Makala

Sababu za Wakenya kupuuza kuchangia hoja ya kumfurusha Gachagua siku ya pili

Na WAANDISHI WETU October 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

SHUGHULI za ushirikishaji wa maoni ya umma katika hoja ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua ziliingia siku yake ya pili Jumamosi huku watu wachache wakijitokeza ikilinganishwa na Ijumaa.

Katika kaunti ya Nyeri, alikozaliwa Bw Gachagua, ni watu wachache waliojitokeza kutoa maoni katika ngazi za maeneo huku polisi wakiimarisha usalama.

Katika eneo bunge la Othaya, polisi wa kupambana na fujo walizingira afisi ya Mbunge Wambugu Wainaina ambako shughuli hiyo ilikuwa ikiendelea.

Kulingana na maafisa wa serikali watu wachache walijitokeza Jumamosi kwa sababu wengi walishiriki zoezi hilo siku ya kwanza.

“Watu wachache wamejitokeza leo (Jumamosi kwa sababu wengi walishiriki zoezi hilo jana (Ijumaa),” akasema afisa huyo.

Idadi ndogo ya watu pia ilishuhudiwa katika maeneo bunge ya Mathira, Mukurweini, Tetu na Kieni.

Hali kama hiyo pia ilishuhudiwa katika sehemu kadhaa nchini.

Shughuli ya Jumamosi, iliendeshwa kutokana na amri ya Mahakama Kuu kwamba Bunge la Kitaifa lihakikishe kuwa raia katika ngazi za maeneo bunge pia wanapewa nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu hoja hiyo iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.

Katika eneo bunge la Laikipia Mashariki idadi ya watu waliojitokeza ilikuwa ndogo zaidi ikilinganishwa na siku iliyotangulia.

Isitoshe, maafisa wa bunge la kitaifa ambao walitarajiwa kusimamia shughuli hiyo ya ushirikishaji wa maoni yao umma hawakujitokeza.

Polisi ndio walikuwa wakishika doria katika afisi hiyo ya hazina ya ustawi wa eneo bunge hilo (NG-CDF).

Ajabu ni kwamba shughuli hiyo pia haikuendelea katika afisa za NG-CDF katika eneo bunge la Kibwezi Magharibi linalowakilishwa Bw Mutuse ambaye ndiye mdhamini wa hoja hiyo.

Aidha, idadi ndogo zaidi ya wakazi wa kaunti ya Trans Nzoia walijitokeza kutoa maoni yao kwa hoja hiyo iliyowasilishwa rasmi katika Bunge la Kitaifa Jumanne, Oktoba 1.

Uchunguzi  wetu katika afisi za eneo bunge la Saboti na ile ya Mbunge Mwakilishi wa Kaunti hiyo ulibaini kuwa kulikuwa na shughuli chache kwani wakazi wetu waliisusia shughuli hiyo.

Wale tuliozungumza nao walisema hawakuwa na wakati wa kusafiri hadi afisi za eneo bunge hilo wakisema kuwa wangeletewa fomu hizo manyumbani mwao au kazini.

“Sina wakati wala pesa za kutumia kama nauli kusafiri hadi afisi za eneo bunge langu la Kiminini ilhali ninafahamu kwa suala hili tayari limeamuliwa,” akasema Bi Agnes Nyongeza, mkazi wa eneo bunge la Kiminini.

Hali sawa na hiyo ilishuhudiwa katika maeneo bunge ya Kapenguria, Sigor na Kacheliba na Pokot Kusini katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Idadi ndogo ya watu walijitokeza kutoa maoni yao katika afisi za hazina za maendeleo katika maeneo bunge hayo.

Hata hivyo, hali ya watu kukanganyikiwa na makabiliano yaliathiri shughuli ya ushirikishaji wa maoni ya umma katika eneo bunge la Turbo, kaunti ya Uasin Gishu, anakotoka Rais William Ruto.

Baadhi ya wakazi walilalamika kuwa hawakupewa nafasi ya kutoa maoni yao kinzani kuhusu mchakato huo wa kumtimua Bw Gachagua.

Na katika eneo la magharibi mwa Kenya, wakazi hawakuwa na msisimko wa kushiriki katika zoezi hilo.

Katika maeneo bunge ya kaunti ya Kisumu wakazi waliachwa gizani kwani hawakufahamu ni wapi walipaswa kuenda kushiriki zoezi hilo.

Maeneo bunge hayo ni Kisumu ya Kati, Kisumu Mjini Magharibi, Kisumu Mjini Mashariki, Muhoroni, Seme, Nyakach na Nyando.

Wakazi wengi wengi, hata hivyo, walisema wamezongwa na shughuli za kujitafutia riziki na hivyo hawana haja ya kutoa maoni yao kuhusu hoja hiyo

Hali kama hiyo pia ilishuhudiwa katika kaunti za Mombasa na Nairobi.

Wakati huo huo, watu wanaoishi na ulemavu (PWDs) katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya wametofautiana kuhusu hoja ya kumbandua Naibu Rais Bw Gachagua.

Mwenyekiti wa muungano wa PWD kaunti ya Mandera Bw Hafid Maalim alipinga hoja hiyo akiitaka kama inayooongozwa na nia mbaya ya kisiasa akisema wabunge wajikite katika changamoto za kiuchumi zinawasibu Wakenya.

Lakini mwenyekiti wa muungano huo kaunti ya Garissa Bw Adan Hassan aliunga mkono hoja hiyo akisema Bw Gachagua amekuwa akiendeleza ukabila nchini.

Ripoti za Mercy Mwende, Manase Otsialo, Mwangi Ndirangu, Pius Maundu, Rushdie Oudia, Titus Ominde, George Munene, Evans Jaola, Oscar Kakai na Stephen Munyiri

Imetafsiriwa na Charles Wasonga