• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
SEKTA YA ELIMU: Sababu zinazochangia kushuka kwa utendakazi wa walimu nchini

SEKTA YA ELIMU: Sababu zinazochangia kushuka kwa utendakazi wa walimu nchini

Na CHARLES WASONGA

MIGOMO ya kila mara, mishahara duni na mazingira mabaya ya kufanyia kazi ni miongoni mwa sababu zinazochangia kushuka kwa viwango vya utendakazi wa walimu katika mataifa kadha ya Afrika, ikiwemo Kenya.

Kwa mujibu wa ripoti moja ya Benki ya Dunia ni kwamba licha ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kuanzisha mpango ambapo walimu wanahitajika kutia saini kandarasi ya utendakazi, hatua hiyo haijaimarisha utendakazi wa walimu.

Ripoti hiyo kwa kichwa, ‘The World Bank Development Report (2019)’ pia inatambua hali duni ya mafunzo katika vyuo vya mafunzo ya walimu kama sababu inayochangia walimu kutokuwa na umilisi ufaao wa masomo wanayofundisha.

“Hii ndiyo maana baadhi ya wanafunzi walio katika madarasa ya juu katika shule za msingi, hawawezi kumudu masomo ya viwango vya chini,” inasema ripoti hiyo iliyotolewa mwezi wa Juni mwaka huu.

Ufichuzi huu unaakisi matokeo ya tafiti kadha ambazo zimewahi kufanywa nchini na Shirika la Uwezo Kenya katika miaka ya awali.

Benki hii ambayo hufadhili mipango kadha katika sekta ya elimu nchini inapendekeza kupigwa kalamu kwa walimu watepetevu.

Aidha, inapendekeza kuboreshwa kwa mafunzo ya walimu, “kama njia ya kuzalisha walimu wanaomudu masomo watakayofundisha.”

Lakini katika mahojiano kwa ajili ya makala haya, Katibu Mkuu wa Chama Kitaifa cha Walimu (Knut) Wilson Sossion anasema kile kinachodaiwa kuwa utepetevu wa walimu husababishwa na mishahara duni na mzigo mkubwa wa kazi.

“Siwezi kukubali wala kupinga tathmini ya Benki ya Dunia. Lakini ukweli ni kwamba walimu wengi wamevunjwa moyo kutokana na malipo duni kwa upande mmoja na kazi nyingi kwa upande mwingine,” anasema.

Bw Sossion ambaye pia ni mbunge maalum aliyetuliwa na chama cha ODM kuwakilisha maslahi ya wafanyakazi, anaongeza kwamba ni kutokana na hali hii ambapo Knut imekuwa katika mstari wa mbele kupigania nyongeza ya mishahara ya walimu na kupandishwa vyeo kwa walimu ili “kuwapa motisha ya kuchapa kazi”.

Mapema wiki hii chama hicho kilitishia kuitisha mgomo kupinga hatua ya TSC kupunguza mishahara ya zaidi ya walimu 103,600 waliopaswa kunufaika kutokana na mkataba wa nyongeza ya mshahara (CBA) wa kati ya 2017 hadi 2021.

Adhabu

Itakumbukwa kwamba mapema mwaka wa 2017, Rais Uhuru Kenyatta aliamuru TSC kuwaadhibu vikali walimu wanaokosa kufika kazini “bila sababu maalumu”.

Akiongea katika Ikulu ya Nairobi alipoelezea kujitolea kwa serikali kutekeleza mkataba wa nyongeza ya mishahara (CBA) ya walimu katika miaka ya 2017 hadi 2021, Rais alisema kwamba tabia ya walimu kukosa kufika shuleni ndiyo imechangia kudorora kwa viwango vya elimu katika maeneo kadha nchini.

Lakini licha ya agizo hilo pamoja na hali kwamba TSC inatekeleza mpango wa kutathmini uwajibikaji wa walimu chini ya mwavuli wa kandarasi ya utendakazi, hakuna takwimu imetolewa kuonyesha idadi ya walimu waliopigwa kalamu kwa msingi wa utepetevu kazini.

Hii ina maana kwamba wadau katika sekta ya elimu bado wana kibarua kikubwa kuafikia azma ya kuimarisha utendakazi wa walimu.

  • Tags

You can share this post!

Nyadhifa za uongozi Jubilee Party...

KINA CHA FIKIRA: Umilisi wa Kiswahili u katika kuyamudu...

adminleo