• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Sabina Chege kusukuma kurejeshwa vikao vya elimu ya ziada; wazazi na wanafunzi wanasemaje kuhusu ‘tuition’?

Sabina Chege kusukuma kurejeshwa vikao vya elimu ya ziada; wazazi na wanafunzi wanasemaje kuhusu ‘tuition’?

Na MWANGI MUIRURI

MWAKILISHI wa Wanawake wa Kaunti ya Murang’a katika bunge la kitaifa, Sabina Chege ameandaa mswada bungeni akitaka elimu ya ziada almaarufu ‘tuition’ irejeshwe.

Analenga kufanyia marekebisho sheria ya Basic Education Act (2013), na ambayo ndiyo hudhibiti elimu ya sekondari na ya msingi.

Akiwa tayari amefanya hivyo kupitia kwa kamati ya elimu bungeni inayoongozwa na mbunge wa Tinderet Julius Melly, Bi Chege anasema kuwa lengo lake kuu limewekezwa katika busara yake ya kibinafsi kuwa kuna wanafunzi ambao wana ugumu wa kuelewa masomo na ndiposa wanafaa kusaidiwa kupitia elimu hiyo ya ziada.

“Ibara ya 10 katika marekebisho yangu ni kuwa, elimu hiyo ya ziada irejeshwe ndipo wale walio na changamoto ya kushika kwa kasi masomo wapate fursa ya kuhimiziwa au kusisitiziwa waliko na ugumu na waelewe. Pia ninapendekeza kuwa katika shule yoyote ile ambayo itakumbatia elimu hiyo ya ziada, kila mzazi akubali kupitia hiari yake bila shinikizo na kukubali huko kuwe katika maandishi yaliyotiwa sahihi na msimamizi wa shule na mzazi,” asema Bi Chege.

Marekebisho hayo ya Chege ambayo anasukuma pia yanalenga kutoa shinikizo kwa wizara ya elimu kupitia waziri husika kujitwika wajibu wa kuwalipia karo wote ambao ni werevu, wamepita mitihani lakini hawana hela za kuendelea na masomo.

Taifa Leo iliingia mtaani kusaka maoni ya hali hii na haya hapa ni baadhi ya majibu tuliyokumbana nayo.

Njeri Kibui

“Mimi ni mzazi na ninapinga marekebisho hayo ya Bi Chege. Nikiwa kutoka Kaunti ya Kiambu, nimejionea kwa macho yangu na pia nikashuhudia moja kwa moja elimu hiyo ya ziada ikitumiwa kupora wazazi. Sijapata mahala popote katika marekebisho hayo ambapo Bi Chege amepependekeza elimu hiyo iwe bila malipo. Ninaunga mkono hali ya sasa ambapo Basic Education Act (2013) huifanya ‘tuition’ kuwa ukiukaji wa kanuni na sheria na ambapo atakayenaswa akijihusisha nayo adhabu ni mwaka mmoja gerezani au faini ya Sh100,000 au zote mbili.”

Rimmon

“Mimi sitaki kushinikizwa niwe katika darasa kila wakati. Mimi huwakosa sana nyanya yangu na babu yangu kutoka mashambani. Shule zikifungwa ndio wakati mimi hupata fursa ya kusafiri hadi mashambani kukaa na jamaa na marafiki wa mashinani. Sabina Chege anafaa ajue niko na haki ya kutembelea mashinani na anafaa ashtakiwe na Okoiti Omtatah ikiwa analenga kunipiga marufuku ya pia kujumuika na starehe za likizo. Tukipiga kura katika shule yetu ninajua tutakataa marekebisho hayo!”

Rose

“Sidhani Bi Chege anajua anachosukuma kwa kuwa kwa sasa tumeambiwa mfumo wa elimu unabadilishwa ili tukumbatie uwezo wa kielimu na wa kiufundi na hata usanii katika wanafunzi. Ikiwa mwanafunzi haelewi masomo, badala ya kumshinikiza awe katika darasa akisomeshwa katika hali ambayo itaonekana unamtesa, unafaa kumchunguza ujue uwezo wake kamili ni mgani. Hivyo ndivyo atathibitiwa katika mkondo wa kujitambua na ajengwe katika uwezo huo wake. Hata Bi Chege hakuanza maisha haya akiwa mwanasiasa. Alijitambua baadaye na kwa kuwa aliungwa mkono, akafaulu. Mbona hakuanza maisha kama mwanasayansi au mhubiri? Uwezo ndio wa kuzingatiwa.”

