Safari ya maisha ya kijana ambaye koroboi haikuzima ndoto yake
Na MWANGI MUIRURI
@Mlincoln
WAKATI Kelvin Karani alijiunga na darasa la nane mwaka wa 2013, hisia za jinsi familia yake ilikuwa ikimtegemea kuiongoza kutoka maisha ya uchochole zilimkaba, akiahidi angewajibikia ‘jukumu’ hilo.
Alielewa kuwa akiwa kitindamimba katika familia yao ya watoto wengine watatu ambayo baba hufanya vibarua katika sehemu za kupata malighafi ya ujenzi huku mamake akiwa kibarua wa kusaka riziki kijijini, ikiwa angemakinikia uthabiti wake ndani ya elimu, basi angeishia kuwa mwokozi katika familia hiyo.
Anasema akiwa darasa la nane alianza kung’amua hali halisi ya familia yao kuwa ikiwa kupata elimu, chakula na mavazi ilikuwa shida, basi angezubaa katika masomo, angeishia tu kusononesha wazazi wake ndani ya lindi la umaskini mkuu usio na matumaini.
“Nilielewa kuwa mimi nilikuwa tegemeo kuu kwa wazazi wangu. Walikuwa wananiombea sana na kunishauri nizingatie elimu kama uwekezaji wa familia yetu. Nilikubali kwa asilimia 100,” anafichua.
Katika ndoto zake, alikuwa amejipa ratiba ya kuafikia ufanisi wa baadaye ambapo alikuwa akitazamia kupita vizuri mtihani wa darasa la nane, ajiunge na Shule ya Upili ya Wavulana ya Starehe, aingie chuo kikuu na asomee taaluma ya uhandisi na hapo safari ya kuandika awamu mpya ya historia ya familia yao ianze.
‘Nilikuwa natazamia mimi nikiwa mhandisi na niwe na pato, niinue familia yetu kutoka kwa umasikini, nijijenge pia na nizindue familia yangu ambayo ingeepuka mahangaiko ya maisha ya familia yetu,” anasema.
Mei 16, 2013, Karani alikuwa akidurusu usiku wa manane kujiandaa kwa mtihani aliokuwa aufanye asubuhi iliyofuatia katika shule ya msingi ya umma ya Mugumo-ini.
“Sikuwa nikifanya masihara katika masomo yangu. Nilikuwa nalenga kuweka msingi thabiti wa imani kwa wazazi wangu kuwa nilikuwa na uwezo wa kupita mitihani. Nilisoma mara nikasinzia na nikalala. Taa ya koroboi ambayo nilikuwa naitumia kupata mwangaza nikisoma ilikuwa karibu nami,” anasema.
Anasimulia kuwa hajui jinsi alivyoishia kulala karibu na miale ya moto wa taa hiyo.
Wakati alielewa kuwa alikuwa ameshika moto, moto ambao ulikuwa umeshika fulana yake aliyokuwa amevaa kujikinga makali ya baridi kwa kuwa nyumba yao ni ya mabati juu na kando, hakuwa na nguvu kupiga usiahi anusuriwe au ajinusuru.
“Niliamshwa na harufu ya shaka ndani ya moshi mwingi ndani ya nyumba. Kwa giza na nikiwa bado na maruerue ya usingizi, nilichukua tochi na nikaiwasha… Ole Wangu! Picha mbovu zaidi maishani mwangu hadi sasa ya mtoto wangu akiwa amezirai huku akiteketea,” anasimulia babake mzazi, Alfred Njoroge.
Baba hakujali kuwa yeye ni mwanamume ambaye huzimwa na ujasiri kupiga nduru aghalabu katika baadhi ya desturi ambazo asili yake haiko wazi.
Alipiga usiahi, tena kwa sauti na hapo mama mtoto aliamka na kuzidisha nduru na kuwavutia majirani.
Taharuki kuu katika boma hilo liloko katika kijiji cha Kabaria ndani ya Kaunti ndogo ya Kigumo!
Shughuli ya uokozi bila mpangilio huku majirani wakisaidia ilishuhudiwa.
Walizima moto na hatimaye mtoto akapelekwa katika hospitali ambayo ilikuwa kilomita 30 katika Mji wa Maragua ndani ya Kaunti ya Murang’a.
Kwa miezi minne, Karani akawa mkazi ndani ya hospitali hiyo akitibiwa. Wauguzi wakifanya juu chini kunusuru maisha yake..
