Makala

Sarah Wairimu aachiliwa kwa masharti makali

October 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Ijumaa ilimwachilia kwa masharti makali ya dhamana Sarah Wairimu Kamotho anayekabiliwa na shtaka la kumuua mumewe Tob Cohen huku mshukiwa mwingine Peter Karanja akishtakiwa.

Jaji Stellah Mutuku, alimwamuru Sarah awasilishe dhamana ya Sh4 milioni na wadhamini wawili wa Sh2 milioni kila mmoja.

Akishindwa kupata dhamana hiyo, Sarah aliagizwa alipe dhamana ya Sh2 milioni pesa taslimu.

Akitupilia mbali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) la kupinga mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana, Jaji Mutuku alisema, “ Korti imepewa mamlaka na uwezo kuhakikisha kwamba mshukiwa yeyote hajawavuruga mashahidi.”

Jaji huyo alisema upande wa mashtaka unaongozwa na Bi Catherine Mwaniki na Bi Wangui Gichuhi haukuwasilisha ushahidi wa kutosha kuiwezesha mahakama kumnyima dhamana mshtakiwa ambaye amekaa rumande kwa siku 46 tangu alipotiwa nguvuni.

“Dhamana ni haki ya kila mshukiwa hata ikiwa anakabiliwa na kesi ya aina gani. Haki hii inaweza tu kutwaliwa na mahakama iwapo kuna ushahidi wa kutosha mshukiwa atavuruga kesi ama kwa njia moja au nyingine,” alisema Jaji Mutuku.

Jaji huyo alitupilia mbali ombi la mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kuomba mshtakiwa anyimwe dhamana akisema “hakuwasilisha ushahidi wowote kuthibitisha kwamba Sarah atatoroka na atawavuruga mashahidi.”

Hata hivyo Jaji huyo alimwekea Sarah masharti makali ya kuondoka gereza la Langata alikozuiliwa baada ya kukanusha shtaka la kumuua mumewe usiku wa Julai 19/20, 2019.

Jaji Mutuku alimwamuru Sarah asithubutu kukanyaga katika jumba lao lenye thamani ya Sh400 milioni katika mtaa wa kifahari wa Kitisuru hadi kesi inayomkabili isikizwe na kuamuliwa.

“Ikiwa unataka kuenda katika nyumba hiyo mlikoishi na marehemu, basi itakubidi uwasilishe ombi hapa mahakamani ndipo usindikizwe na maafisa wa polisi kurudi huko,” alisema Jaji Mutuku.

Ushahidi

Jaji huyo alisema jumba hilo la kifahari liko chini ya uangalizi wa polisi na linalindwa kwa vile ni mojawapo ya ushahidi.

Tangu aliposhikwa Agosti 28, 2019, jumba hilo liliwekwa chini ya ulinzi wa polisi.

Mwili wa Cohen, raia wa Uholanzi mwenye asili ya Kiyahudi ulikutwa umetupwa ndani ya tangi la maji.

Maiti yake ilipatikana baada ya siku 60 tangu aripotiwe kutoweka.

Pia mshtakiwa aliagizwa asitembelee biashara za mumewe hata ikiwa alikuwa mshirika katika kampuni hizo.

Jaji Mutuku alimwagiza mshtakiwa awasilishe mahakamani anwani za wadhamini watakaomsimamia dhamana.

Pia aliamriwa awasilishe anwani ya baba yake mzazi, Bw Japheth Kamotho ambaye mahakama ilifahamishwa ndiye atakuwa akiishi naye katika eneo la Lanet, Kaunti ya Nakuru.

Jaji huyo pia alimtaka Sarah aliyekana kumuua mumewe usiku wa Julai 19/20, 2019, awasilishe mahakamani maelezo jinsi atakavyokuwa akijikimu kimaisha ikitiliwa maanani “alikuwa anamtegemea mumewe.”

Jaji Mutuku alimwamuru mshtakiwa asiwashawishi wafanyakazi aliokuwa amewaajiri kwa vile ni mashahidi katika kesi hiyo.

“Wakati utakapokuwa nje hautazugumza na nduguye marehemu Dkt Bernard Cohen na dada yake Bi Gabrielle,” aliagiza Jaji Mutuku.

Jaji huyo atawahoji wadhamini watakaofika kortini kuomba wawe wadhamini watakaomlipia Sarah dhamana.

Bi Mwaniki aliomba mahakama iruhusu maafisa wa afisi ya DPP kuwahoji wadhamini watakaofika kortini kule walikotoa pesa Sh2 milioni watakazomlipa dhamana Sarah.

“Hatutakubali pesa zilizopatikana kwa njia isiyofaa kutumika kumlipia dhamana mshtakiwa,” alisema Bi Mwaniki.

Ombi hilo lilimgwara wakili anayemwakilisha Sarah, Bw Philip Murgor aliyesema “hatutalipa na noti za Sh1,000 zilizopigwa marufuku.”

Bw Murgor alieleza mahakama hajui pesa zilizopatikana kwa njia ya ufisadi huwa zimekaa namna gani.

Mahakama ilimruhusu Bi Mwaniki au afisa mwingine yeyote kuwako wadhamini wakihojiwa.

Baadaye Ijumaa mwendo wa saa kumi na mbili na nusu Sarah aliachiliwa kutoka gerezani na kupelekwa nyumbani Lanet, Nakuru na baba yake baada ya kulipa dhamana.