Makala

Samidoh atoa ushahidi unaokinzana na maelezo ya DJ Fatxo kuhusu kifo cha Mwathi

Na RICHARD MUNGUTI August 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANAMUZIKI maarufu Samuel Muchoki almaarufu Samidoh Jumatatu (Agosti 11,2025) alikanusha madai kwamba mtaalam wa marembo ya nyumba Jeff Mwathi alijitoa uhai.

Akitoa ushahidi katika uchunguzi unaondelea katika mahakama ya Milimani kubaini kilichosababisha kifo cha Mwathi, Samidoh alisema “alipofika katika makazi ambapo Mwathi alidaiwa aliruka kutoka kwenye orofa na kuanguka chini alikuwa na tashwishi kuhusu madai ya muuzaji nguo huyo kujiua.”

Samidoh alimweleza hakimu mwandamizi Rose Ndombi kwamba alimjua Mwathi tangu utotoni na kamwe “hangejiua.”

Mahakama ilijulishwa kwamba Mwathi na DJ Fatxo wametoka katika Kaunti ya Nyandarua.

Alimsifu DJ huyo kama mkufunzi wake katika masuala ya muziki na hakuwa na nia mbaya ya kumharibia sifa kwa njia yoyote ile.

“DJ Fatxo ndiye alinifundisha mambo ya muziki. Ninamuunga mkono niwezavyo na kamwe sina nia ya kumhujumu. Kile nataka ni kujua kilichomuua binamu yangu,” Samidoh alieleza mahakama.

Samidoh ambaye pia ni afisa wa polisi aliambia mahakama alipigiwa simu na Dj Fatxo mnamo Februari 22, 2023 na kumweleza Mwathi ametoweka.

Afisa huyo wa polisi alikuwa anahudhuria mkutano Kiambu.

Alikawia kufika kwa makazi ya Mwathi na hakuchukulia suala hilo kwa uzito akisema mmoja huripotiwa ametoweka baada ya masaa 72.

Hata hivyo, alifululiza hadi kituo cha polisi cha Kasarani siku iliyofuata kupiga ripoti.

Kwa mujibu wa afidaviti iliyowasilishwa kortini Machi 27, 2023, familia ya Mwathi ilifahamishwa alijiua kwa kuruka kupitia kwenye dirisha.

Samidoh aliambia mahakama aliingiwa na tashwishi na kufikiria Mwathi alirushwa nje.

Samidoh alifichua kwamba alipowasili katika makazi ya Redwood Apartments ambapo Mwathi alifia, polisi walikuwa hajaweka utepe kuzuia watu kufika alipokuwa ameanguka.

Aliwapata wasichana watatu na wanaume wawili waliodaiwa kutoka Tatu City.

Kwa makisio aliambia korti Mwathi alikufa kati ya 11 alfajiri na saa 12.

Polisi walifika saa moja baadaye.

Mahakama ilielezwa video za kamerza za CCTV zilionyesha DT Fatxo aliondoka akiwa na wasichana watatu.

Mwathi hakuandamana nao.

Pia alisema kutokana na video hizo aliona Mwathi akianguka.

Alipohojiwa na wakili Danstan Omari, Samidoh alisema kitanda cha Mwathi kilikuwa kimetandikwa barabara na hakikuwa kimesukumwa kwenye ukuta kubashiri alikikanyaga akijirusha.

Mahakama ilielezwa Mwathi alirushwa kupitia dirishani.

Uchunguzi utaendelea Agosti 18-19, 2025.