Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Aliniambia ataoa mke wa pili kulingana na desturi

July 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SHANGAZI

KWAKO Shangazi. Nina umri wa miaka 23 na niliolewa majuzi tu. Sasa ndio tunajiandaa kupata mtoto wetu wa kwanza lakini kuna jambo ambalo mume wangu aliniambia hivi majuzi nikaingiwa na wasiwasi. Aliniambia kuwa kulingana na desturi ya jamii yake, mwanamume hawezi kuwa na mke mmoja. Nilimuuliza iwapo yeye pia anafuata desturi hiyo akaniambia ni lazima hatimaye ataoa mke wa pili. Sijawahi kufikiria kuwa na mke-mwenza na sitakubali. Nafikiria kumuacha. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninaamini mume wako alikufahamisha hayo ili kukuandaa mapema kwa jambo hilo. Lakini alichelewa. Angekwambia bado mkiwa wapenzi, hungekubali kuolewa naye kwa sababu unasema huwezi kuishi na mke-mwenza. Ni vyema umejua kabla hamjapata watoto. Kama huo ndio msimamo wako, sidhani kuna nafasi ya kushauriana kwa sababu amekwambia wazi kuwa ni lazima ataoa mke mwingine. Itakuwa heri kwako kutoka sasa. Umri wako bado ni mdogo, utaolewa tena.

 

Tulijuana kiajali

Kwako Shangazi. Kuna mwanamke aliyenipigia simu kimakosa na tangu wakati huo tumekuwa tukiwasiliana. Sasa tumejuana kwa mwaka mmoja ingawa hatujaonana. Ameniambia ananipenda nami pia nampenda na yuko tayari tukutane. Kabla ya kufanya hivyo nimeamua kutafuta ushauri wako.

Kupitia SMS

Haiwezekani kamwe kwa watu kupendana kupitia kwa simu kama hawajaonana hata siku moja. Hisia za kimapenzi hutokana na mtu kuona mwingine ana kwa ana. Madai yenu eti mnapendana ni dhana tu. Ni vyema kwamba mmepanga kuonana na huo pia ndio ushauri wangu. Ni baada ya hapo ambapo mtajua ukweli wa hisia za kila mmoja wenu kwa mwenzake.

 

Anakamia asali yangu

Vipi Shangazi? Niko katika uhusiano mchanga, haujamaliza hata mwaka lakini mpenzi wangu amekuwa akitaka kuonja asali akidai eti hatua hiyo itaongezea zaidi mapenzi yake kwangu. Je, ni kweli?

Kupitia SMS

Madai ya mpenzi wako hayana ukweli hata kidogo. Nahisi kuwa nia yake hasa ni hiyo asali na anataka kutumia ujanja huo ili aipate kisha akutoroke. Mapenzi ya dhati katika uhusiano yanafaa kunoga na kudumu hata bila hiyo asali hadi wawili kufunga ndoa. Kama unavyosema, uhusiano wenu ni mchanga sana na ni ajabu kwamba mwenzako tayari adai hilo kutoka kwako. Usikubali.

 

Nashuku lengo lake

Hujambo Shangazi? Nilikuwa nimeolewa lakini mume wangu akaaga dunia na kuniachia watoto wetu wanne. Sasa kuna mwanamume anayetaka kunioa lakini mimi nimejitegemea kimaisha. Nina biashara nzuri na ninaishi kwangu. Mimi pia nampenda lakini ninashuku labda anavutiwa na mali yangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Mali yako ni yako na hakuna anayeweza kukunyang’anya. Iwapo umetosheka kuwa mwanamume huyo anakupenda kwa dhati nawe pia unampenda, huna sababu ya kumshuku. Mpe nafasi hiyo. Ukigundua baadaye kuwa shabaha yake ni mali yako, una haki ya kumpiga teke.

 

Kisura aliniacha ghafla

Shikamoo Shangazi! Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana fulani kwa mwaka mmoja sasa. Juzi alinishangaza sana aliponiambia kuwa amebadili nia yake kwangu eti ameamua kumrudia mpenzi wake wa awali. Ninampenda sana na sijui nitafanya nini.

GEORGE, Nakuru

Uhusiano wa kimapenzi ni chaguo la mtu binafsi na mhusika ana haki ya kujiondoa wakati wowote akiamua kufanya hivyo. Huenda msichana huyo ameona upungufu fulani kwako ndipo akaamua kukuacha na kumrudia mpenzi wake wa awali. Kubali uamuzi wake huo ili uweze kumuondoa katika mawazo yako na kutafuta mwingine.

 

Wake wawili ni zigo

Nina umri wa miaka 32 na nina wake wawili. Wa kwanza nimeishi naye zaidi ya miaka sita na tumezaa watoto watatu. Huyu wa pili tuna mwaka mmoja unusu na tumepata mtoto mmoja. Tatizo ni kwamba, hataki kunisikiliza. Mtoto akiwa mgonjwa hataki kumpeleka hospitali ama kliniki. Ingawa ameokoka, mtoto bado anateseka. Naomba unisaidie.

Iwapo umeshindwa kusikilizana naye, inawezekana unahitaji usaidizi wa wazee ama watu wazima katika familia zenu ili kuweza kuelewana na mkeo. Kwani yawezekana kuna mambo mengine yanayoendelea baina yenu ambayo yanamuumiza mkeo na anatenda ayatendayo ikiwa ni njia ya kufikisha ujumbe kwako.