Serikali yalenga kudhibiti miujiza feki na shughuli potovu za kidini nchini
SERIKALI kupitia afisi ya Mkuu wa Mawaziri imeandaa mapendekezo makali yanayolenga kudhibiti shughuli za kidini nchini, ikiwemo miujiza feki, hatua inayozua mjadala kati ya serikali na viongozi wa dini.
Rasimu mbili, moja ikiwa Sera ya Mashirika ya Kidini ya 2024 na Mswada wa Mashirika ya Kidini wa 2024, zinanuiwa kutoa mfumo wa kisheria wa kusimamia mashirika ya kidini, kukabiliana na misimamo mikali ya kidini, na kuzuia matumizi mabaya ya uhuru wa kuabudu.
Kwa mujibu wa serikali, rasimu hizo zimetokana na mapendekezo ya Kamati Maalum ya Rais ya kuchunguza Mfumo wa Kisheria wa Mashirika ya Kidini, iliyoongozwa na Mchungaji Mutava Musyimi.
Kamati hiyo iliundwa baada ya mkasa wa Shakahola uliotikisa taifa, ambapo zaidi ya watu 500 walipoteza maisha wakifuata mafundisho ya kiongozi wa kidini anayedai kuwa nabii, Paul Mackenzie, aliyewashawishi wafuasi wake kufa kwa njaa ili “kukutana na Yesu.”
Serikali inasema kwamba mswada huo mpya unalenga kuzuia Wakenya kuangukia mikononi mwa walaghai wanaojifanya watumishi wa Mungu lakini wanaendesha ibada hatari na kujinufaisha kifedha kwa njia ya udanganyifu.
Miongoni mwa vifungu vilivyopendekezwa, Kifungu cha Saba cha mswada huo kinasema wazi kuwa taasisi yoyote ya kidini haitaruhusiwa kushiriki au kuendesha shughuli za kisiasa kwa lengo la kuleta ushawishi wa kisiasa au kuunga mkono chama cha kisiasa au mgombeaji.
Kukiuka kifungu hicho kutasababisha faini isiyozidi Sh500,000 au kifungo cha miezi sita, au adhabu zote mbili.Kuhusu ibada hatari na itikadi kali, mswada unapiga marufuku mtu yeyote kulazimisha, kutisha au kumdanganya mwingine kushiriki ibada au mafundisho yanayoweza kuhatarisha afya, usalama au maisha.
Atakayepatikana na hatia atatozwa faini ya hadi Sh5 milioni au kifungo cha miaka 20, au vyote viwili.
Pia, mswada unakataza mtu yeyote kutumia vitisho, udanganyifu, au nguvu kumshawishi mtu ajiunge na dini fulani au kumzuia kuiacha. Adhabu kwa kosa hilo ni faini ya hadi Sh1 milioni au kifungo cha miaka mitatu.
Hata hivyo, unapendekeza kwamba mzazi au mlezi halali hatashtakiwa iwapo ataelekeza mtoto wake katika imani au maadili ya dini fulani, kwa kuwa jukumu hilo linatambuliwa na Katiba.
Zaidi ya hayo, viongozi wa dini wanaotumia miujiza ya uongo, baraka au maombi bandia kwa nia ya kupata fedha au mali kutoka kwa waumini, watakabiliwa na adhabu kali ya faini isiyozidi Sh5 milioni au kifungo cha miaka 10, au zote mbili.
Kifungu kingine kinasema kuwa mtu yeyote atakayejificha chini ya mwavuli wa dini na kudhalilisha imani ya wengine au kufanya jambo lolote linaloweza kuhatarisha maisha, afya au usalama wa mtu mwingine atatozwa faini ya hadi Sh5 milioni au kifungo cha miaka 20.
Mswada huo unapendekeza kuundwa kwa Tume ya Masuala ya Kidini itakayokuwa na mamlaka ya kisheria na uwezo wa kudumu.
Tume hiyo itahusika na usajili wa makanisa, misikiti na mashirika ya kidini, pamoja na kuandaa kanuni za maadili na uendeshaji wa taasisi hizo.
Tume pia itakuwa na jukumu la kufuatilia shughuli za viongozi wa dini, kuhakikisha wanazingatia maadili, uwazi wa kifedha na kanuni za utawala bora.
Hata hivyo, pendekezo hilo limekumbana na upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa makanisa na taasisi za Kiislamu.
Baraza la Makanisa na Wahubiri wa Kenya (CCAK) lilimtaka Rais William Ruto kuingilia kati na kusitisha rasimu hiyo, hadi wadau wote wa kidini watakaposhirikishwa ipasavyo.
“Katiba iko wazi kwamba serikali na dini ni vitu viwili tofauti.
Tunashangaa kwa nini serikali inataka kudhibiti taasisi za kidini huku ikipendekeza adhabu kali za kifungo na faini,” alisema Askofu Hudson Ndeda, mwenyekiti wa CCAK.
Askofu Ndeda aliongeza kuwa serikali inaonekana kutaka kudhibiti mahubiri ya mtandaoni, televisheni za Kikristo na hata kuwatisha wachungaji ili wasiwe huru kufundisha mafundisho yao.
Kanisa la Deliverance, Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya (Supkem), pamoja na mashirika mengine ya kidini, pia yamelaani mswada huo yakisema kuwa hauakisi maoni yao waliyowasilisha kwa kamati ya Mutava Musyimi.
Viongozi wa dini wanasema badala ya kuweka sheria kandamizi, serikali inapaswa kuimarisha elimu ya umma kuhusu dini potovu na kuwekeza katika ushirikiano na viongozi wa kweli wa dini.