'Serikali ya Rais Kenyatta ilenge kuwainua vijana kimaisha'
Na SAMMY WAWERU
AWAMU ya pili na ya mwisho ya Rais Uhuru Kenyatta ameweka wazi kuwa siasa ziegeshwe kando, Wakenya wafanyiwe maendeleo.
Ni tamko alilolielekezea kila kiongozi, hasa baraza lake la mawaziri na ambao ni macho na mikono yake katika kazi. Baada ya kuhifadhi kiti chake katika uchaguzi wa 2017, si mara moja ama mbili ameonya mawaziri kuwa “kila mmoja atabeba mzigo wake” ikiwa idara anayoongoza itazembea kazini, pamoja na kutumia ofisi vibaya na kufuja mali ya umma.
Rais Kenyatta amezipa kipaumbele ajenda kuu nne, ambazo ni; matibabu bora kwa wote, ujenzi wa viwanda, usalama wa chakula na makazi nafuu.
Ni nguzo ambazo naibu wake Dkt William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanazipigia debe.
Viwanda
Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wamebashiri hatua hii kama njia ya kuhakikisha Rais ameacha rekodi bora ya utendakazi, atakapostaafu 2022.
Katika ajenda ya ujenzi wa viwanda, Rais Kenyatta amesema inapania kutatua suala la ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana.
Ikumbukwe kwamba kati ya Wakenya milioni 45, idadi kubwa ni vijana na wengi kupata kazi imekuwa kitendawili.
Maelfu hufuzu kwa vyeti mbalimbali vya masomo katika taasisi za juu za elimu, ikiwamo vyuo vikuu.
Hawa wote, sharti gurudumu la maisha lisukumwe, liwe liwalo.
Rais amenukuliwa akikashifu wanaotaka nyongeza ya mishahara na marupurupu, ghadhabu akizielekeza kwa wauguzi wanaogoma, akihoji serikali haina pesa kuafikia matakwa yao.
Huu ujenzi wa viwanda unahitaji ufadhili wa kutosha, na ni bayana haiwezekani maeneo yote kuvipata kabla na baada ya hatamu ya Kenyatta kukamilika. Sijui, huenda basi yakapata kabla ya muda wa Ruwaza ya 2030 kukamilika.
Kiongozi wa nchi amekuwa akifanya ziara katika mataifa mbalimbali ulimwenguni kwa kile kimetajwa kama kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Kenya na mataifa hayo.
Ziara hizo pia zimelenga kustawisha sekta ya biashara na utalii, kati ya nchi hii na mataifa hayo. Sababu kuu ikiwa kupiga jeki uchumi.
Ushauri wa mtaalamu wa uchumi
Sekta ya biashara ndogondogo na zile za wastani (SMEs) imeonesha wazi ina uwezo wa kusitiri asilimia kubwa ya wananchi. Mwaka uliopita, Rais alisema SME imebuni nafasi za kazi kwa zaidi ya asilimia 75 ya Wakenya.
Alisema sekta hii ni kitega uchumi kikuu cha serikali, akisisitiza haja ya serikali kuu na zile za kaunti kushirikiana kuiinua.
“Jamii ya SME imewakilisha asilimia 75 ya ajira zinazofanywa nchini, tunahitaji kuwa na kikao tuone tutakavyoiinua. Sekta hii inatudai,” alisema Rais akihutubu katika kongamano lililoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Strathmore, jijini Nairobi na wadau wa SMEs.
Biashara hizi ndogondogo maarufu juakali, ndicho chanzo hasa cha bidhaa zinazotumika nchini.
“Kwa mujibu wa historia ya mataifa yaliyobobea kibiashara na kuwa na viwanda tajika duniani, yalianza kupitia SMEs,” akasema Michael Muriuki, mtaalamu wa masuala ya kiuchumi na biashara kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali.
Kulingana na mdau huyu, mbali na ahadi za Rais kuimarisha sekta hii, anapaswa kutekeleza kila kitu kwa matendo.
Taifa hili lina raslimali ya kutosha kujiendeleza kimaendeleo, na Bw Muriuki anasema ziara za Kenyatta katika mataifa ya nje zinafaa kufungua nafasi ya soko ya bidhaa.
Ardhi za umma zilizonyakuliwa na wahuni na kurejeshwa na serikali, zikiundwa maduka madogomadogo, zitafaa SME kwa kiasi kikubwa. Muriuki anasema si lazima majengo makubwa yafanywe ili kuunda viwanda, ikizingatiwa kwamba serikali inadai haina fedha.
“Palipo na ardhi inayomilikiwa na umma, serikali iunde maduka ya kukodi, wananchi wawekeze katika biashara. Itapata ushuru, na wananchi watajiimarisha. Nafasi nyingi za kazi zitajiri,” ashauri mtaalamu huyu.
Talanta
Kandokando mwa barabara kuu, mita chache husemekana ni mali ya serikali, ardhi hizo zikiundwa maduka, vijana wanaofuzu vyuoni wataweza kujiajiri kwa kuweka biashara. Kuna wengi waliojaaliwa talanta mbalimbali za sanaa, kama utengenezaji wa bidhaa za urembo na utanashati, zinazodumisha utamaduni wetu kama shanga na mavazi, zikiwa chache tu kuzitaja.
Moses Mwangi, mtengenezaji wa bidhaa za shanga anasema sanaa si kitega uchumi pekee, ila ni kivutio cha watalii nchini. “Wengi wamejaaliwa vipaji mbalimbali vya usanii, kila mmoja ni kivutio cha watalii kwa njia yake,” asema Bw Mwangi.
Kauli yake inawiana na ya Beatrice Mwaura, msusi wa mikeka kwa nyuzi.
Hata hivyo, Beatrice anasema kinacholemaza wengi kudhihirisha jitihada zao ni kukosa mahali maalumu kuendeshea gange.
Bw Kirugumi Gitonga, muundaji wa maua ya urembesho wa maskani, eneo la Mwihoko, Kiambu, anasema amenoa vijana wengi kupitia karakana yake ndogo, na iwapo angepata nafasi ya kutosha bila shaka sanaa yake ingeunda kiwanda.
Serikali ikiitikia kuunda maduka ya kukodisha, mbali na kutumika kuendesha biashara, yatakuwa karakana ya waliojaaliwa kisanaa.
“Maduka hayo yasawazishwe kodi ambayo vijana watamudu, kwa mfano Sh1,500 kila mwezi. Serikali itashangaa kuona vijana waliojaaliwa vipaji katika sanaa wakijitokeza na kujiajiri, huu ndio mkondo wa kuanzisha viwanda na lalama za ukosefu wa kazi zitapungua,” aeleza Muriuki, mtaalamu wa masuala ya biashara na uchumi. Anaongeza kusema kwamba, serikali ihimize mashirika ya kifedha kuondoa masharti magumu yanayowanyima mikopo, ili wajiimarishe.