Makala

Serikali ilifanya vizuri kutuondolea jukumu la nidhamu kwa wanafunzi -Mwalimu

April 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

WALIMU wengi nchini wanaepuka ugomvi na dharau kutoka kwa wazazi huku wakitumia mtindo wa kufunza na kisha kwenda nyumbani baada ya serikali kuondoa adhabu ya kiboko shuleni.

Sheria ya Elimu kwenye Katiba Ibara ya 36, inasema kuwa hakuna mwanafunzi atakayefanyiwa ukatili, unyama au adhabu ya kudhalilisha kwa namna yoyote ile, iwe ya kimwili au ya kisaikolojia. Wanaokiuka wanachukuliwa hatua kulipa faini ya Sh100,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani.

Mjini Nairobi, mwalimu Gedion Ntabo anasema mbinu hiyo ni afueni ili kuepuka mashaka kwa kurekebisha mwanafunzi. Alisema adhabu kwa wanafunzi imesalia jukumu la mzazi mwenyewe.

“Kuna wakati mwanafunzi aliadhibiwa kwa kuzuiliwa kwa muda. Hii ilikua adhabu ya dakika thelathini. Kilichotushangaza, mwanafunzi alifeki kuzimia na kumwarifu mzaziwe. Mzaziwe alifika shuleni akiwa amewaka na kurusha cheche za maneno mazito mazito. Wanafunzi walikuwa wakimsikia,” alisema Bw Ntabo.

Kulingana naye, ni wanafunzi wachache ambao huadhibiwa baada ya kuwepo na maelewano na wazazi wao.

“Ni mapenzi ya mzazi tu. Ni wachache ambao hushirikiana na walimu ili kuhakikisha watoto wao wanasalia kuwa na mienendo bora,” aliongeza Bw Ntabo.

Shule anayofunza Bi Carolyne Kimani| PICHA| FRIDAH OKACHI

Mwalimu wa shule ya msingi, mjini Nairobi Bi Carolyne Kimani alilalamikia wazazi kudekeza wanao hadi masomoni. Kando na kufunza wajibu wake ukisalia kuandika kwenye shajara ili kuwasilisha ujumbe kumfikia mzazi.

“Kazi yetu imesalia kuangalia shajara, kuandika na kutia sahihi tu. Mwanafunzi akija kama hajafanya kazi ya ziada kutoka nyumbani, nitaandika ujumbe kumfahamisha mzaziwe. Ukisema unamwadhibu yule mtoto kwa kumpanga jinsi anavyofaa kufanya utalaumiwa bure,” alisema Bi Kimani.

Alilalamikia kwa wakati mmoja jinsi mzazi alimtumia ujumbe wa kumwonya kumpa mwanawe kazi ya ziada akidai inamchosha vidole.

“Kabla muhula kuanza, mzazi aliandika kwenye shajara kuwa nahitaji kuwacha kumpa mwanawe kazi ya ziada ambayo ni nyingi. Alisema nampa mwanawe kazi nyingi na yenye uzito. Baada ya wiki mbili alikuja kuniuliza mbona tena sipeani kazi ya ziada,” alifedheheka Bi kimani.

Mtaa wa Waruku, eneo bunge la Dagoretti Kaskazini mzazi Anne Nagaya alikosoa walimu kwa wakati mwingine kujiweka kwenye kiwango cha watakatifu kisha kujifanya kuwa waathiriwa.

Kulingana nay eye, mbinu hii ya kufunza na kuondoka imeathiri wanafunzi wengi wakiwemo wanawe. Pia, alilazimika kufanya uchunguzi wa kina.

“Sikatai kuwa mwanangu alifanya kosa, lakini mwalimu kuzungumza maneno ambayo hayafurahishi kwenye masikio ya mwanagu ni tatizo. Kila wakati akifanya kosa lazima azungumze kwa namna ya kumtusi kulingana na maumbile yake,” alisema Bi Nagaya.

Mwenyekiti wa wazazi nchini, Bw Nicholus Maiyo, aliambia Taifa Leo, kwamba mwanzo kulikuwepo na changamoto ya walimu kushindwa watafanya vipi. Lakini kwa sasa kuna wale wametafuta mbinu mwafaka ya kuhakikisha mwanafunzi anaadhibiwa na bado anasalia shuleni.