“Huo usiku wa mtoto wangu kushika moto ndio usiku mimba yangu ya miezi mitano ilitoka. Nilimwona akiwa anaaga dunia…mtoto niliyemzaa na kumlea hadi kiwango hicho cha kuwa darasa la nane…tegemeo la familia yetu maishani….Mungu ni mwema kwamba leo hii huyu mtoto yu hai na nitamshukuru Maulana milele kumhusu,” asema mamake Karani, Bi Susan Murugi.
Alipoachiliwa kutoka hospitali ya Maragua, ingawa akiwa na alama ya kimaisha katika mbele ya shingo lake, alishikilia kuwa bado alikuwa na ile ndoto yake ya kufanikiwa kimaisha kupitia elimu.
Ingawa madaktari wake walimwelekeza kuwa angehitaji upasuaji maalum baada ya miaka mitano ili ulemavu aliopata katika shingo lake na ambalo humwathiri katika maongezi kwa kuwa mdomo uliathirika pia, huu ni mwaka wa sita na umasikini ndani ya familia yao haujamwezesha kupata ufadhili wa kutibiwa.
“Hilo si hoja, Mungu amekuwa mwema kwangu hadi leo hii. Cha maana ni kuwa mimi sio mtu wa kupoteza imani katika maisha. Aliyeninusru kutoka kwa mauti ya moto ndiye aliniponya na ndiye bado nategemea kunifanikishia ndoto za maisha yangu. Na huyo ni Mungu Muumba wa yote, wote na vyote,” anasema Karani.
Alirejelea masomo yake Oktoba 2013 na akafanya mtihani wa kujiandaa kwa ule wa mwisho wa KCPE na akapata maksi 319 dhidi ya 500.
Alishangaza wazazi, walimu na wengine waliopata ufahamu kwa kuwa, nje ya darasa kwa takriban miezi sita, akipona majeraha yaliyokuwa na hatari ya kumwangamiza, alipata alama hizo.
Wakistaajabu ya Musa, ya Firauni yakaja yakibebwa na uyu huyu Karani kwa kuwa alipata maksi 342 katika matokeo rasmi ya KCPE 2013.
Changamoto ya ukosefu wa karo ikamwandama na baada ya kushauriana kama familia, aliamua kurudia darasa la nane tena na mwaka wa 2014, karani akapata maksi 372/500.
“Bahati sasa ikasimama kwa kuwa mabwanyenye wa Kaunti ya Murang’a walikuwa wameunda wakfu wa kusaidia watoto kutoka familia maskini kupata elimu. Mtoto wangu akapata ufadhili na akajiunga na shule ya upili ya Njiiris,” anasema babake.
Anasema kuwa “mimi pamoja na bibi yangu tulilia machozi tulipomuona mtoto wetu akibeba sanduku lake akipishwa ndani ya bweni akaanze maisha yake kama mwanafunzi ndani ya shule hiyo ya hadhi Kaunti ya Murang’a.”
Miaka minne baadaye, leo hii Karani anatazamia kujiunga na Chuo Kikuu cha Technical University of Kenya (TUK) baada ya kupata alama ya A (-) ya pointi 76.
Kozi ambayo anaingia kufanya ni uhandisi wa kimawasiliano na stima.
“Hadi sasa bado niko kwa mkondo wa Baraka za Maulana. Nyuma kuko sawa, na mbele naona kuko sawa. Nimeanza kunusa ufanisi sasa. Nimeanza kuona taswira ya mamangu akikoma kupewa kazi za kibarua na majirani. Namuona babangu akiondoka kutoka huko anakochimbia mabwanyenye malighafi ya ujenzi. Naona watoto wetu wengine watatu wakipata ufadhili kutoka kwangu wa kuafikia ndoto za maisha yao…” anasema akilengwalengwa na machozi.
Kinachobakia sasa, ni apate ufadhili wa kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha ulemavu shingoni na mdiomoni mwake na pia apate ufadhili wa Bodi ya Utoaji wa Mikopo kwa Wanaosomea Elimu ya Juu, Higher Education Loans Board, (Helb), hazina ya basari ya mbunge wa Kigumo, Wangari Mwaniki na wahisani hapa na pale kupata hela za lufanikisha awamu hii yake muhimu ya kuelekea kuafikia ndoto zake za kimaisha.