Makala

Sababu iliyonifanya nirushe chini bunduki na kuchukua Biblia

April 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA OSCAR KAKAI

ILIKUWA bahati alivyoponyoka kifo mara nyingi akiwa katika uhalifu.

Anapokumbuka maisha yake ya zamani, Pasta Daniel Kaporion anahisi kuwa angeumia ama kuuawa kama wandani wake wa ujangili kupitia kupigwa risasi.

Pasta huyo anasema kuwa alijiunga kwenye ujangili akiwa na umri wa miaka 17.

Akielezea hali yake ya zamani, Pasta Kaporion alikuwa akiishi kwenye msitu akiwa uchi wa mnyama sababu hakuwa na ufahamu kuhusu nguo.

Kaporion, ambaye sasa ni mwinjilisti shupavu, anasema kuwa alikuwa akiua watu wengi kwenye mashambulio kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Turkana.

“Mara ya kwanza nilipovaalia long’i, nilihisi mwili wangu ukiuma. Nilibaki sina amani na sikuwa na nia ya kuvalia nguo tena,” anaeleza Pasta Kaporion.

Pasta huyo mwenye umri wa miaka 40 alibadilika na kupata wokovu mwaka wa 2006.

“Niliona majangili wenzangu, marafiki na watu wa ukoo wakiuawa. Pasta Musa Lomuria alinisaidia kuacha maovu hayo. Alinisaidia na kunichochea kuacha uhuni,”anasema.

Taifa Leo ilipatana na Pasta huyo akihubiri neno la Mungu kwenye kanisa jipya lililojengwa kwa udongo na mabati eneo la Kotulupogh kwenye wadi ya Masol, kaunti ndogo ya Pokot Magharibi.

“Mara nyingi, bunduki ilikuwa ikikaa kando yangu. Nilikuwa jangili mbaya lakini nashukuru Mungu kwa kuniokoa,” anasema Pasta Kaporion.

Akiwa amebeba Biblia mkononi, mhubiri  huyo alielezea jinsi aliepuka kifo chupuchupu.

“Nilikuwa ninaishi kama mnyama kwenye msitu lakini Mungu alinikujia,” mhuburi huyo aliambia waumini katika kanisa la Agape.

Pasta Kaporion ambaye anatoka katika kijiji cha  Nasolot, eneo la Turkwel alijenga kanisa mwaka wa 2019 eneo la Kotulupoh baada ya kutumwa na Askofu wa kanisa la Agape eneo hilo Peter Siwa.

“Askofu aliniagiza kwenye eneo ambalo hakuna kanisa na watu wanamjua Mungu. Alininunulia nguo zangu za kwanza,” anasema.

Anaeleza kuwa alijenga kanisa hilo baada ya kuuza baadhi ya mifugo wake na kupata usaidizi kutoka kwa viongozi wengine wa kidini.

“Niliamua kutumia mali yangu kidogo sababu nilihisi kuwa watu wangu wanamhitaji Mungu,” anasema.

Anasema kuwa mara ya kwanza walianza kuabudia chini ya mti.

“Tuliabudia chini ya mti kabla ya kuanza ujenzi,” anasema.

Eneo la Kotulupogh lilikuwa uwanja wa vita kati ya jamii hasimu za Pokot na Turkana ambao huzozania mifugo.

Zaidi ya miaka 50, eneo la Kotulupogh lilikuwa halikalki na watu kutoka jamii za Turkana na Pokot zilikuwa zikiibiana mifugo.

Eneo hilo pia hushuhudia visa vya ukeketaji kwa asilimia 100 na kiwango cha juu cha ujinga.

Lakini leo, kanisa linasimama kwenye ardhi hiyo ya mapigano na milio ya risasi imenyamaza. Wakazi wamebadilisha silaha haramu na Bibilia huku waliokuwa wahalifu wakimuabudu Mungu kuokoa roho zao.

 

[email protected]