Makala

Sehemu ya bunge yateketezwa

Na SAMMY WAWERU June 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SEHEMU ya Bunge la Seneti imeteketezwa Jumanne, Juni 25, 2024 na kundi la vijana kufuatia maandamano yanayoendelea maeneo tofauti nchini.

Maandamano hayo yanayoongozwa na vijana wa kizazi cha sasa, maarufu kama Gen Z, yameonekana kuchacha Nairobi, Bunge la Seneti la lile la Kitaifa yakivamiwa.

Sehemu ya lile la Seneti imechomwa licha ya maafisa wa polisi kushika doria katika malango yake.

Moshi unaonekana ukifuka, huku makundi ya vijana wenye hasira na ghadhabu wakikimbizana na polisi kujaribu kuingia mabunge hayo mawili.

Duru zinaarifu wabunge wamehepa, kwa minajili ya usalama wao.

Vijana wanaandamana kupinga Mswada wa Fedha 2024, ambao Jumanne mchana ulipitishwa na Bunge la Kitaifa.

Mswada huo, ambao sasa unatarajiwa kutiwa saini na Rais William Ruto kuwa sheria kuiwezesha serikali kukusanya ushuru mpya wa Sh347 bilioni kufadhili bajeti ya mwaka wa 2024/2025, ulipitishwa na wabunge 195 waliopiga kura ya NDIO kuunga mkono marekebisho, huku wabunge 106 wakirusha kura ya LA, kuupinga.

Wengi wa waandamanaji wakiwa Gen Z, wanaukataa kwa msingi kuwa utachangia gharama ya maisha kupanda mara dufu.

Idadi ya watu isiyojulikana wanaripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, ikiwemo Chama cha Mawakili Nchini (LSK), yamekashifu vikali polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi kutuliza waandamanaji.

Jumapili, Juni 23, 2024, Rais Ruto aliahidi kufanya mazungumzo na vijana ili kuangazia malalamishi yao.