Sababu za wajane kukosa kurithi mali ya waume wao
IMEBAINIKA kuwa kutosajiliwa kisheria kwa ndoa na ukosefu wa wosia ni sababu kuu zinazochangia wajane kukosa kurithi mali ya waume zao.
Wanawake wanaohudhuria vikao vya kutoa uhamasisho kuhusu haki yao ya kurithi mali ya waume zao wanapofariki huambiwa kuwa ndoa halali huwa ni zile zilizosajiliwa.
“Ili mtu aitwe mjane, ina maana kuwa alikuwa mke. Ili mtu aitwe mke ina maana kuwa ndoa yake ilikuwa rasmi,” anaeleza Afisa Mkuu Mtendaji wa muungano wa kutatua masuala ya Ardhi, Land Alliance Faith Alubbe.
Kulingana na Sheria ya Ndoa ya 2014, ndoa ni kuja pamoja kwa mume na mke kwa njia inayotambuliwa kisheria. Kuna ndoa ya kisasa, ndoa ya kikristo, ndoa za kitamaduni, ndoa za Kihindu na ndoa za Kiislamu.
Chini ya Sheria ya Mali ya Wanandoa ya 2023, mali hiyo hujumuisha makazi, vitu vyote vilivyoko ndani ya nyumba, mali inayomilikiwa kwa pamoja na mke na mume na mali waliyopata wakiwa katika ndoa.
Sheria hiyo inatambua mali ya ndoa kama ile inayomilikiwa na mume na mke na boma lao la kifamilia.
“Mke huwa na haki ya kumiliki mali ya ndoa baada ya mumewe kufariki. Hii hufanyika kupitia mchakato rasmi wa urithi,” anaongeza Bi Alubbe.
“Mchakato huo hufanywa haraka ikiwa hamna mvutano.”
“Kile mwanamke anahitaji kufanya ni kufika katika afisi ya chifu ili apewe barua rasmi inayothibitisha kuwa marehemu mumewe alikuwa akiishi katika eneo hilo na kwamba chifu huyo aliwafahamu kama wanandoa,” Bi Alubbe.
Afisa huyo mtendaji wa Land Alliance anaongeza kuwa mjane kama huyo pia anahitaji stakabadhi kama vile cheti cha kifo na leseni ya mazishi ambazo zitawasilishwa kortini ili atambuliwe kuwa msimamizi wa pekee wa mali hiyo.
Bi Alubbe anasema utaratibu huo huwa ni ngumu zaidi mjane alikuwa katika ndoa isiyosajiliwa kisheria.
“Katika mahusiano ya kuja-tuishi, huwa hamna stakabadhi ya kuonyesha kuwa walikuwa mume na mke. Mwenzake anapofariki, mwanamke huyo atalazimika kwenda kortini ili apate stakabadhi ya kuonyesha alichukuliwa kama mkewe marehemu,” Bi Alubbe anaeleza.
“Baada ya hapo anaweza kuendelea na mchakato wa kurithi mali kulingana na sheria ya urithi,” anaongeza.