Waithaka

“Ninaunga mkono marekebisho hayo ya Bi Chege kwa kuwa kwanza, nampenda kama mwanasiasa wa Kaunti yangu ya Murang’a. Pili, Bi Chege alikuwa mwenyekiti wa kamati hiyo ya Elimu katika kipindi cha awamu yake ya kwanza bungeni kati ya 2013 na 2017. Akiwa katika kamati ya Afya kwa sasa, ameonyesha kuwa ako na uwezo wa kujadili masuala yanayoathiri mwananchi kwa njia ya ueledi, busara na hekima. Ikiwa ameonelea hii elimu ya ziada inafaa, basi kama aliyeanza maisha yake ya kitaaluma kama mwalimu wa sekondari kisha akawa mtangazaji na muigizaji, na sasa mwanasiasa, ako na tajiriba ya kuelewa kuhusu masuala ya kijamii. Namuunga mkono.”

Mukami

Mukami wa Gredi ya Sita. Picha/ Mwangi Muiruri

“Kibinafsi ninaunga mkono marekebisho hayo ila tu kwa masharti. Ikiwa ni lazima elimu hiyo ya ziada irejeshwe, basi iwe ni kwa kila mwanafunzi wala sio kwa njia ya kuwabagua wengine. Ikiwa wale ambao ni wadhaifu ndio watashirikishwa, ikiwa watapata makali zaidi na wale ambao walidhaniwa kuwa wababe kimasomo waanguke, si huo utakuwa ni ubaguzi wa wazi? Ikiwa baadhi ya wale wadhaifu watakosa wazazi wa kugharimia elimu hiyo na wengine wapate pesa za malipo, si tutaunda ubaguzi zaidi na utengano wa uwezo katika mitihani? Hii ni njama tu ya kuwapa walimu wakuu kijisababu cha kubagua wazazi na wanafunzi na kuwatenganisha katika msingi wa uwezo wa pato.”

Mercy

Mercy, Kidato cha Tatu. Picha/ Mwangi Muiruri

“Bi Chege katika siku za hivi punde amekuwa na shida ya kimaoni. Sijui ni kwa nini amekuwa akiniangusha kwa kiwango kikuu kutokana na matamshi yake ya kukera. Juzi nimemuona kwa runinga akipongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwapa kazi wanasiasa walioanguka kura – wa kutoka Murang’a – kazi. Nilijiuliza kama hao ndio wanaosaka kazi katika kaunti yangu ya nyumbani Murang’a. Juzi amekuwa katika vyombo vya habari akisema kuwa watumizi wa mihadarati wasiwe wakiadhibiwa kwa kuwa ni wagonjwa. Sasa anasema watoto wanyimwe haki yao ya kupumzisha akili kutoka muhula wa kimasomo. Hata kumjadili Bi Chege kunaniudhi kabisa.”

Marvin

Marvin wa Gredi ya Kwanza. Picha/ Mwangi Muiruri

“Mimi sina udhaifu wa masomo kwa kuwa ni vigumu niwe nambari mbili. Mimi huwa nambari moja katika mitihani. Wale ambao hawapiti mitihani wanafaa watie bidii wakiwa nyumbani kwa likizo na wasaidiwe na wale wamesoma katika familia zao. Mimi sipendi kila saa kuwa karibu na mwalimu kwa kuwa hunikanya kuwa huru kucheza. Likizo ni nzuri sana kwa kuwa hata ndio wakati unapata fursa ya kutembea katika maeneo mengi ya nchi. Wale wetu ambao hawakupata nafasi ya kututembelea shuleni tunakutana nao wakati wa likizo. Mimi hata ikisemwa niwe nakaa shuleni wakati wa likizo nitakataa. Nitaambia mamangu anihamishe au amshtaki mwalimu huyo kwa waziri Fred Matiang’i. Huyo waziri alisema wakati wa kufungwa shule tukae nyumbani au tukamatwe wote. Mimi sitaki kwenda jela, huyo mbunge apelekwe jela mwenyewe.”

You can share this post!

Mutua ‘azima’ matumaini ya seneta kuhusu Sh390...

KINAYA: Mariga hana deni lako, huwezi kumlazimisha kufanya...

adminleo