Sasa ni afueni kwa Gen Zs, baada ya serikali kuondoa rasmi ada ya vitambulisho
WAKENYA sasa wamepata afueni baada ya serikali kufutilia mbali ada ya Sh300 inayotozwa wanaowasilisha maombi ya vitambulisho vya kitaifa, kulingana na agizo la Rais William Ruto.
Kulingana na toleo la Jumatano (Machi 19, 2025) la gazeti rasmi la serikali, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alifanya mabadiliko kwa Sheria ya Usajili wa Watu kuondoa ada ya kupata hati hiyo muhimu.
“Kwa kutekeleza mamlaka yaliyoko katika sehemu ya 16 ya Sheria ya Usajili wa Watu, Waziri wa Usalama wa Ndani anatoa kanuni ifuatayo: Kwamba Mpangilio wa Sita wa Kanuni ya Kanuni ya Usajili wa Watu imefanyiwa mabadiliko kwa kuondoa “Sh300” inayotajwa kama ada inayotozwa mtu ambaye hajawahi kupata kitambulisho cha kitaifa. Kwa hivyo, hakuna ada yoyote itakayotozwa anayetuma maombi ya kitambulisha cha kitaifa mara ya kwanza,” Bw Murkomen akaeleza.
Akiongea katika eneo la Kibra, Nairobi, wiki jana Rais Ruto alitangaza kuwa Wakenya waliotimu umri wa miaka 18 kwenda juu watapewa vitambulisho vya kitaifa bila malipo.
Juni 2024, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki (ambaye kwa sasa ni naibu wa rais) aliongeza ada ya kupata vitambulisho vya kitaifa kutoka Sh100 hadi Sh300.
Lakini akiondoa ada hiyo Alhamisi wiki jana, Rais Ruto alisema kuwa serikali yake inalenga kuhakikisha Wakenya wengine wanapata vitambulisho vya kitaifa bila kugharamika.
“Ningependa kutangaza nikiwa hapa Kibra leo (Alhamisi) kwamba vitambulisho vya kitaifa sasa vitatolewa bure. Tunataka kuhakikisha kuwa kila Mkenya anapata stakabadhi hii kumwezesha kupata huduma za serikali kwa urahisi,” akaeleza.