Makala

Sababu za Wakenya kubuni jina ‘Kasongo’ ambalo Ruto alidensi wimbo wake katika sherehe

Na FRIDAH OKACHI January 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA mtandaoni huwa wabunifu kwa kuwapa watu maarufu majina kulingana na tabia zao ili kuelezea hisia zao.

Oktoba 2024, baada ya kuvunjika kwa ndoa ya kisiasa kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa Naibu wake Rigathi Gachagua, Wakenya walibuni jina Kasongo na kuanza kusambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Jina hilo lilipata maarufu mno mapema Novemba 2024, kwa kuonyesha jinsi wawili hao walitengana na kumlaumu Rais kuwa mwepesi wa kusahau haraka licha ya kusaidiwa na Bw Gachagua kupata urais.

Mara kwa mara huwa ucheshi usiozuiliwa mitandaoni wakiendelea kuunda jina hilo lenye utani, ambalo lilipata mvuto kwa kuelezea kero zao na kukosoa serikali kutokana na utekaji nyara na ufisadi.

Katika mtandao wa TikTok, Stacy Akoto anacheza wimbo huo, ukionyesha jinsi utawala wa sasa umeshindwa kukabiliana na ufisadi, gharama ya juu ya maisha, na utekaji wa nyara. Wimbo huo unaonyesha jinsi mwanamke (Wakenya) anamuomba mumewe kurejea nyumbani na kutekeleza majukumu yake vilivyo.

Januari 1, 2025 Rais William Ruto alionekana kukubali jina hilo la utani na lenye utata. Hii ni baada kudensi wimbo huo wakati wa kuvuka mwaka katika Ikulu ya Rais, Kaunti ya Kisii.

Wimbo Kasongo ulitungwa na Kundi la Super Mazembe mwaka 1977 ambao walipata makao yao nchini Kenya 1975 baada ya kusafiri kutoka Zambia na kupitia Tanzania.

Kundi hilo la Super Mazembe, walimtembelea Kasongo wa Kanema mtaani Eastleigh na kumpata hayuko.

Mkewe wa Kasongo wa Kanema aliwafahamisha kuwa mumewe huwa hapatikani nyumbani. Hivyo, Super Mazembe kutunga wimbo huo wakimtaka Kasongo arudi nyumbani na kutekeleza majukumu yake.

Katika wimbo huo, mkewe analalamika na kulia. Anamweleza kuwa bado anamsubiri na kusalia barabarani kuona atatokea wapi.

Novemba 2022, Wakenya hao hao, pia walimpa jina lingine ambalo ni Zakayo.

Walilinganisha mienendo yake na ile ya Zakayo kwenye Biblia, anayejulikana kama mtoza ushuru mwenye tamaa ambaye alipanda mti ili kumwona Yesu.

Walimtaja Rais mara kwa mara kuhusiana na sera za kodi alizoweka.

Tangu alipochaguliwa rais mnamo Agosti 2022, Bw Ruto aliazisha msururu wa kodi mpya na kuongeza zile za zamani. Hatua hiyo, ilimfanya asipendwe na Wakenya wengi wanaoamini kuwa alikiuka ahadi yake ya kampeni ya kutetea masilahi ya “hustlers” wale wanaopambana na hali ngumu ya kiuchumi.

Katika hotuba yake ya Desemba 12, 2022, Bw Ruto alikubali kwamba kodi hizo ni ghali na chungu. Kwa upande wake, alisema kodi za juu ni muhimu na zitawezesha serikali kupunguza kukopa na kupunguza deni la taifa, ambalo kwa wakati huo lilifikuwa Sh10 trilioni.

“Tumechukua maamuzi sahihi, mara nyingine tukifanya maamuzi magumu na yenye uchungu, ili kuirejesha Kenya kutoka ukingo wa hatari ya deni,” alisema.

Baadaye Rais Ruto alionekana kutokuwa na tatatizo kwa kufafananishwa na Zakayo wa Biblia.

“Tayari nimeitwa Zakayo katika baadhi ya maeneo, labda tutakuwa na siku ya mtoza ushuru,” alisema kwa utani mwezi Mei, 2023.

Hata hivyo, Wakenya wengi hawakubaliani naye.

Uchungu wa kodi ulijikita katika mazungumzo ya kila siku, hasa kwa kuzingatia gharama ya juu ya maisha.

Hadi pale vijana wa Gen Z walipofanya maandamano ya kupinga mswada wa Fedha 2024.