Safari ya Zack Kinuthia kielimu hadi kuwa Waziri Msaidizi wa Elimu
Na MWANGI MUIRURI
SAFARI ya Naibu Waziri wa Elimu Zack Kinuthia ya kuishia katika makuu ya serikali ilikuwa na changamoto tele.
Ni safari ambayo isipokuwa ni neema za Maulana kijana huyu wa Mama Lucy Mugure kutoka kijiji cha Gatitu kilichoko kaunti ndogo ya Kigumo ndani ya Kaunti ya Murang’a ingekwama.
Kwa mujibu wa mamake, kijana huyu ambaye wengi walishtushwa Januari 15 ambapo Rais Uhuru Kenyatta alimteua katika wadhifa huu, safari ya mwanaye hadi sasa inaweza tu ikatajwa kama Baraka ya muujiza wa Mungu.
“Alipokamilisha elimu ya darasa la nane, nilikosa karo ya kumwezesha kujiunga na shule ya upili ya Kigumo Bendera, nikamsihi arudie masomo ya shule ya msingi kwa kawaida yake kuwa mtiifu na aliyeelewa masaibu yangu ya kifedha, alitii,” asema mama huyo.
Kinuthia sasa alipata mwaliko wa kujiunga na shule ya upili ya Gaichanjiru iliyoko katika kaunti ndogo ya Kandara lakini yapo madai kuna ukora ulichezwa na barua yake akakabidhiwa mtu mwingine.
“Nilililia mwalimu mkuu katika shule hiyo ya upili akubali kumpa mtoto wangu nafasi na akaingiwa na utu na akampokea,” asema.
Shida kubwa ilikuwa kupata karo ya kumwezesha Kinuthia kukamilisha elimu yake ya sekondari.
“Nilikuwa nachotea majirani maji ili wanilipe pesa za kumlipia Kinuthia karo. Kwa mtungi mmoja nilikuwa nikilipwa Sh10. Nilikuwa pia nikipewa kibarua cha kudumisha usafi katika kituo cha polisi cha Kigumo ambapo nilikuwa nikipokezwa Sh80 kwa siku moja ya kufanya kazi kwa masaa 10. Kwa kila lisaa malipo yalikuwa Sh8,” asema.
Mama Mugure anasema kuwa kijana huyu alikuwa mjasiri na mtulivu na uwezo wake wa kuhimili mipigo ya kimaisha ulimwandama akiwa mdogo baada ya kushuhudia na kuelewa kuhusu shida za kifedha katika maisha ya mamake mzazi.
Ni ujasiri huu ambao ulimwezesha kuwania urais wa Chuo kikuu cha Nairobi kwa wanafunzi mwaka wa 2013 na akafanikiwa.
Akiwa katika chuo hiki cha Nairobi kama Rais wa wanafunzi, Naibu Chansela alikuwa Prof George Magoha ambaye kwa sasa ndiye amekutana naye katika Wizara ya Elimu sasa (Magoha) akiwa mkubwa wake.
Aidha, alijipenyeza hadi kwa mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto na ambapo alizindua miradi kemkem ya kisiasa akiwaunga mkono hadi kwa jitihada zake na wengine, UhuRuto wakaunda serikali.
Weledi wake wa kusoma jinsi mawimbi ya kisiasa yanavyovuma ulimwezesha kukoma kumuunga mkono Ruto na badala yake akabakia mfuasi sugu wa Rais Kenyatta.
Alhamisi imekuwa ni kinaya kikuu katika kaunti ndogo ya Kigumo ambapo maafisa wanaohudumu katika kituo kile mamake Kinuthia alikuwa kibarua akilipwa Sh80 kwa siku, ndio walikuwa katika msafara wa kumpa ulinzi kijana huyu akiwa katika ziara ya kikazi.
Mamake hakuficha furaha yake alipojitokeza barabarani kumlaki mwana, akiwa na fahari kuu ya kumwona aliyehangaika naye akimwelimisha sasa ameafikia makubwa ya hadhi.
Huku maafisa wa polisi na walinzi wakiwazima wengine kumsongea Kinuthia, wakati mama alitokea usalama huo ulikaa kando na mama na mwana wakasongeana wakijuliana hali na baadaye akimjulisha kwa wote waliokuwa hapo karibu kama “mzazi aliyenileta duniani hii na akanilea kwa maziwa yake na nguvu zake hadi nikawa mimi huyu hapa.”
Ni picha ambayo ilisababisha machozi ya tafakari kwa wengi waliokuwa katika msafara huo huku wengine wakisikika wakisema kwa sauti “Mungu wa waja halali na huu ni ushahidi tosha.”