Makala

Seneta Nyutu ajitangaza balozi wa mimba Mlima Kenya

March 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI 

SENETA wa Murang’a Joe Nyutu amesema atakuwa balozi wa mimba Mlima Kenya akiwa kwa wadhifa huo hadi 2032.

Bw Nyutu alisema hayo mnamo Ijumaa.

“Mimi ninanuia kuwa Seneta hapa Murang’a hadi 2032 na ninalenga kuacha kaunti hii katika kipindi hicho ikiwa na watu 2 milioni kutoka 1.1 walioko sasa,” akasema Bw Nyutu.

Alisema kwamba analenga pia kuacha Kaunti hiyo ikiwa na mgao wa Sh12 bilioni kutoka kwa Hazina Kuu, hii ikiwa ni nyongeza maradufu ya kiwango cha sasa.

Bw Nyutu akiongea katika Mji wa Maragua baada ya kushuhudia kufunguliwa tena kwa kiwanda cha maziwa cha Kaunti (MCC) ambacho kilikuwa kimesambaratika, alisema kwamba akikutana na mwanamke aliye na mimba atakuwa anampa pongezi.

“Nitakuwa ninampa mjamzito pongezi zangu kupitia zawadi ya pesa, bora tu isiwe ni kitambi cha kunywa uji,” akachekesha.

Bw Nyutu alisema kwamba kwa sasa anaeneza jumbe sita katika maeneo bunge yote Saba ya Kaunti, “tumuogope Mungu, tumtumainie, tutajirike, tuwekeze na tuongezeke kama jamii”.

Alisema analenga kuwa Seneta wa awamu mbili kwa kuwa utajiri wa Kaunti unaweza tu ukaitishiwa pesa za ufadhili kutoka bunge hilo.

Alisema kwamba katika kuafikia injili hiyo, atashirikiana na viongozi wote wa Kaunti “na tukiingia kwa debe 2027 kumchagua Rais William Ruto tena kwa awamu ya pili, tuwe tumejiweka pema kung’ang’ania urais 2032 kama Kaunti ya Murang’a”.

Bw Nyutu ni mfuasi sugu wa kupanda ngazi kwa mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Bw Nyutu alisema kwamba “kwa sasa tumempa Bw Nyoro nafasi ya kutembea katika Kaunti nyingine za maeneo nje ya Mlima Kenya ili ajifahamishe huko nasi huku nyumbani tukimshabikia kama shujaa na mzalendo”.

Seneta huyo alisema Kaunti ya Murang’a itachangia pakubwa siasa za 2027 na 2032.

“Sisi Murang’a tutakuwa katika mstari wa mbele kufanikisha siasa za Rais Ruto 2027 na pia za kitaifa 2032. Tutafanya hivyo kupitia kuunga mkono serikali hii iliyoko kwa sasa pamoja na mikakati yake na pia kumwombea Bw Nyoro kama shujaa wa kutoka hapa nyumbani,” akasema.

Alisema anaunga mkono vita dhidi ya pombe kiholela na mihadarati “lakini bora tu vita hivyo visigeuzwe kuwa ufisadi wa maafisa husika wa kuwakamata vijana kiholela na kuwadai hongo ili wasitupwe jela”.

Aidha, aliitaka serikali za kitaifa na Kaunti ziimarishe juhudi za kuzindua viwanda ili kuwapa kazi wafanyakazi wanaopoteza kazi katika baa zilizofungwa na pia wale wanaokombolewa kutoka kwa ulevi.

“Tukiwa tumeondoa ulevi kiholela na kisha tuwe na nafasi za kazi ya kuimarisha mapato katika familia tutakuwa na uhalali wa kudai familia ziongeze watoto,” akasema.

Alisema serikali ya Murang’a chini ya uongozi wa Gavana Irungu Kang’ata iko katika mkondo wa ufanisi “na Rais Ruto pamoja na Naibu wake Bw Rigathi Gachagua wameonyesha nia njema ya kutatua changamoto za nchi”.

Alisema kila mtu anatambua Bw Nyoro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya bajeti za utekelezaji maendeleo katika Bunge la Kitaifa.

[email protected]