita Taveta Jumapili.
“Nchii hii haiwezi kufeli. Ninawaonea huruma wapinzani wenye roho mbaya wanaopenda kuona nchi imeanguka. Ninawasihi Wakenya kukataa fitina na uongo kutoka kwa wasiopenda kuona nchi inasonga mbele,” akaongeza Rais akiahidi kuleta mageuzi.
Kiongozi wa nchi alisema haya alipohudhuria ibada katika kanisa la Soul Harvest Church akiandamana na Mwakilishi wa Kike wa Taita Taveta Lydia Haika, Mbunge wa Taveta John Bwire na Mwenyekiti wa Shirika la Hazina ya Kilimo (AFC) John Mruttu.
Rais alidokeza kuwa alihudhuria ibada eneo la Taveta baada ya kuzuru shamba lake eneo hilo.
“Nilifaa kuhudhuria ibada kwingine lakini nilimtuma mwakilishi. Nilikuwa na fursa ya kuja katika shamba langu na tukaamua kushiriki ibada hapa,” akasema. Dkt Ruto aliahidi kukarabati barabara ya Taveta – Illasit iliyo katika hali mbaya.
Aliangazia malalamishi ya viongozi wa mtaa kufuatia kufutiliwa mbali kwa mkataba wa serikali na mashirika binafsi (PPP) wa Sh8 bilioni kujenga barabara ya Taveta – Kajiado sababu za gharama ya juu.
“Kuna wenye mashaka kuhusu kujengwa kwa barabara hii. Nilipozuru eneo hili wiki mbili zilizopita, niliwahakikishia kuwa barabara itatengenezwa. Wenye mashaka wanafaa kungoja hadi Januari ili waone ujenzi ukianza,” akasema Rais.
Mnamo Ijumaa, Rais Ruto alishikilia kuwa nchi imekuwa imara kiuchumi, kuna mfumko wa bei ya bidhaa na shilingi ya Kenya imekuwa thabiti. Alisema haya alipokuwa Mombasa katika maadhimisho ya 60 ya Idara ya Wanajeshi wa Majini.
Kwa upande wake Bw Mruttu alitilia mkazo juhudi za serikali za kuimarisha nchi kiuchumi akiwataka Wakenya kuwa na subira huku Rais akiwa kazini.
“Mipango ya serikali ya nyumba za bei nafuu, Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) na mfumo wa ufadhili wa elimu ya chuo, itabadilisha pakubwa maisha ya Wakenya,” akasema.
Bi Haika aliwahimiza wakazi kujisajili katika Bima mpya ya afya ya Kijamii (SHIF) na kuangazia malalamishi kuhusu mpango wa Linda Mama na EduAfya.
“Watu wana wasiwasi kuwa mipango ya Linda Mama na EduAfya imeondolewa. Lakini ninawahakikishia kuwa imeboreshwa katika bima mpya,” akasema.
Bw Bwire, mbunge aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Wiper, anaendelea kuunga mkono ajenda za Rais Ruto. Hii ni kinyume na Kiongozi wake Wiper Kalonzo Musyoka ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan