Sababu za kuamua kuchomwa badala ya kuzikwa mwigizaji Ouda akiwa wa hivi punde
NA WANDERI KAMAU
HABARI kwamba mwigizaji Charles ‘Charlie’ Ouda atachomwa katika makaburi ya Kariokor, jijini Nairobi, Alhamisi, zimeibua kumbukumbu za watu wengine maarufu nchini walioamua kuchomwa badala ya kuzikwa.
Kwenye taarifa Jumapili, familia hiyo ilisema ulikuwa uamuzi wa mwgizaji huyo maarufu kuchomwa.
Taarifa hizo ziliwashangaza mashabiki wengi wake, baadhi wakisema kwamba walitarajia wangepata nafasi ya kumuaga marehemu, kwa mfano kwa kuutazama mwili wake.
Wakenya wengine maarufu walioamua kuchomwa ni aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom, Bw Bob Collymore, aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Jeremiah Kiere-ini, Bi Jane Kiano, mwanasiasa Kenneth Matiba, mwanamazingira Wangari Mathai, Bw John Macharia (mwanawe mmiliki wa kampuni ya Royal Media Services, SK Macharia), Mwanasheria Mkuu wa zamani Charles Njonjo, Askofu Manasses Kuria na mkewe Mary Kuria kati ya wengine.
Kulingana na familia ya Bw Collymore, yeye binafsi ndiye aliyeamua kuchomwa baada ya kufariki mnamo 2019.
Mkewe Bw Collymore, Bi Wambui, alisema kuwa mumewe alikuwa mtu mnyenyekevu kwenye uhai na hata baada yake kufariki.
“Alikuwa mtu wa kipekee. Msimamo na mtazamo wake maishani ndizo zilimfanya kuamua kuchomwa. Hakutaka mbwembwe katika mambo yake,”akasema.
Kwa Bw Kiere-ini, familia yake pia ilisema ndiye aliyefanya uamuzi wa kuchomwa.
Ijapokuwa haikutoa maelezo mengi baada ya kifo chake mnamo 2019, ilibainika baadaye kuwa bwanyenye huyo alikuwa ashatangaza akiwa hai kwamba hayo ndiyo yalikuwa matamanio yake.
Profesa Wangari Mathai pia aliwashangaza wengi, ilipobainika kwamba alikuwa ameamua kuchomwa.
Kulingana na familia yake, Prof Mathai, ambaye pia alikuwa mshindi wa Tuzo ya Nobeli, hakutaka kuharibu mazingira.
“Kimsingi, jeneza lake lingetengeneza kwa mbao. Hilo lilimaanisha kuwa kuna mti au miti kadhaa ingekatwa ili kumtengenezea jeneza hilo. Hakutaka kuona uharibifu wa mazingira akiwa hai na hata baada ya kuondoka duniani,” likaeleza shirika la Greenbelt Movement, alilolianzisha.
Mwili wa Prof Mathai uliwekwa kwenye jeneza lililotengenezwa kwa mafunjo kabla ya kuchomwa.
Watu wengi walimsifu kwa kuonyesha hali ya kujali mazingira hata baada ya kufariki mnamo 2011.
Kwa mwanasiasa Matiba, familia yake ilisema ulikuwa uamuzi wake tangu mwanzoni kuchomwa.
Hata hivyo, familia ya Askofu Kuria na mkewe, Mary, ilisema uamuzi wao ulitokana na imani yao kwamba mwili wa mwanadamu utarejea kwenye mchanga baada yake kufariki.
Askofu Kuria alikuwa miongoni mwa viongozi maarufu sana wa Kanisa la Kianglikana (ACK) nchini.
Hata hivyo, uamuzi wake ulizua migawanyiko miongoni mwa Wakristo, baadhi wakisema kwamba uchomaji miili haulingani na mafundisho ya Biblia.
Uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali umebaini kuwa watu wengi hufanya maamuzi yao wenyewe kuchomwa, huku wengine wakilenga kuziepushia familia zao gharama kubwa za kuandaa mazishi.