• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Safu yote ya Seneti kusikiliza kesi dhidi ya Dkt Monda

Safu yote ya Seneti kusikiliza kesi dhidi ya Dkt Monda

NA CHARLES WASONGA

VIKAO vya kusikiliza kesi dhidi ya Naibu Gavana wa Kisii Robert Monda aliyetimuliwa na madiwani, vitafanywa na safu ya maseneta wote.

Hii ni baada ya kuangushwa kwa hoja iliyowasilishwa na kiongozi wa wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot kutaka kuundwa kamati ya maseneta 11 kuchunguza mashtaka dhidi yake.

Hoja hiyo ilianguka baada ya Seneta huyo wa Kericho kukosa kupata muungaji mkono wa hoja hiyo.

Hii ni baada ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ambaye alikuwa ameteuliwa kutekeleza wajibu huo, kukataa dakika za mwisho.

“Ama kwa hakika nilimwambia Kiongozi wa Wengi kuniondoa kwenye orodha ya wanaounga mkono hoja hii,” Bw Sifuna akasema.

Baada ya usemi huo, Spika wa Seneti Amason Kingi alitangaza kuwa hoja hiyo ilikuwa imefeli.

“Ni wazi kwamba ewe kiongozi wa wengi huna muungaji mkono wa hoja hii,” Spika Kingi akasema.

Spika akaongeza: “Kwa hivyo, hoja ya kubuniwa kwa kamati ya wanachama 11 kushughulikia hoja ya kumwondoa afisini Naibu Gavana wa Kisii Robert Monda imefeli. Sasa suala hili litashughulikiwa katika kamati ya bunge lote. Nitatoa mwelekeo zaidi baada ya muda mfupi.”

Awali, Seneta Cheruiyot alikuwa amependekeza kubuniwa kwa kamati ya maseneta 11 kuchunguza madai dhidi ya Bw Monda.

Mawakili wa Monda na madiwani 53 watafika mbele ya seneti kutetea misimamo yao.

Pande hizo mbili pia zitapewa nafasi ya kuwasilisha mashahidi wao ili kujenga kesi zao.

Madiwani wa Kisii walipitisha hoja ya kumng’oa afisini Dkt Monda mwezi Februari baada ya madiwani 53, kati ya 70 kuunga mkono hoja hiyo.

Diwani mmoja alisusia shughuli hiyo ilhali wengine  13 wakaipinga.

Sehemu ya 33 (2) (a) ya Sheria ya Serikali za Kaunti inasema kuwa Spika wa Bunge la Kaunti atamjulisha Spika wa Seneti kuhusu uamuzi wa bunge lake ndani ya siku mbili.

Baada ya kutimuliwa kwa Dkt Monda mnamo Februari 29, 2024, afisi ya Bw Kingi ilijulishwa mnamo Machi 2, 2024, kuhusu uamuzi huo.

Miongoni mwa tuhuma dhidi ya Dkt Monda ni matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake, ukiukaji wa Katibu na mienendo mibaya.

Dkt Monda amekana mashtaka hayo yote.

“Sijawahi kukabiliwa na tuhuma za ufisadi maishani mwangu. Wakati huu ndio ninasikia mambo kama hayo. Ninamajibu tosha na ni wajibu wa wadhamini wa hoja hii kuhakikisha kuwa wanajenga kesi yao dhidi yangu,” akasema.

Hoja za kuwaondoa afisini magavana na manaibu gavana huibua mgawanyiko katika Seneti huku pande za Kenya Kwanza na Azimio zikikinzana.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Seneti kushughulikia hoja ya kumwondoa afisini Naibu Gavana.

Hoja ya kwanza ilikuwa mwaka 2023 ambapo Naibu Gavana wa Siaya William Oduol aliponea.

Hii ni baada ya maseneta wa Kenya Kwanza kutumia wingi wao kuwalemea wenzao wa Azimio waliotaka Dkt Oduol atimuliwe.

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa watano wakamatwa Mukuru, maafisa waharibu lita...

Mackenzie aomba apunguziwe mashtaka kutoka 191 hadi 12

T L